Ndugu za Yosefu Wanarudi, na Yakobo Anawafuata (continued)
Njaa inaendelea. Ndugu za Yosefu wanashuka kwenda Misri kwa mara ya pili, na baba yao anawafuata.
1706 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Hivyo Israeli akaondoka na vyote vilivyokuwa mali yake, naye alipofika Beer-Sheba, akamtolea dhabihu Mungu wa Isaki baba yake.
2 Mungu akanena na Israeli katika maono usiku na kusema, “Yakobo! Yakobo!”
Akajibu, “Mimi hapa.”
3 Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako, usiogope kushuka Misri, kwa maana huko nitakufanya taifa kubwa. 4 Nitashuka Misri pamoja nawe, nami hakika nitakurudisha tena Kanaani. Mikono ya Yosefu mwenyewe ndiyo itakayofunga macho yako.”
5 Ndipo Yakobo akaondoka Beer-Sheba nao wana wa Israeli wakamchukua baba yao Yakobo na watoto wao na wake zao katika magari ya kukokotwa yale Farao aliyokuwa amempelekea kumsafirisha. 6 Wakachukua pia mifugo yao na mali walizokuwa wamezipata Kanaani, Yakobo na uzao wake wote wakashuka Misri. 7 Akawachukua wanawe na binti zake, wajukuu wake wa kiume na wa kike, yaani uzao wake wote mpaka Misri.
8 Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli (Yakobo na wazao wake), waliokwenda Misri:
Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo.
9 Wana wa Reubeni ni:
Hanoki, Palu, Hesroni na Karmi.
10 Wana wa Simeoni ni:
Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani.
11 Wana wa Lawi ni:
Gershoni, Kohathi na Merari.
12 Wana wa Yuda ni:
Eri, Onani, Shela, Peresi na Zera (lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani).
Wana wa Peresi ni:
Hesroni na Hamuli.
13 Wana wa Isakari ni:
Tola, Puva, Yashubu na Shimroni.
14 Wana wa Zabuloni ni:
Seredi, Eloni na Yaleeli.
15 Hawa ndio wana wa Lea aliomzalia Yakobo huko Padan-Aramu pamoja na binti yake Dina. Jumla ya wanawe na binti zake walikuwa thelathini na watatu.
16 Wana wa Gadi ni:
Sefoni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi na Areli.
17 Wana wa Asheri ni:
Imna, Ishva, Ishvi na Beria.
Dada yao alikuwa Sera.
Wana wa Beria ni:
Heberi na Malkieli.
18 Hawa ndio watoto Zilpa aliomzalia Yakobo, ambao Labani alimpa binti yake Lea; jumla yao walikuwa kumi na sita.
19 Wana wa Raheli mke wa Yakobo ni:
Yosefu na Benyamini. 20 Huko Misri, Asenathi binti wa Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni, alimzalia Yosefu wana wawili, Manase na Efraimu.
21 Wana wa Benyamini ni:
Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu na Ardi.
22 Hawa ndio wana wa Raheli aliomzalia Yakobo; jumla yao ni kumi na wanne.
23 Mwana wa Dani ni:
Hushimu.
24 Wana wa Naftali ni:
Yaseeli, Guni, Yeseri na Shilemu.
25 Hawa walikuwa wana wa Bilha aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alikuwa amempa Raheli binti yake; jumla yao walikuwa saba.
26 Wote waliokwenda Misri pamoja na Yakobo, waliokuwa wazao wake hasa pasipo kuhesabu wakwe zake, walikuwa watu sitini na sita. 27 Pamoja na wana wawili waliozaliwa na Yosefu huko Misri, jumla yote ya jamaa ya Yakobo, waliokwenda Misri, walikuwa sabini.
28 Basi Yakobo akamtanguliza Yuda aende kwa Yosefu ili amwelekeze njia ya Gosheni. Walipofika nchi ya Gosheni, 29 gari kubwa zuri la Yosefu liliandaliwa, naye akaenda Gosheni kumlaki baba yake Israeli. Mara Yosefu alipofika mbele yake, alimkumbatia baba yake, akalia kwa muda mrefu.
30 Israeli akamwambia Yosefu, “Sasa niko tayari kufa, kwa kuwa nimejionea mwenyewe kwamba bado uko hai.”
31 Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, “Nitapanda kwa Farao na kumwambia, ‘Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa wakiishi katika nchi ya Kanaani, wamekuja kwangu. 32 Watu hao ni wachunga mifugo, huchunga mifugo, wamekuja na makundi ya kondoo, mbuzi na ngʼombe pamoja na kila kitu walicho nacho.’ 33 Farao atakapowaita na kuwaulizeni, ‘Kazi yenu ni nini?’ 34 Mjibuni, ‘Watumwa wako wamekuwa wachunga mifugo tangu ujana wetu mpaka sasa, kama baba zetu walivyofanya.’ Ndipo mtakaporuhusiwa kukaa katika nchi ya Gosheni, kwa kuwa wachunga mifugo wote ni chukizo kwa Wamisri.”
47:1 Yosefu akaenda na kumwambia Farao, “Baba yangu na ndugu zangu wamekuja kutoka nchi ya Kanaani wakiwa na makundi yao ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, pamoja na kila kitu walicho nacho, nao sasa wapo huko Gosheni.” 2 Akachagua ndugu zake watano na kuwaonyesha kwa Farao.
3 Farao akawauliza hao ndugu zake, “Kazi yenu ni nini?”
Wakamjibu, “Watumishi wako ni wachunga mifugo, kama vile baba zetu walivyokuwa.” 4 Pia wakamwambia Farao, “Tumekuja kukaa huku kwa muda mfupi, kwa sababu njaa ni kali huko Kanaani, na mifugo ya watumishi wako haina malisho. Kwa hiyo sasa, tafadhali uruhusu watumishi wako wakae huko Gosheni.”
5 Farao akamwambia Yosefu, “Baba yako na ndugu zako wamekuja kwako, 6 nayo nchi ya Misri ipo mbele yako, uwakalishe baba yako na ndugu zako katika sehemu iliyo bora kupita zote katika nchi. Na waishi Gosheni. Kama unamfahamu yeyote miongoni mwao mwenye uwezo maalum, waweke wawe wasimamizi wa mifugo yangu.”
7 Ndipo Yosefu akamleta Yakobo baba yake na kumtambulisha mbele ya Farao. Baada ya Yakobo kumbariki Farao, 8 Farao akamuuliza, “Je una umri gani?”
9 Naye Yakobo akamwambia Farao, “Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni miaka 130. Miaka yangu imekuwa michache na ya taabu, wala haikufikia miaka ya kusafiri ya baba zangu.” 10 Kisha Yakobo akambariki Farao, naye akaondoka mbele ya uso wake.
11 Ndipo Yosefu akawakalisha baba yake na ndugu zake katika nchi ya Misri na kuwapa milki katika sehemu bora sana ya nchi, wilaya ya Ramesesi, kama Farao alivyoelekeza. 12 Pia Yosefu akampa baba yake, na ndugu zake na wote wa nyumbani mwa baba yake vyakula, kwa kulingana na hesabu ya watoto wao.
Yosefu Anatawala Misri 1704 KK
13 Hata hivyo, hapakuwepo chakula katika sehemu yote kwa kuwa njaa ilikuwa kali sana; Misri na Kanaani zote zikaharibiwa kwa sababu ya njaa. 14 Yosefu akakusanya fedha zote zilizopatikana kutoka mauzo ya nafaka huko Misri na Kanaani, akazileta kwenye jumba la kifalme la Farao. 15 Fedha za watu wa Misri na Kanaani zilipokwisha, Wamisri wote wakamjia Yosefu na kumwambia, “Tupatie chakula. Kwa nini tufe mbele ya macho yako? Fedha zetu zimekwisha.”
16 Yosefu akawaambia, “Basi leteni mifugo yenu, nitawauzia chakula kwa kubadilisha na mifugo yenu, kwa kuwa fedha zenu zimekwisha.” 17 Kwa hiyo wakaleta mifugo yao kwa Yosefu, naye akawapa chakula kwa kubadilishana na farasi zao, kondoo na mbuzi zao, ngʼombe na punda zao. Katika mwaka huo wote Yosefu akawapa chakula kwa kubadilishana na mifugo yao yote.
18 Mwaka ule ulipokwisha, wakamjia mwaka uliofuata na kumwambia, “Hatuwezi kuficha ukweli mbele za bwana wetu kwamba, kwa kuwa fedha zetu zimekwisha na wanyama wetu ni mali yako, sasa hakuna chochote kilichosalia kwa ajili ya bwana wetu isipokuwa miili yetu na ardhi yetu. 19 Kwa nini tuangamie mbele ya macho yako, sisi pamoja na nchi yetu? Utununue sisi pamoja na ardhi yetu ili kubadilishana kwa chakula. Nasi pamoja na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao. Tupe sisi mbegu ili tuweze kuishi wala tusife, nchi yetu isije ikawa ukiwa.”
20 Kwa hiyo Yosefu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri. Wamisri, mmoja baada ya mwingine, waliuza mashamba yao, kwa sababu njaa ilikuwa kali sana kwao. Nchi ikawa mali ya Farao, 21 naye Yosefu akawafanya watu watumike kama watumwa, kuanzia upande mmoja wa Misri hadi upande mwingine. 22 Hata hivyo, hakununua nchi ya makuhani, kwa sababu walikuwa wanapata mgawo wao wa kawaida kutoka kwa Farao, nao walikuwa na chakula cha kuwatosha kutokana na mgawo waliopewa na Farao. Hii ndiyo sababu hawakuuza ardhi yao.
23 Yosefu akawaambia watu, “Kwa vile nimewanunua ninyi pamoja na nchi yenu leo kuwa mali ya Farao, hapa kuna mbegu kwa ajili yenu ili mweze kuziotesha. 24 Lakini wakati mazao yatakapokuwa tayari, mpeni Farao sehemu ya tano. Sehemu hizo nne zitakazobaki mtaziweka kama mbegu kwa ajili ya mashamba na kwa ajili ya chakula chenu wenyewe na cha watu wa nyumbani mwenu na watoto wenu.”
25 Wakamwambia, “Umeokoa maisha yetu. Basi na tupate kibali mbele ya macho ya bwana wetu; tutakuwa watumwa wa Farao.”
26 Basi Yosefu akaiweka iwe sheria kuhusu nchi ya Misri, ambayo inatumika mpaka leo, kwamba, sehemu ya tano ya mazao ni mali ya Farao. Ni nchi ya makuhani tu ambayo haikuwa ya Farao.