Kuvuka Yordani

1451 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yoshua 1:10–18

10 Ndipo Yoshua akawaagiza maafisa wa watu akisema, 11 “Pitieni katika kambi yote mkawaambie watu, ‘Wekeni tayari mahitaji yenu. Siku tatu kuanzia sasa mtavuka hii Yordani ili kuingia na kuimiliki nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa iwe yenu wenyewe.’ ”

12 Lakini kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, Yoshua akasema, 13 “Kumbukeni agizo lile Mose mtumishi wa Bwana alilowapa: ‘Bwana Mungu wenu anawapa ninyi raha, naye amewapa nchi hii.’ 14 Wake zenu, watoto wenu na mifugo yenu watakaa katika nchi ile Mose aliyowapa mashariki ya Yordani, lakini mashujaa wenu wote, wakiwa wamevikwa silaha kikamilifu lazima wavuke mbele ya ndugu zenu. Imewapasa kuwasaidia ndugu zenu hadi 15 Bwana awape nao raha, kama alivyokwisha kufanya kwa ajili yenu hadi wao pia watakapokuwa wamemiliki nchi ile Bwana Mungu wenu anayowapa. Baada ya hilo, mwaweza kurudi na kukalia nchi yenu wenyewe, ambayo Mose mtumishi wa Bwana aliwapa mashariki mwa Yordani kuelekea linakochomoza jua.”

16 Ndipo wakamjibu Yoshua, “Chochote ambacho umetuagiza tutafanya na popote utakapotutuma tutakwenda. 17 Kama vile tulivyomtii Mose kikamilifu, ndivyo tutakavyokutii wewe. Bwana Mungu wako na awe pamoja nawe tu kama vile alivyokuwa pamoja na Mose. 18 Yeyote atakayeasi neno lako na kuacha kuyatii maneno yako, au chochote utakachowaamuru, atauawa. Uwe imara na hodari tu!”

Yoshua 3–4

1 Yoshua na Waisraeli wote wakaondoka asubuhi na mapema kutoka Shitimu, wakaenda mpaka Mto Yordani, ambako walipiga kambi kabla ya kuvuka. 2 Baada ya siku tatu maafisa wakapita katika kambi yote, 3 wakitoa maagizo kwa watu, wakiwaambia: “Mtakapoona Sanduku la Agano la Bwana Mungu wenu, likichukuliwa na Walawi ambao ndio makuhani, mtaondoka hapo mlipo na kulifuata. 4 Ndipo mtakapotambua njia mtakayoiendea, kwa kuwa hamjawahi kuipita kabla. Lakini msisogee karibu, bali kuwe na umbali wa dhiraa 2,000 kati yenu na Sanduku.”

5 Ndipo Yoshua akawaambia hao watu, “Jitakaseni, kwa kuwa kesho Bwana atatenda mambo ya kushangaza katikati yenu.”

6 Yoshua akawaambia makuhani, “Liinueni Sanduku la Agano mkatangulie mbele ya watu.” Hivyo wakaliinua na kutangulia mbele yao.

7 Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Leo nitaanza kukutukuza machoni pa Israeli yote, ili wapate kujua kuwa niko pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Mose. 8 Uwaambie makuhani wanaochukua Sanduku la Agano, ‘Mnapofika kwenye ukingo wa maji ya Yordani, nendeni mkasimame ndani ya mto.’ ”

9 Yoshua akawaambia Waisraeli, “Njooni hapa msikilize maneno ya Bwana Mungu wenu. 10 Hivi ndivyo mtakavyojua ya kuwa Mungu aliye hai yupo katikati yenu, na kwamba kwa hakika atawafukuza mbele yenu hao Wakanaani, Wahiti, Wahivi, Waperizi, Wagirgashi, Waamori na Wayebusi. 11 Tazameni, Sanduku la Agano la Bwana wa dunia yote litaingia ndani ya Mto Yordani likiwa limewatangulia. 12 Sasa basi, chagueni watu kumi na wawili kutoka makabila ya Israeli, mtu mmoja kutoka kila kabila. 13 Mara tu nyayo za makuhani walichukualo Sanduku la Bwana, Bwana wa dunia yote, zitakapokanyaga ndani ya Mto Yordani, maji hayo yatiririkayo kutoka juu yatatindika na kusimama kama chuguu.”

14 Basi, watu walipovunja kambi ili kuvuka Yordani, makuhani wakiwa wamebeba Sanduku la Agano waliwatangulia. 15 Wakati huu ulikuwa wakati wa mavuno, nao Mto Yordani ulikuwa umefurika hadi kwenye kingo zake. Ilikuwa kawaida ya Yordani kufurika nyakati zote za mavuno. Mara tu makuhani wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Agano walipofika mtoni na nyayo zao kuzama ndani ya yale maji, 16 maji hayo yaliyotiririka kutoka upande wa juu yaliacha kutiririka yakasimama kama chuguu mbali kabisa nao, kwenye mji ulioitwa Adamu kwenye eneo la Sarethani, wakati yale maji yaliyokuwa yanatiririka kuingia kwenye Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), yalitindika kabisa. Hivyo watu wakavuka kukabili Yeriko.

17 Wale makuhani waliobeba Sanduku la Agano la Bwana, wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Mto Yordani, wakati Waisraeli wote wakiwa wanapita hadi taifa lote likaisha kuvuka mahali pakavu.

4:1 Wakati taifa lote lilipokwisha kuvuka Mto Yordani, Bwana akamwambia Yoshua, 2 “Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa watu, kila kabila mtu mmoja, 3 nawe uwaambie wachukue mawe kumi na mawili katikati ya Mto Yordani, palepale makuhani waliposimama, wayachukue na kuyaweka mahali mtakapokaa usiku huu wa leo.”

4 Basi Yoshua akawaita watu kumi na wawili ambao alikuwa amewachagua kutoka miongoni mwa Waisraeli, mtu mmoja kutoka kila kabila, 5 naye akawaambia, “Mtangulie mbele ya Sanduku la Bwana Mungu wenu, mwende katikati ya Mto Yordani. Kila mmoja wenu atainua jiwe begani mwake, kufuatana na hesabu ya makabila ya Waisraeli, 6 kuwa kama ishara katikati yenu. Siku zijazo, wakati watoto wenu watakapowauliza, ‘Ni nini maana ya mawe haya?’ 7 waambieni kwamba maji ya Mto Yordani yaliyokuwa yakitiririka yalitindika mbele ya Sanduku la Agano la Bwana. Wakati lilipovuka Yordani, maji ya Yordani yalitindika. Mawe haya yatakuwa kumbukumbu kwa watu wa Israeli milele.”

8 Hivyo Waisraeli wakafanya kama Yoshua alivyowaagiza. Wakachukua mawe kumi na mawili kutoka katikati ya Mto Yordani, kulingana na hesabu ya kabila za Waisraeli kama Bwana alivyomwambia Yoshua, nao wakayabeba hadi kambini mwao, mahali walipoyatua chini. 9 Yoshua akayasimamisha yale mawe kumi na mawili ambayo yalikuwa katikati ya Mto Yordani, mahali pale ambapo miguu ya makuhani waliobeba Sanduku la Agano iliposimama. Nayo yako huko mpaka leo.

10 Makuhani waliobeba lile Sanduku walibakia wakiwa wamesimama katikati ya Mto Yordani mpaka kila kitu Bwana alichomwamuru Yoshua kilipokuwa kimefanywa na watu, sawasawa na vile Mose alivyokuwa amemwamuru Yoshua. Watu wakafanya haraka kuvuka, 11 na mara tu watu wote walipokwisha kuvuka, Sanduku la Bwana na makuhani wakavuka watu wakiwa wanatazama. 12 Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakavuka mbele ya Waisraeli, wakiwa wamevaa silaha, kama Mose alivyowaamuru. 13 Kiasi cha watu 40,000 waliojiandaa kwa vita walivuka mbele za Bwana hadi nchi tambarare za Yeriko kwa ajili ya vita.

14 Siku ile Bwana akamtukuza Yoshua mbele ya Israeli yote, nao wakamheshimu siku zote za maisha yake, kama vile walivyomheshimu Mose.

15 Basi Bwana akamwambia Yoshua, 16 “Waamuru hao makuhani wanaolibeba Sanduku la Ushuhuda, wapande kutoka ndani ya Mto Yordani.”

17 Kwa hiyo Yoshua akawaamuru hao makuhani akisema, “Pandeni kutoka ndani ya Mto Yordani.”

18 Nao makuhani wakapanda kutoka ndani ya Mto Yordani wakilibeba hilo Sanduku la Agano la Bwana. Mara tu walipoiweka miguu yao penye kingo, nje ya mto, maji ya Yordani yakarudi kufurika kama ilivyokuwa kabla.

19 Siku ya kumi ya mwezi wa kwanza watu walipanda kutoka Yordani na kupiga kambi huko Gilgali, kwenye mpaka wa mashariki ya Yeriko. 20 Naye Yoshua akayasimamisha huko Gilgali yale mawe kumi na mawili ambayo walikuwa wameyachukua katikati ya Mto Yordani. 21 Akawaambia Waisraeli, “Wazao wenu watakapowauliza baba zao siku zijazo wakisema, ‘Mawe haya maana yake ni nini?’ 22 Basi waambieni, ‘Israeli ilivukia mahali pakavu katika Mto Yordani.’ 23 Kwa maana Bwana Mungu wenu alikausha maji ya Yordani mbele yenu, hadi mlipomaliza kuvuka. Bwana Mungu wenu alifanya haya kwa Mto Yordani sawasawa na kile alichoifanyia Bahari ya Shamu wakati alipoikausha mbele yetu hadi tulipomaliza kuvuka. 24 Alifanya hivi ili kwamba mataifa yote ya dunia yapate kujua kuwa mkono wa Bwana ni wenye nguvu, na ili kwamba kila wakati mpate kumcha Bwana Mungu wenu.”