Yesu Anaijaribu Imani ya Wale Kumi na Wawili
Karibu na Kaisaria Filipi, Yesu anaijaribu imani ya wale Kumi na Wawili kwamba yeye ndiye Masiya.
29 au 28 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 16:13–20
16:13 Basi Yesu alipofika katika eneo la Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake, “Watu husema kwamba mimi Mwana wa Adamu ni nani?”
14 Wakamjibu, “Baadhi husema ni Yohana Mbatizaji; wengine husema ni Eliya; na bado wengine husema ni Yeremia au mmojawapo wa manabii.”
15 Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”
16 Simoni Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”
17 Naye Yesu akamwambia, “Heri wewe, Simoni Bar-Yona, kwa maana hili halikufunuliwa kwako na mwanadamu, bali na Baba yangu aliye mbinguni. 18 Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, hata malango ya Kuzimu hayataweza kulishinda. 19 Nitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni, na lolote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, nalo lolote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.”
20 Kisha akawakataza wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Kristo.
Marko 8:27–30
8:27 Yesu na wanafunzi wake wakaondoka kwenda katika vijiji vya Kaisaria-Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”
28 Wakamjibu, “Baadhi husema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine husema ni Eliya, na bado wengine husema wewe ni mmojawapo wa manabii.”
29 Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”
Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo.”
30 Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake.
Luka 9:18–21
9:18 Wakati mmoja, Yesu alipokuwa akiomba faraghani, nao wanafunzi wake wakiwa pamoja naye, akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”
19 Wakamjibu, “Baadhi husema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine husema ni Eliya, na bado wengine husema kwamba ni mmoja wa manabii wa kale amefufuka kutoka kwa wafu.”
20 Kisha akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”
Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo wa Mungu.”
21 Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote jambo hilo.
Yesu Anatabiri Kifo na Ufufuo Wake
Yesu anatabiri kwa uwazi kwamba yeye, Masiya, atakataliwa na kuuawa, na atafufuka siku ya tatu.
Mathayo 16:21–26
16:21 Tangu wakati huo, Yesu alianza kuwaeleza wanafunzi wake kwamba hana budi kwenda Yerusalemu na kupata mateso mengi mikononi mwa wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na kwamba itampasa auawe lakini siku ya tatu kufufuliwa.
22 Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea akisema, “Haiwezekani, Bwana! Jambo hili kamwe halitakupata!”
23 Lakini Yesu akageuka na kumwambia Petro, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
24 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.
25 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata.
26 Kwa maana, je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?
Marko 8:31–37
8:31 Ndipo akaanza kuwafundisha wanafunzi wake kuwa Mwana wa Adamu lazima atapata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na kwamba itampasa auawe lakini baada ya siku tatu afufuke.
32 Aliyasema haya waziwazi, ndipo Petro akamchukua kando na akaanza kumkemea.
33 Lakini Yesu alipogeuka na kuwaangalia wanafunzi wake, akamkemea Petro. Akasema, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
34 Ndipo akauita ule umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akasema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.
35 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili atayaokoa.
36 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? 37 Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?
Luka 9:22–25
9:22 Yesu akasema, “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na itampasa auawe, lakini siku ya tatu kufufuliwa kutoka mauti.”
23 Kisha akawaambia wote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate.
24 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa.
25 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akapoteza au kuangamiza nafsi yake?
Kuja kwa Mwana wa Adamu Katika Kizazi Hicho
Mathayo 16:27–28
16:27 Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. 28 Nawaambia kweli, baadhi yenu hapa hawataonja mauti kabla ya kumwona Mwana wa Adamu akija katika Ufalme wake.”
Marko 8:38–9:1
8:38 Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”
9:1 Yesu akaendelea kuwaambia, “Amin, nawaambia, kuna watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu.”
Luka 9:26–27
9:26 Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu atakapokuja katika utukufu wake na katika utukufu wa Baba, pamoja na malaika watakatifu. 27 Amin, nawaambia, wako baadhi ya watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu.”