Kipindi cha 4: Tangu Kuingia Kanaani Hadi Kifo cha Daudi
Tangu Waisraeli walipoingia Kanaani chini ya uongozi wa Yoshua, hadi kifo cha Daudi.
Sehemu ya 1: Kutekwa kwa Kanaani
Kukabidhiwa kwa Yoshua Wajibu
1451 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Baada ya kifo cha Mose mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua mwana wa Nuni, msaidizi wa Mose: 2 “Mtumishi wangu Mose amekufa. Sasa basi, wewe pamoja na watu wote hawa, jiandaeni kuvuka huu Mto Yordani kuingia nchi ambayo karibu nitawapa wana wa Israeli. 3 Kila mahali nyayo za miguu yenu zitakapokanyaga nimewapa, kama vile nilivyomwahidi Mose. 4 Nchi yenu itaenea kuanzia jangwa hili hadi Lebanoni, tena kuanzia mto mkubwa wa Frati, yaani nchi yote ya Wahiti, hadi Bahari ile Kubwa iliyoko upande wa magharibi. 5 Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.
6 “Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”
Yoshua Atuma Wapelelezi
1 Kisha Yoshua mwana wa Nuni kwa siri akawatuma wapelelezi wawili kutoka Shitimu, akawaambia, “Nendeni mkaikague hiyo nchi, hasa Yeriko.” Kwa hiyo wakaenda na kuingia kwenye nyumba ya kahaba mmoja jina lake Rahabu na kukaa humo.
2 Mfalme wa Yeriko akaambiwa, “Tazama! Baadhi ya Waisraeli wamekuja huku usiku huu kuipeleleza nchi.” 3 Hivyo mfalme wa Yeriko akatuma huu ujumbe kwa Rahabu: “Watoe wale watu waliokujia na kuingia nyumbani mwako, kwa sababu wamekuja kuipeleleza nchi yote.”
4 Lakini huyo mwanamke alikuwa amewachukua hao watu wawili na kuwaficha. Akasema, “Naam, watu hao walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka. 5 Kulipoingia giza, wakati wa kufunga lango la mji, watu hao waliondoka. Sijui njia waliyoiendea. Wafuatilieni haraka. Huenda mkawapata.” 6 (Lakini alikuwa amewapandisha darini akawafunika kwa mabua ya kitani aliyokuwa ameyatandika darini.) 7 Basi hao watu wakaondoka kuwafuatilia hao wapelelezi katika njia ile inayoelekea vivuko vya Yordani, mara tu wafuatiliaji walipotoka nje, lango likafungwa.
8 Kabla wale wapelelezi hawajalala, Rahabu akawaendea huko juu darini, 9 akawaambia, “Ninajua kuwa Bwana amewapa nchi hii na hofu kuu imetuangukia kwa sababu yenu, kiasi kwamba wote waishio katika nchi hii wanayeyuka kwa hofu kwa sababu yenu. 10 Tumesikia jinsi Bwana alivyokausha maji ya Bahari ya Shamu kwa ajili yenu mlipotoka Misri, pia lile mlilowatendea Sihoni na Ogu, wafalme wawili wa Waamori mashariki mwa Yordani, ambao mliwaangamiza kabisa. 11 Tuliposikia juu ya hili, mioyo yetu iliyeyuka na kila mmoja alikosa ujasiri kwa sababu yenu, kwa maana Bwana Mungu wenu ni Mungu juu mbinguni na duniani chini. 12 Sasa basi, tafadhali niapieni kwa Bwana, kwamba mtaitendea hisani jamaa ya baba yangu, kwa kuwa mimi nimewatendea hisani. Nipeni ishara ya uaminifu 13 kwamba mtayahifadhi maisha ya baba yangu na mama yangu, ndugu zangu wa kiume na wa kike, pamoja na wale wote walio wa kwao na kwamba mtatuokoa na kifo.”
14 Wale watu wakamhakikishia Rahabu, “Uhai wetu kwa uhai wenu! Ikiwa hutatoa habari ya nini tunachofanya, wakati Bwana atakapotupa nchi hii, tutawatendea kwa hisani na kwa uaminifu.”
15 Kisha akawateremsha dirishani kwa kamba, kwa kuwa nyumba yake aliyokuwa anaishi ilikuwa sehemu ya ukuta wa mji. 16 Alikuwa amewaambia, “Nendeni vilimani ili wale wafuatiliaji wasiwapate. Jificheni huko kwa siku tatu mpaka watakaporudi, hatimaye mwende zenu.”
17 Wale watu wakamwambia, “Hiki kiapo ulichotuapisha hakitatufunga, 18 isipokuwa, hapo tutakapoingia katika nchi hii, utakuwa umefunga hii kamba nyekundu dirishani pale ulipotuteremshia na kama utakuwa umewaleta baba yako na mama yako, ndugu zako na jamaa yako yote ndani ya nyumba yako. 19 Ikiwa mtu yeyote atatoka nje ya nyumba yako akaenda mtaani, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe, hatutawajibika. Lakini yule ambaye atakuwa ndani pamoja nawe, kama mkono wa mtu yeyote ukiwa juu yake damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu. 20 Lakini ikiwa utatoa habari ya shughuli yetu tunayofanya, tutakuwa tumefunguliwa kutoka kwenye kiapo hiki ulichotufanya tuape.”
21 Naye akajibu, “Nimekubali. Na iwe kama mnavyosema.” Kwa hiyo akaagana nao, nao wakaondoka. Yeye akaifunga ile kamba nyekundu dirishani.
22 Walipoondoka, wakaelekea vilimani na kukaa huko siku tatu, hadi wale waliokuwa wakiwafuatilia wakawa wamewatafuta njia nzima na kurudi pasipo kuwapata. 23 Ndipo wale watu wawili wakaanza kurudi. Wakashuka kutoka kule vilimani, wakavuka mto na kuja kwa Yoshua mwana wa Nuni, na kumweleza kila kitu kilichowapata. 24 Wakamwambia Yoshua, “Hakika Bwana ametupa nchi yote mikononi mwetu; watu wote wanayeyuka kwa hofu kwa sababu yetu.”