Mafarisayo na Masadukayo Wanamshambulia Yesu huko Magadani
Ziara fupi huko Magadani (Dalmanutha) katika Galilaya, na shambulio kali la Mafarisayo na Masadukayo (ona kwamba sasa wanajitokeza kumpinga Yesu).
29 au 28 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 15:39–16:4
15:39 Baada ya kuaga ule umati wa watu, Yesu aliingia katika mashua, akaenda sehemu za Magadani.
16:1 Mafarisayo na Masadukayo wakamjia Yesu na kumjaribu kwa kumwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.
2 Yesu akawajibu, “Ifikapo jioni, mnasema, ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri, kwa kuwa anga ni nyekundu.’ 3 Nanyi wakati wa asubuhi mnasema, ‘Leo kutakuwa na dhoruba, kwa sababu anga ni nyekundu na mawingu yametanda.’ Mnajua jinsi ya kupambanua kule kuonekana kwa anga, lakini hamwezi kupambanua dalili za nyakati. 4 Kizazi kiovu na cha uzinzi kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ya Yona.” Yesu akawaacha, akaenda zake.
Marko 8:10–12
8:10 aliingia kwenye mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda sehemu za Dalmanutha.
11 Mafarisayo wakaja, wakaanza kumhoji Yesu. Ili kumtega, wakamwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni. 12 Akahuzunika moyoni, akawaambia, “Kwa nini kizazi hiki kinataka ishara? Amin nawaambieni, hakitapewa ishara yoyote.”
Yesu Anamponya Mwanaume Kipofu huko Bethsaida
Kujitenga kwa mara ya nne, kwenda Bethsaida Juliasi katika eneo la Herode Filipo, mtawala wa robo. Wakiwa njiani kuvuka ziwa, Yesu anawakemea wanafunzi kwa ukali kwa kukosa kwao ufahamu, na huko Bethsaida anamponya mtu kipofu.
Mathayo 16:5–12
16:5 Wanafunzi wake walipofika ngʼambo ya bahari, walikuwa wamesahau kuchukua mikate.
6 Yesu akawaambia, “Jihadharini. Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ya Masadukayo.”
7 Wakajadiliana wao kwa wao, wakisema, “Ni kwa sababu hatukuleta mikate.”
8 Yesu, akifahamu majadiliano yao, akauliza, “Enyi wa imani haba! Mbona mnajadiliana miongoni mwenu kuhusu kutokuwa na mikate? 9 Je, bado hamwelewi? Je, hamkumbuki ile mikate mitano iliyolisha watu 5,000 na idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya?
10 Au ile mikate saba iliyolisha watu 4,000 na idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya?
11 Inakuwaje mnashindwa kuelewa kwamba nilikuwa sisemi nanyi habari za mikate? Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
12 Ndipo wakaelewa kwamba alikuwa hasemi juu ya chachu ya kutengeneza mikate, bali juu ya mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Marko 8:13–26
8:13 Kisha akawaacha, akarudi kwenye mashua, akavuka hadi ngʼambo.
14 Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate ya kutosha. Walikuwa na mkate mmoja tu kwenye mashua.
15 Yesu akawaonya: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na ya Herode.”
16 Wakajadiliana wao kwa wao, na kusema, “Anasema hivi kwa sababu hatukuleta mikate.”
17 Yesu, akifahamu majadiliano yao, akawauliza: “Mbona mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Je, bado hamtambui wala hamwelewi? Je, mbona mioyo yenu ni migumu kiasi hicho?
18 Je, mna macho lakini mnashindwa kuona, na mna masikio lakini mnashindwa kusikia? Je, hamkumbuki?
19 Nilipoimega ile mikate mitano kuwalisha watu 5,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa vya masazo?”
Wakamjibu, “Kumi na viwili.”
20 “Je, nilipoimega ile mikate saba kuwalisha watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa vya masazo?”
Wakamjibu, “Saba.”
21 Ndipo akawauliza, “Je, bado hamwelewi?”
22 Wakafika Bethsaida na baadhi ya watu wakamleta mtu mmoja kipofu wakamsihi Yesu amguse. 23 Yesu akamshika mkono huyo kipofu akampeleka nje ya kijiji. Baada ya kuyatemea mate macho ya yule kipofu na kumwekea mikono, Yesu akamuuliza, “Unaona chochote?”
24 Yule kipofu akaangalia, akasema, “Ninaona watu, wanaonekana kama miti inayotembea.”
25 Yesu akamwekea tena mikono machoni. Kisha macho yake yakafunguka, kuona kwake kukarejea naye akaona kila kitu dhahiri. 26 Yesu akamuaga aende nyumbani kwake, akimwambia, “Hata kijijini usiingie.”