Mose Apanda Mlima Nebo Ili Afe
1451 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
48 Siku hiyo hiyo Bwana akamwambia Mose, 49 “Kwea katika mapangano ya Mlima Abarimu hadi kilima cha Nebo kilichoko Moabu, ngʼambo ya Yeriko, na uitazame Kanaani, nchi ninayowapa Waisraeli kama milki yao wenyewe. 50 Utafia kwenye mlima huo unaokwea na kukusanyika pamoja na watu wako, kama ndugu yako Aroni alivyofia juu ya Mlima Hori naye akakusanyika kwa watu wake. 51 Hii ni kwa sababu ninyi wawili mlivunja uaminifu nami mbele ya Waisraeli kwenye maji ya Meriba-Kadeshi katika Jangwa la Sini, na kwa sababu hamkuuinua utakatifu wangu miongoni mwa Waisraeli. 52 Kwa hiyo, utaiona tu nchi kwa mbali; wewe hutaingia nchi ninayowapa watu wa Israeli.”
Mose Abariki Watu
1 Hii ndiyo baraka Mose mtu wa Mungu aliyotamka kwa Waisraeli kabla ya kifo chake. 2 Alisema:
“Bwana alikuja kutoka Mlima Sinai,
akachomoza kama jua juu yao
kutoka Mlima Seiri,
akaangaza kutoka Mlima Parani.
Alikuja pamoja na watakatifu makumi elfu
kutoka kusini,
kutoka materemko ya mlima wake.
3 Hakika ni wewe ambaye huwapenda watu,
watakatifu wako wote wamo mkononi mwako.
Miguuni pako wote wanasujudu
na kutoka kwako wanapokea mafundisho,
4 sheria ile Mose aliyotupa sisi,
tulio milki ya kusanyiko la Yakobo.
5 Alikuwa mfalme juu ya Yeshuruni
wakati viongozi wa watu walipokusanyika,
pamoja na makabila ya Israeli.
6 “Reubeni na aishi, asife,
wala watu wake wasiwe wachache.”
7 Akasema hili kuhusu Yuda:
“Ee Bwana, sikia kilio cha Yuda,
mlete kwa watu wake.
Kwa mikono yake mwenyewe hujitetea.
Naam, uwe msaada wake
dhidi ya adui zake!”
8 Kuhusu Lawi alisema:
“Thumimu yako na Urimu yako ulimpa,
mtu yule uliyemfadhili.
Ulimjaribu huko Masa
na kushindana naye
kwenye maji ya Meriba.
9 Alinena hivi kuhusu baba yake na mama yake,
‘Mimi siwahitaji kamwe.’
Akawasahau jamaa zake,
asiwatambue hata watoto wake,
lakini akaliangalia neno lako
na kulilinda Agano lako.
10 Humfundisha Yakobo mausia yako
na Israeli sheria yako.
Hufukiza uvumba mbele zako
na sadaka nzima za kuteketezwa
juu ya madhabahu yako.
11 Ee Bwana, bariki ustadi wake wote,
nawe upendezwe na kazi ya mikono yake.
Vipige viuno vya wale wainukao dhidi yake;
wapige adui zake hata wasiinuke tena.”
12 Kuhusu Benyamini akasema:
“Mwache mpenzi wa Bwana
apumzike salama kwake,
kwa maana humkinga mchana kutwa,
na yule Bwana ampendaye
hupumzika kati ya mabega yake.”
13 Kuhusu Yosefu akasema:
“Bwana na aibariki nchi yake
kwa umande wa thamani
kutoka mbinguni juu,
na vilindi vya maji
vilivyotulia chini;
14 pamoja na vitu vilivyo bora sana
viletwavyo na jua,
na vitu vizuri sana vinavyoweza
kutolewa na mwezi;
15 pamoja na zawadi bora sana
za milima ya zamani
na kwa wingi wa baraka
za vilima vya milele;
16 pamoja na baraka nzuri mno
za ardhi na ukamilifu wake,
na upendeleo wake yeye
aliyeishi kwenye kichaka
kilichokuwa kinawaka moto.
Hivi vyote na vikae juu ya kichwa cha Yosefu,
juu ya paji la uso la aliye mkuu
miongoni mwa ndugu zake.
17 Katika fahari yeye ni kama fahali mzaliwa wa kwanza;
pembe zake ni pembe za nyati,
na kwa pembe hizo atapiga mataifa,
hata yaliyo miisho ya dunia.
Hivyo ndivyo yalivyo makumi elfu ya Efraimu;
hivyo ndivyo yalivyo maelfu ya Manase.”
18 Kuhusu Zabuloni akasema:
“Shangilia, Zabuloni, wakati wa kutoka nje,
nawe Isakari, katika mahema yako.
19 Watawaita mataifa kwenye mlima,
na huko mtatoa dhabihu za haki;
watajifurahisha kwa wingi uliojaza bahari,
kwa hazina zilizofichwa mchangani.”
20 Kuhusu Gadi akasema:
“Atabarikiwa yeye aongezaye milki ya Gadi!
Gadi huishi huko kama simba,
akirarua kwenye mkono au kichwa.
21 Alijichagulia nchi nzuri kuliko zote
kwa ajili yake mwenyewe;
fungu la kiongozi lilikuwa limehifadhiwa
kwa ajili yake.
Viongozi wa watu walipokusanyika,
alitimiza haki ya mapenzi ya Bwana,
na hukumu zake kuhusu Israeli.”
22 Kuhusu Dani akasema:
“Dani ni mwana simba,
akiruka kutoka Bashani.”
23 Kuhusu Naftali akasema:
“Naftali amejaa tele upendeleo wa Bwana,
naye amejaa baraka yake;
atarithi magharibi na kusini.”
24 Kuhusu Asheri akasema:
“Aliyebarikiwa zaidi sana katika wana ni Asheri;
yeye na apate upendeleo kwa ndugu zake,
yeye na anawe miguu yake kwenye mafuta.
25 Makomeo ya malango yako yawe chuma na shaba,
nazo nguvu zako zitakuwa sawa na siku zako.
26 “Hakuna mwingine kama Mungu wa Yeshuruni,
ambaye hupanda juu ya mbingu ili akusaidie,
na juu ya mawingu katika utukufu wake.
27 Mungu wa milele ni kimbilio lako,
na chini kuna mikono ya milele.
Atamfukuza adui yako mbele yako,
akisema, ‘Mwangamize yeye!’
28 Hivyo Israeli ataishi salama peke yake.
Mzao wa Yakobo ni salama
katika nchi ya nafaka na divai mpya,
mahali ambapo mbingu
hudondosha umande.
29 Ee Israeli, wewe umebarikiwa!
Ni nani kama wewe,
taifa lililookolewa na Bwana?
Yeye ni ngao yako na msaada wako,
na upanga wako uliotukuka.
Adui zako watatetemeka mbele yako,
nawe utapakanyaga
mahali pao pa juu.”
Mose Afa, na Watu Waomboleza
1 Kisha Mose akaupanda mlima Nebo kutoka tambarare za Moabu mpaka kilele cha Pisga, ngʼambo ya Yeriko. Huko Bwana akamwonyesha nchi yote: kutoka Gileadi mpaka Dani, 2 Naftali yote, nchi ya Efraimu na Manase, nchi yote ya Yuda mpaka bahari ya magharibi, 3 Negebu na nchi yote kuanzia Bonde la Yeriko, Mji wa Mitende, hadi Soari. 4 Kisha Bwana akamwambia, “Hii ndiyo nchi niliyomwahidi Abrahamu na Isaki na Yakobo kwa kiapo niliposema, ‘Nitawapa wazao wako.’ Nimekuruhusu uione kwa macho yako, lakini hutavuka kuingia.”
5 Naye Mose mtumishi wa Bwana akafa huko Moabu, kama Bwana alivyokuwa amesema. 6 Mungu akamzika huko Moabu, katika bonde mkabala na Beth-Peori, lakini hakuna ajuaye kaburi lake lilipo mpaka leo. 7 Mose alikuwa na umri wa miaka mia moja na ishirini alipofariki; hata hivyo nguvu ya macho yake haikufifia wala mwili wake haukudhoofika. 8 Waisraeli wakaomboleza kwa ajili ya Mose kwenye tambarare za Moabu kwa siku thelathini, mpaka wakati wa kulia na kuomboleza ulipopita.
9 Basi Yoshua mwana wa Nuni alijazwa roho ya hekima kwa sababu Mose alikuwa ameweka mikono yake juu yake. Kwa hiyo Waisraeli wakamsikiliza na wakafanya yale ambayo Bwana alikuwa amemwagiza Mose.
10 Tangu wakati huo, katika Israeli hajainuka nabii mwingine kama Mose, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso, 11 aliyetenda ishara zote zile za miujiza na maajabu ambayo Bwana alimtuma kuyatenda huko Misri, yaani kwa Farao na maafisa wake wote na nchi yake yote. 12 Kwa kuwa hakuna mtu yeyote aliyewahi kuonyesha nguvu nyingi ama kutenda matendo ya kutisha ambayo Mose aliwahi kuyafanya mbele ya Israeli yote.