Yesu Anapelekwa Misri na Watoto wa Bethlehemu Wanauawa

Mtoto Yesu anabebwa hadi Misri, na watoto walioko Bethlehemu wanauawa.

Inaelekea 5 KK

5 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 2:13–18

2:13 Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto akamwambia, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.”

14 Kisha Yosefu akaondoka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake wakati wa usiku, nao wakaenda Misri 15 ambako walikaa mpaka Herode alipofariki. Hili lilifanyika ili litimie lile lililonenwa na Bwana kwa kinywa cha nabii kusema: “Nilimwita mwanangu kutoka Misri.”

16 Herode alipongʼamua kwamba wale wataalamu wa nyota wamemshinda kwa akili, alikasirika sana, naye akatoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili kurudi chini katika mji wa Bethlehemu na sehemu zote za jirani, kufuatana na ule muda alioambiwa na wale wataalamu wa nyota. 17 Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia.

18 “Sauti ilisikika huko Rama,

maombolezo na kilio kikubwa,

Raheli akilia kwa ajili ya wanawe,

akikataa kufarijiwa,

kwa sababu hawako tena.”

Yesu Analetwa kutoka Misri hadi Nazareti 4 KK

Inaelekea 4 KK

Mathayo 2:19–23

2:19 Baada ya Herode kufa, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto huko Misri

20 na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wanatafuta uhai wa mtoto wamekufa.”

21 Basi Yosefu, akaondoka akamchukua mtoto na mama yake wakaenda mpaka nchi ya Israeli. 22 Lakini aliposikia kwamba Arkelao alikuwa anatawala huko Uyahudi mahali pa Herode baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye akiisha kuonywa katika ndoto, akaenda zake sehemu za Galilaya, 23 akaenda akaishi katika mji ulioitwa Nazareti. Hivyo likawa limetimia neno lililonenwa na manabii, “Ataitwa Mnazarayo.”

Luka 2:39

2:39 Yosefu na Maria walipokuwa wamekamilisha mambo yote yaliyotakiwa na Sheria ya Bwana, walirudi mjini kwao Nazareti huko Galilaya.

Utoto wa Yesu huko Nazareti 4 KK hadi 7 BK

Inaelekea 4 KK hadi 7 BK

Luka 2:40

2:40 Naye yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu, akiwa amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

Mvulana Yesu Anatembelea Yerusalemu Akiwa na Miaka Kumi na Miwili 7 au 8 BK

Inaelekea 7 au 8 BK

Luka 2:41–50

2:41 Kila mwaka Yosefu na Maria mama yake Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka. 42 Yesu alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, walipanda kwenda kwenye Sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. 43 Baada ya Sikukuu kumalizika, wakati Yosefu na Maria mama yake walipokuwa wakirudi nyumbani, Yesu alibaki Yerusalemu lakini hawakutambua. 44 Wao wakidhani kuwa yuko miongoni mwa wasafiri, walienda mwendo wa kutwa nzima. Ndipo wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa zao na marafiki. 45 Walipomkosa walirudi Yerusalemu ili kumtafuta. 46 Baada ya siku tatu wakamkuta ndani ya Hekalu, akiwa ameketi katikati ya walimu wa sheria, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47 Wote waliomsikia walistaajabishwa na uwezo wake mkubwa wa kuelewa, na majibu aliyoyatoa. 48 Yosefu na Maria mama yake walipomwona walishangaa. Mama yake akamuuliza, “Mwanangu, mbona umetufanyia hivi? Tazama, mimi na baba yako tumekuwa tukikutafuta kwa wasiwasi mkubwa kila mahali.”

49 Yesu akawaambia, “Kwa nini kunitafuta? Hamkujua kwamba imenipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?”

50 Lakini wao hawakuelewa maana ya lile alilowaambia.

Miaka Kumi na Minane huko Nazareti 6 hadi 26 BK

Inaelekea 7 BK hadi 26 BK (au 6 hadi 25)

Luka 2:51–52

2:51 Ndipo akashuka pamoja nao hadi Nazareti, naye alikuwa mtiifu kwao. Lakini mama yake akayaweka moyoni mwake mambo haya yote. 52 Naye Yesu akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.