Yesu Anamponya Mama Mkwe wa Petro na Wengine Wengi
Huko Kapernaumu, nyumbani kwa Petro
27 hadi 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 8:14–17
8:14 Yesu alipoingia nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, akiwa ana homa.
15 Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, naye akainuka na kuanza kumhudumia.
16 Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuwaponya wagonjwa wote.
17 Haya yalifanyika ili litimie lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba:
“Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu
na alichukua magonjwa yetu.”
Marko 1:29–34
1:29 Mara walipotoka katika sinagogi, walikwenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea.
30 Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake.
31 Hivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.
32 Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu.
33 Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo.
34 Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme, kwa sababu walimjua yeye ni nani.
Luka 4:38–41
4:38 Yesu akatoka katika sinagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Basi huko alimkuta mama mkwe wa Simoni akiwa ameshikwa na homa kali, nao wakamwomba Yesu amsaidie.
39 Hivyo Yesu akamwinamia na kukemea ile homa, nayo ikamwacha. Akaamka saa ile ile, naye akaanza kuwahudumia.
40 Jua lilipokuwa linatua, watu wakamletea Yesu watu wote waliokuwa na maradhi mbalimbali, naye akaweka mikono yake juu ya kila mgonjwa, naye akawaponya.
41 Pepo wachafu pia wakawatoka watu wengi, nao walipokuwa wakitoka wakapiga kelele, wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea na kuwazuia wasiseme, kwa maana walimjua kuwa yeye ndiye Kristo.
Yesu Anazunguka Galilaya kwa Mara ya Kwanza Pamoja na Wale Wavuvi Wanne
Hapa Yesu anafanya safari yake ya kwanza ya kuzunguka Galilaya pamoja na wale wavuvi wanne, ambao sasa amewaita wamfuate daima. Wanaporudi Kapernaumu, Mathayo anaitwa, na miujiza mbalimbali inaamsha shauku ya makutano na uadui wa Mafarisayo dhidi ya mafundisho ya Kristo.
Mathayo 4:23–25
4:23 Yesu akapita katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu. 24 Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Shamu, nao watu wakamletea wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na maumivu, waliopagawa na pepo wachafu, wenye kifafa na waliopooza, naye akawaponya. 25 Makutano makubwa ya watu yakawa yanamjia kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Uyahudi na kutoka ngʼambo ya Mto Yordani.
Marko 1:35–39
1:35 Alfajiri na mapema sana kulipokuwa bado kuna giza, Yesu akaamka, akaondoka, akaenda mahali pa faragha ili kuomba. 36 Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta,
37 nao walipomwona, wakamwambia, “Kila mtu anakutafuta!”
38 Yesu akawajibu, “Twendeni mahali pengine kwenye vijiji jirani, ili niweze kuhubiri huko pia, kwa sababu hicho ndicho nilichokuja kukifanya.”
39 Kwa hiyo akazunguka Galilaya kote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu.
Luka 4:42–44
4:42 Kesho yake, kulipopambazuka, Yesu alikwenda mahali pa faragha. Watu wengi wakawa wanamtafuta kila mahali, nao walipomwona wakajaribu kumzuia asiondoke.
43 Lakini yeye akawaambia, “Imenipasa kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa maana kwa kusudi hili nilitumwa.”
44 Naye aliendelea kuhubiri katika masinagogi ya Uyahudi.
Yesu Anamponya Mwenye Ukoma
Mwenye ukoma anaponywa, na kuna msisimko mkubwa miongoni mwa watu.
Mathayo 8:2–4
8:2 Mtu mmoja mwenye ukoma akaja na kupiga magoti mbele yake, akasema, “Bwana, kama ukitaka, unaweza kunitakasa.”
3 Yesu akanyoosha mkono wake akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Mara yule mtu akatakasika ukoma wake.
4 Kisha Yesu akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote. Lakini nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na utoe sadaka aliyoamuru Mose, ili kuwa ushuhuda kwao.”
Marko 1:40–45
1:40 Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akamwomba akipiga magoti, akamwambia, “Ukitaka, waweza kunitakasa.”
41 Yesu, akiwa amejawa na huruma, akanyoosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka. Takasika!” 42 Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika.
43 Baada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake 44 akimwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote habari hizi, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka alizoagiza Mose kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.”
45 Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo, Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi lakini alikaa sehemu zisizo na watu. Hata hivyo watu wakamfuata huko kutoka kila upande.
Luka 5:12–16
5:12 Ikawa siku moja Yesu alipokuwa katika mji fulani, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamjia. Alipomwona Yesu, alianguka chini mpaka uso wake ukagusa ardhi, akamsihi akisema, “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.”
13 Yesu akanyoosha mkono wake, akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Na mara ukoma wake ukatakasika.
14 Yesu akamwagiza akisema, “Usimwambie mtu yeyote, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani na ukatoe sadaka alizoagiza Mose kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.”
15 Lakini habari zake Yesu zikazidi sana kuenea kotekote kuliko wakati mwingine wowote. Makutano makubwa ya watu yalikuwa yakikusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. 16 Lakini mara kwa mara Yesu alijitenga nao ili kwenda mahali pa faragha kuomba.