Yesu Anatolewa Hekaluni
Yesu anatolewa hekaluni, ambako Simeoni na Ana wanampa heshima.
Yerusalemu
6 au 5 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Luka 2:22–38
2:22 Ulipotimia wakati wa utakaso wake Maria kwa mujibu wa Sheria ya Mose, basi Yosefu na Maria walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Bwana 23 (kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana, kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Bwana”), 24 na pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa katika Sheria ya Bwana: “Hua wawili au makinda mawili ya njiwa.”
25 Basi alikuwako huko Yerusalemu mtu mmoja jina lake Simeoni, ambaye alikuwa mwenye haki na mcha Mungu, akitarajia faraja ya Israeli, na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. 26 Roho Mtakatifu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Kristo wa Bwana. 27 Simeoni, akiwa ameongozwa na Roho Mtakatifu, alikwenda Hekaluni. Wazazi walipomleta mtoto Yesu ili kumfanyia kama ilivyokuwa desturi ya Sheria, 28 ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema:
29 “Bwana Mwenyezi, kama ulivyoahidi,
sasa wamruhusu mtumishi wako
aende zake kwa amani.
30 Kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako,
31 ulioweka tayari machoni pa watu wote,
32 nuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu wa Mataifa
na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli.”
33 Naye Yosefu na mama yake mtoto wakastaajabu kwa yale yaliyokuwa yamesemwa kumhusu huyo mtoto. 34 Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, “Mtoto huyu amewekwa kwa makusudi ya kuanguka na kuinuka kwa wengi katika Israeli. Atakuwa ishara ambayo watu watanena dhidi yake, 35 ili mawazo ya mioyo mingi yadhihirike. Nao upanga utauchoma moyo wako.”
36 Tena alikuwako Hekaluni nabii mmoja mwanamke, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana; naye alikuwa ameolewa na kuishi na mume kwa miaka saba tu, kisha mumewe akafa. 37 Hivyo alikuwa mjane na umri wake ulikuwa miaka themanini na minne. Yeye hakuondoka humo Hekaluni usiku wala mchana, bali alikuwa akimwabudu Mungu, akifunga na kuomba. 38 Wakati huo huo, Ana alikuja akaanza kusifu, akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu.
Wataalamu wa Mambo ya Nyota Wanamtembelea Mfalme wa Wayahudi Aliyezaliwa Karibuni
Yerusalemu na Bethlehemu
Mathayo 2:1–12
2:1 Baada ya Yesu kuzaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Uyahudi, wakati wa utawala wa Mfalme Herode, wataalamu wa mambo ya nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu 2 wakiuliza, “Yuko wapi huyo aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake ikitokea mashariki, nasi tumekuja kumwabudu.”
3 Mfalme Herode aliposikia jambo hili aliingiwa na hofu sana pamoja na watu wote wa Yerusalemu. 4 Herode akawaita pamoja viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, akawauliza ni mahali gani ambapo Kristo angezaliwa. 5 Nao wakamwambia, “Katika Bethlehemu ya Uyahudi, kwa maana hivyo ndivyo ilivyoandikwa na nabii:
6 “ ‘Nawe, Bethlehemu, katika nchi ya Yuda,
wewe si mdogo miongoni
mwa watawala wa Yuda;
kwa maana kutoka kwako atakuja mtawala
atakayekuwa mchungaji
wa watu wangu Israeli.’ ”
7 Ndipo Herode akawaita wale wataalamu wa nyota kwa siri na kutaka kujua kutoka kwao uhakika kamili wa wakati ile nyota ilionekana. 8 Kisha akawatuma waende Bethlehemu akiwaambia, “Nendeni mkamtafute kwa bidii huyo mtoto. Nanyi mara mtakapomwona, mniletee habari ili na mimi niweze kwenda kumwabudu.”
9 Baada ya kumsikia mfalme, wale wataalamu wa nyota wakaenda zao, nayo ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, nao wakaifuata mpaka iliposimama mahali pale alipokuwa mtoto. 10 Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno. 11 Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Maria mama yake, wakamsujudu na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane. 12 Nao wakiisha kuonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi kwenda katika nchi yao kwa njia nyingine.