Sehemu ya 5: Yohana Mbatizaji Anaanza Huduma Yake

Inaelekea miezi sita, mwaka wa 25 BK. Katika jangwa la Uyahudi na kando ya Yordani

Wakati wa Mwanzo

25 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Marko 1:1

1:1 Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

Luka 3:1–2

3:1 Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato akiwa mtawala wa Uyahudi, Herode akiwa mfalme wa Galilaya, Filipo ndugu yake akiwa mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania akiwa mfalme wa Abilene, 2 nao Anasi na Kayafa wakiwa makuhani wakuu, neno la Mungu likamjia Yohana, mwana wa Zekaria huko jangwani.

Ujumbe na Mjumbe

Mathayo 3:1–6

3:1 Siku hizo Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri katika nyika ya Uyahudi, akisema,

2 “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.”

3 Huyu ndiye yule aliyenenwa habari zake na nabii Isaya aliposema:

“Sauti ya mtu aliaye huko nyikani,

‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana,

yanyoosheni mapito yake.’ ”

4 Basi Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia, akiwa na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. 5 Watu walikuwa wakimwendea kutoka Yerusalemu, Uyahudi yote na nchi zote za kandokando ya Mto Yordani.

6 Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.

Marko 1:2–6

1:2 Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:

“Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,

atakayetengeneza njia mbele yako”:

3 “sauti ya mtu aliaye nyikani.

‘Itengenezeni njia ya Bwana,

yanyoosheni mapito yake.’ ”

4 Yohana alikuja, akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. 5 Watu kutoka Uyahudi wote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.

6 Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu.

Luka 3:3–6

3:3 Akaenda katika nchi yote kandokando ya Mto Yordani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi.

4 Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:

“Sauti ya mtu aliaye nyikani,

‘Itengenezeni njia ya Bwana,

yanyoosheni mapito yake.

5 Kila bonde litajazwa,

kila mlima na kilima vitashushwa.

Njia zilizopinda zitanyooshwa,

na zilizoparuza zitasawazishwa.

6 Nao watu wote watauona

wokovu wa Mungu.’ ”

Mfano wa Mahubiri ya Yohana Mbatizaji

Mathayo 3:7–10

3:7 Lakini alipowaona Mafarisayo na Masadukayo wengi wakija ili kubatizwa, aliwaambia: “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja?

8 Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. 9 Wala msidhani mnaweza kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka kwa mawe haya.

10 Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni.

Luka 3:7–14

3:7 Yohana akauambia ule umati wa watu uliokuwa unakuja ili kubatizwa naye, “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja?

8 Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. Wala msianze kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Kwa maana nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka mawe haya.

9 Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti. Basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”

10 Ule umati wa watu ukamuuliza, “Inatupasa tufanyeje basi?”

11 Yohana akawaambia, “Aliye na kanzu mbili amgawie asiye nayo, naye aliye na chakula na afanye vivyo hivyo.”

12 Watoza ushuru nao wakaja ili wabatizwe, wakamuuliza, “Bwana na sisi inatupasa tufanyeje?”

13 Akawaambia, “Msichukue zaidi ya kiwango mlichopangiwa.”

14 Askari nao wakamuuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?”

Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.”

Yohana Anamwelezea Masiya Kabla ya Kumwona

Mtangulizi, Yohana Mbatizaji, anamwelezea Masiya kabla hajamwona.

Mathayo 3:11–12

3:11 “Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini nyuma yangu anakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuvichukua viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.

12 Pepeto lake liko mkononi mwake, naye atasafisha sakafu yake ya kupuria, na kuikusanya ngano ghalani na kuyateketeza makapi kwa moto usiozimika.”

Marko 1:7–8

1:7 Naye alihubiri akisema, “Baada yangu atakuja yeye aliye na uwezo kuniliko mimi, ambaye sistahili hata kuinama na kulegeza kamba za viatu vyake.

8 Mimi nawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”

Luka 3:15–18

3:15 Watu walikuwa na matazamio makubwa. Wakawa wanajiuliza mioyoni mwao iwapo Yohana angeweza kuwa ndiye Kristo.

16 Yohana akawajibu akawaambia, “Mimi nawabatiza kwa maji. Lakini atakuja aliye na nguvu kuniliko mimi, ambaye sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 17 Pepeto lake liko mkononi, tayari kusafisha sakafu yake ya kupuria na kuikusanya ngano ghalani, lakini makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.” 18 Basi, kwa maonyo mengine mengi Yohana aliwasihi na kuwahubiria watu Habari Njema.