Sehemu ya 6: Vifo vya Yakobo na Mababu

Yakobo Anawabariki Wanawe na Kufa

1689 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mwanzo 47:27–49:33

27 Basi Waisraeli wakaishi Misri katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali huko wakastawi na kuongezeka kwa wingi sana.

28 Yakobo akaishi Misri miaka kumi na saba, nayo miaka ya maisha yake ilikuwa 147. 29 Wakati ulipokaribia wa Israeli kufa, akamwita mwanawe Yosefu na kumwambia, “Kama nimepata kibali machoni pake, weka mkono wako chini ya paja langu na uniahidi kuwa utanifanyia fadhili na uaminifu. Usinizike Misri, 30 lakini nitakapopumzika na baba zangu, unichukue kutoka Misri, ukanizike walipozikwa.”

Yosefu akamwambia, “Nitafanya kama unavyosema.”

31 Akamwambia, “Niapie.” Ndipo Yosefu akamwapia, naye Israeli akaabudu, akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake.

48:1 Baada ya muda Yosefu akaambiwa kwamba, “Baba yako ni mgonjwa.” Kwa hiyo akawachukua wanawe wawili Manase na Efraimu, pamoja naye. 2 Yakobo alipoambiwa, “Mwanao Yosefu amekujia kukuona,” Israeli akakusanya nguvu zake, akaketi kitandani.

3 Yakobo akamwambia Yosefu, “Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu katika nchi ya Kanaani, huko akanibariki, 4 naye akaniambia, ‘Nitakufanya ustawi na kuongezeka hesabu yako, nitakufanya kuwa jamii ya mataifa, nami nitakupa nchi hii uimiliki milele wewe na wazao wako baada yako.’

5 “Sasa basi, wanao wawili waliozaliwa kwako huku Misri kabla sijaja hapa kwako watahesabiwa kuwa ni wangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama vile Reubeni na Simeoni walivyo wangu. 6 Lakini watoto utakaowazaa baada yao watakuwa wako. Katika nchi watakayoirithi, watatambuliwa kwa jina la ndugu zao. 7 Nilipokuwa ninarudi kutoka Padani, katika huzuni yangu Raheli alifariki katika nchi ya Kanaani tulipokuwa tungali tukisafiri, tukiwa karibu kufika Efrathi. Kwa hiyo nilimzika huko, kando ya njia iendayo Efrathi” (yaani Bethlehemu).

8 Wakati Israeli alipowaona wana wa Yosefu, akauliza, “Hawa ni nani?”

9 Yosefu akamjibu baba yake, “Hawa ni wana ambao Mungu amenipa nikiwa huku.”

Ndipo Israeli akasema, “Walete kwangu ili niwabariki.”

10 Basi macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee, naye aliona kwa shida. Kwa hiyo Yosefu akawaleta wanawe karibu na baba yake, Israeli akawabusu na akawakumbatia.

11 Israeli akamwambia Yosefu, “Kamwe sikutazamia kuuona uso wako tena, lakini sasa Mungu ameniruhusu kuwaona watoto wako pia.”

12 Ndipo Yosefu akawaondoa wanawe magotini mwa Israeli naye akasujudu hadi nchi. 13 Yosefu akachukua wale wana wawili, Efraimu kwenye mkono wake wa kuume akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa Israeli, na Manase katika mkono wake wa kushoto akimwelekeza kwenye mkono wa kuume wa Israeli, akawaleta karibu na babu yao. 14 Lakini Israeli akaupeleka mkono wake wa kuume, akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa alikuwa ndiye mdogo, na mkono wake wa kushoto akaukatisha, akauweka juu ya kichwa cha Manase, ingawa Manase alikuwa ndiye mzaliwa wa kwanza.

15 Ndipo akambariki Yosefu akisema,

“Mungu ambaye baba zangu

Abrahamu na Isaki walimtii,

Mungu ambaye amekuwa mchungaji

wa maisha yangu yote mpaka leo hii,

16 Malaika ambaye aliniokoa kutoka madhara yote,

yeye na awabariki vijana hawa.

Na waitwe kwa jina langu

na kwa majina ya baba zangu Abrahamu na Isaki,

wao na waongezeke kwa wingi

katika dunia.”

17 Yosefu alipoona baba yake akiweka mkono wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, hakupendezwa, kwa hiyo akauchukua mkono wa baba yake kutoka kichwa cha Efraimu na kuuweka juu ya kichwa cha Manase. 18 Yosefu akamwambia, “Hapana, baba yangu, huyu ndiye mzaliwa wa kwanza; uweke mkono wako wa kuume juu ya kichwa chake.”

19 Lakini baba yake akakataa, akasema, “Ninajua, mwanangu, ninajua. Yeye pia atakuwa taifa, naye pia atakuwa mkuu. Hata hivyo, ndugu yake mdogo atakuwa mkuu kuliko yeye, nao wazao wake watakuwa kundi la mataifa.” 20 Akawabarikia siku ile na kusema,

“Kwa jina lenu Israeli watatamka baraka hii:

‘Mungu na awafanye kama Efraimu na Manase.’ ”

Kwa hiyo akamtanguliza Efraimu mbele ya Manase.

21 Ndipo Israeli akamwambia Yosefu, “Mimi ninakaribia kufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, na atawarudisha katika nchi ya baba zenu. 22 Kwako wewe, kama aliye juu ya ndugu zako, ninakupa sehemu moja zaidi ya ndugu zako, lile eneo nililoteka kwa Waamori kwa upanga wangu na upinde wangu.”

49:1 Ndipo Yakobo akawaita wanawe na kusema: “Kusanyikeni kunizunguka ili niweze kuwaambia lile litakalowatokea siku zijazo.

2 “Kusanyikeni na msikilize, enyi wana wa Yakobo,

msikilizeni baba yenu Israeli.

3 “Reubeni, wewe ni mzaliwa wangu wa kwanza,

nguvu zangu, tunda la kwanza la nguvu zangu,

umepita kwa heshima, umepita kwa uwezo.

4 Usiyezuiwa kama maji, basi hutakuwa mkuu tena,

kwa kuwa ulipanda kwenye kitanda cha baba yako,

kwenye kitanda changu na kukinajisi.

5 “Simeoni na Lawi ni wana ndugu:

panga zao ni silaha za jeuri.

6 Mimi na nisiingie katika baraza lao,

nami nisiunganike katika kusanyiko lao,

kwa kuwa wamewaua watu katika hasira yao,

walikata mishipa ya miguu ya mafahali

kama walivyopenda.

7 Hasira yao na ilaaniwe, kwa kuwa ni kali mno,

nayo ghadhabu yao ni ya ukatili!

Nitawatawanya katika Yakobo

Na kuwasambaza katika Israeli.

8 “Yuda, ndugu zako watakusifu;

mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako;

wana wa baba yako watakusujudia.

9 Ee Yuda, wewe ni mwana simba;

unarudi toka mawindoni, mwanangu.

Kama simba hunyemelea na kulala chini,

kama simba jike: nani athubutuye kumwamsha?

10 Fimbo ya ufalme haitaondoka kwa Yuda,

wala fimbo ya mtawala kati ya miguu yake,

hadi aje yeye ambaye milki ni yake,

ambaye utii wa mataifa ni wake.

11 Atamfunga punda wake katika mzabibu,

naye mwana-punda wake kwenye tawi lililo bora zaidi;

atafua mavazi yake katika divai,

majoho yake katika damu ya mizabibu.

12 Macho yake yatakuwa mekundu kwa divai,

meno yake yatakuwa meupe kwa maziwa.

13 “Zabuloni ataishi pwani ya bahari

na kuwa bandari za kuegesha meli;

mpaka wake utapanuka kuelekea Sidoni.

14 “Isakari ni punda mwenye nguvu

ambaye amelala kati ya mizigo yake.

15 Aonapo palivyo pazuri mahali pake pa kupumzika

na jinsi nchi yake inavyopendeza,

atainamisha bega lake kwenye mzigo

na kujitolea kwa ajili ya kazi ngumu.

16 “Dani atahukumu watu wake kwa haki

kama mmoja wa makabila ya Israeli.

17 Dani atakuwa nyoka kando ya barabara,

nyoka mwenye sumu kando ya njia,

yule aumaye visigino vya farasi

ili yule ampandaye aanguke chali.

18 “Ee Bwana, nautafuta wokovu wako.

19 “Gadi atashambuliwa ghafula na kundi la washambuliaji,

lakini yeye atawageukia na kuwashinda kabisa.

20 “Chakula cha Asheri kitakuwa kinono,

naye atatoa chakula kitamu kimfaacho mfalme.

21 “Naftali ni kulungu jike aliyeachiwa huru

azaaye watoto wazuri.

22 “Yosefu ni mzabibu uzaao,

mzabibu uzaao ulio kando ya chemchemi,

ambao matawi yake hutanda ukutani.

23 Kwa uchungu wapiga mshale walimshambulia,

wakampiga mshale kwa ukatili.

24 Lakini upinde wake ulibaki imara,

mikono yake ikatiwa nguvu,

na mkono wa Mwenye Nguvu wa Yakobo,

kwa sababu ya Mchungaji, Mwamba wa Israeli,

25 kwa sababu ya Mungu wa baba yako, anayekusaidia,

kwa sababu ya Mwenyezi, yeye anayekubariki

kwa baraka za mbinguni juu,

baraka za kilindi kilichoko chini,

baraka za matitini na za tumbo la uzazi.

26 Baraka za baba yako ni kubwa

kuliko baraka za milima ya kale,

nyingi kuliko vilima vya kale.

Baraka hizo zote na zikae juu ya kichwa cha Yosefu,

juu ya paji la yule mkuu miongoni mwa ndugu zake.

27 “Benyamini ni mbwa mwitu mlafi mwenye njaa kuu;

asubuhi hurarua mawindo yake,

jioni hugawa nyara.”

28 Haya yote ndiyo makabila kumi na mawili ya Israeli, na hivi ndivyo baba yao alivyowaambia alipowabariki, akimpa kila mmoja baraka inayomfaa.

29 Ndipo alipowapa maelekezo haya: “Mimi niko karibu kukusanywa kwa watu wangu. Mnizike pamoja na baba zangu kwenye pango katika shamba la Efroni, Mhiti, 30 pango lililoko katika shamba la Makpela, karibu na Mamre huko Kanaani, ambalo Abrahamu alinunua kwa ajili ya mahali pa kuzikia kutoka kwa Efroni, Mhiti, pamoja na shamba. 31 Huko ndiko Abrahamu na Sara mkewe walikozikwa, huko akazikwa Isaki na Rebeka mkewe, na huko nilimzika Lea. 32 Shamba hilo na pango lililoko ndani yake lilinunuliwa kutoka kwa Wahiti.”

33 Baada ya Yakobo kumaliza kutoa maelekezo hayo kwa wanawe, akarudisha miguu yake kitandani, akapumua pumzi ya mwisho, na akakusanywa kwa watu wake.