Ndugu za Yosefu Wanarudi, na Yakobo Anawafuata (continued)

Njaa inaendelea. Ndugu za Yosefu wanashuka kwenda Misri kwa mara ya pili, na baba yao anawafuata.

1706 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mwanzo 44–45

1 Kisha Yosefu akampa yule msimamizi wa nyumbani mwake maagizo haya: “Jaza magunia ya watu hawa kiasi cha chakula ambacho wanaweza kuchukua, na uweke fedha ya kila mtu kwenye mdomo wa gunia lake. 2 Kisha weka kikombe changu kile cha fedha kwenye mdomo wa gunia la yule mdogo wa wote pamoja na fedha zake ambazo angenunulia nafaka yake.” Naye akafanya kama Yosefu alivyosema.

3 Kulipopambazuka, hao watu wakaruhusiwa kuondoka pamoja na punda zao. 4 Kabla hawajafika mbali kutoka mjini, Yosefu akamwambia mtumishi wake, “Wafuatilie wale watu mara moja, utakapowakuta, waambie, ‘Kwa nini mmelipiza wema kwa ubaya? 5 Je, kikombe hiki sicho anachonywea bwana wangu na pia hukitumia kwa kutabiri mambo yajayo? Hili ni jambo ovu mlilolitenda.’ ”

6 Alipowafikia, akarudia maneno haya kwao. 7 Lakini wakamwambia mtumishi, “Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya? Liwe mbali na watumishi wako wasije wakafanya jambo kama hilo! 8 Hata hivyo tulikurudishia zile fedha kutoka nchi ya Kanaani ambazo tulizikuta kwenye midomo ya magunia yetu. Hivyo kwa nini tuibe fedha au dhahabu kutoka nyumbani kwa bwana wako? 9 Ikiwa yeyote miongoni mwa watumishi wako atapatikana nacho, auawe, na sisi wengine tutakuwa watumwa wa bwana wangu.”

10 Akajibu, “Vema sana; na iwe kama msemavyo. Yeyote atakayekutwa nacho atakuwa mtumwa wangu, lakini ninyi wengine mtakuwa hamna lawama.”

11 Kila mmoja wao akafanya haraka kushusha gunia lake chini na kulifungua. 12 Ndipo msimamizi akaendelea kutafuta, akianzia kwa mkubwa wa wote na akaishia kwa mdogo wa wote. Basi kikombe kikapatikana katika gunia la Benyamini. 13 Kwa jambo hili, wakararua nguo zao. Ndipo wote wakapakiza mizigo yao juu ya punda zao na kurudi mjini.

14 Yosefu alikuwa bado yuko nyumbani mwake wakati Yuda na kaka zake walipoingia, wote wakajitupa chini mbele yake. 15 Yosefu akawaambia, “Ni jambo gani hili mlilolifanya? Hamjui kuwa mtu kama mimi anaweza kufahamu mambo kwa njia ya kutabiri?”

16 Yuda akajibu, “Tutaweza kusema nini kwa bwana wangu? Tutaweza kuzungumza nini? Tutawezaje kuthibitisha kwamba hatuna hatia? Mungu amefunua hatia ya watumishi wako. Sasa sisi tu watumwa wa bwana wangu, sisi wenyewe pamoja na yule aliyepatikana na kikombe.”

17 Lakini Yosefu alisema, “Liwe mbali nami kufanya jambo kama hili! Mtu yule tu aliyekutwa na kikombe ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Ninyi wengine, rudini kwa baba yenu kwa amani.”

18 Ndipo Yuda akamwendea na kumwambia: “Tafadhali bwana wangu, mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa bwana wangu. Usimkasirikie mtumishi wako, ingawa wewe ni sawa na Farao mwenyewe. 19 Bwana wangu aliwauliza watumishi wake, ‘Mnaye baba au ndugu?’ 20 Nasi tukakujibu, ‘Tunaye baba yetu ambaye ni mzee; pia yupo mwanawe mdogo aliyezaliwa katika uzee wake. Ndugu yake amekufa, na huyu mdogo ndiye mwana pekee kwa mama yake aliyebaki, naye baba yake anampenda.’ 

21 “Ndipo ulipowaambia watumishi wako, ‘Mleteni kwangu ili niweze kumwona kwa macho yangu mwenyewe.’ 22 Nasi tukamwambia bwana wangu, ‘Kijana hawezi kumwacha baba yake; akimwacha, baba yake atakufa.’ 23 Lakini ukawaambia watumishi wako, ‘Ndugu yenu mdogo asiposhuka pamoja nanyi, hamtauona uso wangu tena.’ 24 Tuliporudi nyumbani kwa mtumwa wako baba yangu, tulimwambia lile bwana wangu alilokuwa amesema.

25 “Ndipo baba yetu aliposema, ‘Rudini Misri mkanunue chakula kingine.’ 26 Lakini tukamwambia, ‘Hatuwezi kushuka Misri mpaka ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi ndipo tutakapokwenda. Hatutaweza kuuona uso wa yule mtu mpaka ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi.’

27 “Mtumwa wako baba yangu alituambia, ‘Mnajua mke wangu alinizalia wana wawili. 28 Mmojawapo alipotea, nami nikasema, “Hakika ameraruliwa vipande vipande.” Nami sijamwona tangu wakati huo. 29 Ikiwa mtaniondolea huyu tena na akapatwa na madhara, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini nikiwa mwenye huzuni.’

30 “Hivyo sasa, kama kijana hatakuwa pamoja nasi nitakaporudi kwa mtumishi wako baba yangu, na kama baba yangu, ambaye maisha yake yamefungamanishwa na uhai wa kijana huyu, 31 akiona kijana hayupo nasi, atakufa. Watumishi wako watashusha kichwa chenye mvi cha baba yetu kaburini kwa huzuni. 32 Mtumwa wako alimhakikishia baba yangu usalama wa kijana. Nikamwambia, ‘Kama sikumrudisha kwako nitakuwa mwenye lawama mbele yako, baba yangu, maisha yangu yote!’

33 “Sasa basi, tafadhali mruhusu mtumishi abaki hapa kama mtumwa wa bwana wangu badala ya kijana, naye kijana umruhusu arudi na ndugu zake. 34 Ninawezaje kurudi kwa baba yangu kama kijana hatakuwa pamoja nami? La hasha! Usiniache nikaone huzuni ile itakayompata baba yangu.”

45:1 Hapo Yosefu hakuweza kujizuia zaidi mbele ya wote waliokuwa wamesimama karibu naye, akapaza sauti, akasema, “Mwondoeni kila mtu mbele yangu!” Kwa hiyo hapakuwepo mtu yeyote pamoja na Yosefu alipojitambulisha kwa ndugu zake. 2 Naye akalia kwa sauti kubwa kiasi kwamba Wamisri walimsikia, hata watu wa nyumbani mwa Farao wakapata hizo habari.

3 Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu! Je, baba yangu angali hai bado?” Lakini ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwa sababu walipatwa na hofu kuu mbele yake.

4 Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yosefu, yule ambaye mlimuuza Misri! 5 Sasa, msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi. 6 Kwa miaka miwili sasa imekuwepo njaa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwepo kulima wala kuvuna. 7 Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuhifadhi mabaki kwa ajili yenu katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu.

8 “Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kuwa baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote. 9 Sasa rudini haraka kwa baba yangu na mwambieni, ‘Hili ndilo mwanao Yosefu asemalo: Mungu amenifanya mimi kuwa bwana wa Misri yote. Shuka uje kwangu, wala usikawie. 10 Nawe utaishi katika nchi ya Gosheni na kuwa karibu nami, wewe, watoto wako na wajukuu wako, makundi yako ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, pamoja na vyote ulivyo navyo. 11 Nitawatunza huko, kwa sababu bado iko miaka mingine mitano inayokuja ya njaa. La sivyo, wewe na nyumba yako na wote ulio nao mtakuwa fukara.’

12 “Mnaweza kujionea wenyewe, hata ndugu yangu Benyamini, kwamba hakika ni mimi ninayezungumza nanyi. 13 Mwambieni baba yangu juu ya heshima yote niliyopewa huku Misri, na kuhusu kila kitu mlichokiona. Mleteni baba yangu huku haraka.”

14 Ndipo akamkumbatia Benyamini ndugu yake na kulia, naye Benyamini akamkumbatia akilia. 15 Pia akawabusu ndugu zake wote, huku akilia. Baada ya hayo ndugu zake wakazungumza naye.

16 Habari zilipofika kwenye jumba la Farao kwamba ndugu zake Yosefu wamefika, Farao na maafisa wake wote wakafurahi. 17 Farao akamwambia Yosefu, “Waambie ndugu zako, ‘Fanyeni hivi: Pakieni wanyama wenu mrudi mpaka nchi ya Kanaani, 18 mkamlete baba yenu na jamaa zenu kwangu. Nitawapa sehemu nzuri sana ya nchi ya Misri nanyi mtafurahia unono wa nchi.’

19 “Mnaagizwa pia kuwaambia, ‘Fanyeni hivi: Chukueni magari ya kukokotwa kutoka Misri, kwa ajili ya watoto wenu na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje. 20 Msijali kamwe kuhusu mali zenu, kwa sababu mema yote ya Misri yatakuwa yenu.’ ”

21 Hivyo wana wa Israeli wakafanya hivyo. Yosefu akawapa magari ya kukokotwa, kama Farao alivyoagiza, pia akawapa mahitaji kwa ajili ya safari yao. 22 Kila mmoja mavazi mapya, lakini Benyamini akampa shekeli 300 za fedha, na jozi tano za nguo. 23 Hivi ndivyo vitu alivyotuma kwa baba yake: punda kumi waliochukua vitu vizuri vya Misri, punda wake kumi waliobeba nafaka, mikate na mahitaji mengine ya safari. 24 Akaagana na ndugu zake walipokuwa wakiondoka, akawaambia, “Msigombane njiani!”

25 Basi wakatoka Misri na kufika kwa baba yao Yakobo katika nchi ya Kanaani. 26 Wakamwambia baba yao, “Yosefu angali hai! Ukweli ni kwamba yeye ndiye mtawala wa Misri yote.” Yakobo akapigwa na bumbuazi; hakuwasadiki. 27 Lakini walipokwisha kumweleza kila kitu ambacho Yosefu alikuwa amewaambia, na alipoona magari ya kukokotwa Yosefu aliyokuwa amempelekea ya kumchukua aende Misri, roho ya baba yao Yakobo ikahuishwa. 28 Ndipo Israeli akasema, “Nimesadiki! Mwanangu Yosefu bado yu hai. Nitakwenda nikamwone kabla sijafa.”