Katika Wavuvi Wanne Yesu Anapata Wavuvi wa Watu

Kando ya Bahari ya Galilaya, karibu na Kapernaumu

27 hadi 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 4:18–22

4:18 Yesu alipokuwa anatembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake. Walikuwa wakizitupa nyavu zao baharini kwa kuwa wao walikuwa wavuvi.

19 Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.”

20 Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

21 Alipoendelea mbele kutoka pale, akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa wamekaa kwenye mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakizitengeneza nyavu zao. Yesu akawaita.

22 Nao mara wakaiacha mashua yao, pamoja na baba yao, wakamfuata.

Marko 1:16–20

1:16 Yesu alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa wao walikuwa wavuvi.

17 Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.”

18 Mara wakaacha nyavu zao, wakamfuata.

19 Alipokwenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao.

20 Papo hapo akawaita, nao wakamwacha Zebedayo baba yao kwenye mashua pamoja na watumishi wa kuajiriwa, nao wakamfuata Yesu.

Luka 5:1–11

5:1 Siku moja Yesu alipokuwa amesimama karibu na Ziwa la Genesareti, watu wengi wakiwa wanasongana kumzunguka ili wapate kusikia neno la Mungu,

2 akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa, zikiwa zimeachwa hapo na wavuvi waliokuwa wanaosha nyavu zao.

3 Akaingia katika mojawapo ya hizo mashua ambayo ilikuwa ya Simoni, akamwomba aisogeze ndani ya maji kidogo kutoka ufuoni. Kisha akaketi na kufundisha watu akiwa mle ndani ya mashua.

4 Alipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “Sasa peleka mashua hadi kilindini kisha mshushe nyavu zenu mkavue samaki.”

5 Simoni akamjibu, “Bwana, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha na hatukuvua chochote. Lakini, kwa neno lako nitazishusha nyavu.”

6 Nao walipozishusha nyavu zao, wakavua samaki wengi sana, nyavu zao zikajaa zikaanza kukatika. 7 Wakawaashiria wavuvi wenzao kwenye ile mashua nyingine ili waje kuwasaidia. Wakaja, wakajaza mashua zote mbili samaki hata zikaanza kuzama.

8 Simoni Petro alipoona haya yaliyotukia, alianguka miguuni mwa Yesu na kumwambia, “Bwana, ondoka kwangu. Mimi ni mtu mwenye dhambi!” 9 Kwa kuwa yeye na wavuvi wenzake walikuwa wameshangazwa sana na wingi wa samaki waliokuwa wamepata. 10 Vivyo hivyo wenzake Simoni, yaani Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walishangazwa pia.

Ndipo Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.” 11 Hivyo wakasogeza mashua zao mpaka ufuoni mwa bahari, wakaacha kila kitu na kumfuata.

Yesu Anamponya Mtu Mwenye Pepo Katika Sinagogi

Msisimko unajaa katika sinagogi kwa sababu ya mafundisho ya Yesu na kumponya kwake mtu mwenye pepo siku ya Sabato.

Marko 1:21–28

1:21 Wakaenda mpaka Kapernaumu. Ilipofika siku ya Sabato, mara Yesu akaingia sinagogi, akaanza kufundisha.

22 Watu wakashangaa sana kwa mafundisho yake, kwa maana aliwafundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wa sheria. 23 Wakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu,

24 naye akapiga kelele akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”

25 Lakini Yesu akamkemea, akamwambia, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” 26 Yule pepo mchafu akamtikisatikisa huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa.

27 Watu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!”

28 Sifa zake zikaanza kuenea haraka katika eneo lote la karibu na Galilaya.

Luka 4:32–37

4:32 Wakashangazwa sana na mafundisho yake, maana maneno yake yalikuwa na mamlaka.

33 Ndani ya sinagogi palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu. Naye akapiga kelele kwa nguvu akisema,

34 “Tuache! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”

35 Basi Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akisema, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” Yule pepo mchafu akamwangusha yule mtu chini mbele yao wote, akatoka pasipo kumdhuru.

36 Watu wote wakashangaa, wakaambiana, “Mafundisho haya ni ya namna gani? Anawaamuru pepo wachafu kwa mamlaka na nguvu, nao wanatoka!”

37 Habari zake zikaanza kuenea kila mahali katika sehemu ile.