Yesu Anageuka Sura Mlimani
Yesu anageuka sura juu ya mlima (yaelekea Hermoni) karibu na Kaisaria Filipi.
29 au 28 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 17:1–8
17:1 Siku sita baada ya jambo hili, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, akawapeleka juu ya mlima mrefu peke yao.
2 Wakiwa huko, Yesu alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukangʼaa kama jua na nguo zake zikawa na weupe wa kuumiza macho.
3 Ghafula wakawatokea mbele yao Mose na Eliya, wakizungumza na Yesu.
4 Ndipo Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vyema sisi tukae hapa. Ukitaka, nitafanya vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.”
5 Petro alipokuwa angali ananena, ghafula wingu lililongʼaa likawafunika, na sauti ikatoka kwenye hilo wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana. Msikieni yeye.”
6 Wanafunzi waliposikia haya, wakaanguka chini kifudifudi, wakajawa na hofu.
7 Lakini Yesu akaja na kuwagusa, akawaambia, “Inukeni na wala msiogope.”
8 Walipoinua macho yao, hawakumwona mtu mwingine yeyote isipokuwa Yesu.
Marko 9:2–8
9:2 Baada ya siku sita, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana, akawapeleka juu ya mlima mrefu, mahali walipokuwa faraghani. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao.
3 Mavazi yake yakawa na weupe wa kuzima macho, meupe kuliko ambavyo mtu yeyote duniani angaliweza kuyangʼarisha.
4 Mose na Eliya wakawatokea, wakawa wanazungumza na Yesu.
5 Petro akamwambia Yesu, “Rabi, ni vyema sisi tukae hapa. Turuhusu tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.”
6 Petro hakujua aseme nini kwa maana yeye na wenzake walikuwa wameogopa sana.
7 Ndipo pakatokea wingu, likawafunika, nayo sauti kutoka lile wingu ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Msikieni yeye.”
8 Mara walipotazama huku na huku, hawakuona tena mtu mwingine yeyote pamoja nao isipokuwa Yesu.
Luka 9:28–36
9:28 Yapata siku nane baada ya Yesu kusema hayo, aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana, akaenda nao mlimani kuomba.
29 Alipokuwa akiomba, sura ya uso wake ikabadilika, nayo mavazi yake yakametameta kama mwanga wa umeme wa radi.
30 Ghafula wakawaona watu wawili, ndio Mose na Eliya, wakizungumza naye. 31 Walionekana katika utukufu wakizungumza na Yesu kuhusu kifo chake ambacho kingetokea huko Yerusalemu. 32 Petro na wenzake walikuwa wamelala usingizi mzito. Walipoamka, wakaona utukufu wa Yesu na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye.
33 Mose na Eliya walipokuwa wanaondoka, Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri tukae hapa! Tutajenga vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.” Lakini Petro alikuwa hajui asemacho.
34 Alipokuwa bado anazungumza, pakatokea wingu, likawafunika, nao wakaogopa walipoingia mle kwenye wingu.
35 Sauti ikatoka kwenye lile wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, niliyemchagua. Msikieni yeye.”
36 Baada ya sauti hiyo kusema, walimkuta Yesu akiwa peke yake. Wale wanafunzi wakalihifadhi jambo hili, wala kwa wakati huo hawakumwambia mtu yeyote yale waliyokuwa wameyaona.
Wanafunzi Watatu Wanatatanika Kuhusu Eliya
Wanaposhuka mlimani, wale wanafunzi watatu wanatatanika kuhusu ufufuo na kuhusu Eliya.
Mathayo 17:9–13
17:9 Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaagiza, “Msimwambie mtu yeyote mambo mliyoyaona hapa, mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu.”
10 Wale wanafunzi wakamuuliza, “Kwa nini basi walimu wa sheria husema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza?”
11 Yesu akawajibu, “Ni kweli, Eliya lazima aje kwanza, naye atatengeneza mambo yote.
12 Lakini nawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao hawakumtambua, bali walimtendea kila kitu walichotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu pia atateswa mikononi mwao.”
13 Ndipo wale wanafunzi wakaelewa kuwa alikuwa anazungumza nao habari za Yohana Mbatizaji.
Marko 9:9–13
9:9 Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoona, mpaka Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu.
10 Wakalihifadhi jambo hilo wao wenyewe, lakini wakawa wanajiuliza, “Huku kufufuka kwa wafu maana yake nini?”
11 Wakamuuliza, “Kwa nini walimu wa sheria husema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza?”
12 Yesu akawajibu, “Ni kweli, Eliya yuaja kwanza ili kutengeneza mambo yote. Mbona basi imeandikwa kwamba Mwana wa Adamu ni lazima ateseke sana na kudharauliwa?
13 Lakini ninawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyopenda, kama ilivyoandikwa kumhusu yeye.”