Sehemu ya 7: Utumishi Mkuu wa Galilaya

Yaelekea kutoka majira ya kupukutika kwa majani ya mwaka wa 27 BK hadi majira ya kuchipua ya mwaka wa 29 (inaonekana karibu mwaka mmoja na nusu)

Marko anaeleza kipindi hiki kwa undani sana, na Luka anakieleza kwa muhtasari, ilhali Mathayo katika sehemu hii anapanga maelezo yake hasa kulingana na mada. Injili ya Marko inaingia moja kwa moja katika Huduma Kuu ya Galilaya (linganisha muhtasari wa Petro kuhusu maisha ya Kristo alioutoa kwa watu wa nyumbani mwa Kornelio katika Matendo ya Mitume 10:36–43). Wingi wa maelezo unafanya iwe vigumu kuyapanga katika makundi yaliyo wazi, lakini matukio yanaendelea kusonga mbele.

  • Baada ya Kukataliwa Nazareti, Yesu Anahamia Kapernaumu
  • Safari ya kwanza ya kuzunguka Galilaya pamoja na wale wavuvi wanne, na, wakati wa kurudi, kuitwa kwa Mathayo (Lawi), huku umaarufu wa Yesu ukiongezeka.
  • Mabishano Kuhusu Sabato Huko Yerusalemu na Galilaya
  • Yesu Anawachagua Wale Kumi na Wawili na Kuhubiri Mlimani
  • Ushawishi wa Kristo Unaongezeka na Yohana Anauliza Kutoka Gerezani
  • Ziara ya pili ya Galilaya (sasa pamoja na wale Kumi na Wawili), na uadui mkali wa Mafarisayo.
  • Kundi kubwa la kwanza la mifano, pamoja na ziara huko Gerasa (Kursi) na ziara ya mwisho huko Nazareti.
  • Ziara ya tatu ya Galilaya (Yesu akiwafuata wale Kumi na Wawili), na athari yake kwa Herode Antipa.

Yesu Anafundisha Galilaya

Maelezo ya jumla kuhusu mafundisho ya Yesu huko Galilaya.

27 hadi 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 4:17

4:17 Tangu wakati huo, Yesu alianza kuhubiri akisema: “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.”

Marko 1:15

1:15 akisema, “Wakati umewadia, Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema.”

Luka 4:15

4:15 Akaanza kufundisha kwenye masinagogi yao, na kila mmoja akamsifu.

Huko Kana Yesu Anamponya Mwana wa Afisa

Huko Kana, Yesu anamponya mwana wa afisa wa mfalme kutoka Kapernaumu.

Hapa, katika sehemu inayohusu kukataliwa Nazareti na makazi mapya huko Kapernaumu, Yesu anatembelea tena Kana na Nazareti, anawaita tena wale wavuvi wanne kando ya Bahari ya Galilaya, na kuanza huduma yake ya kufundisha na kuponya huko Kapernaumu.

Yohana 4:46–54

4:46 Hivyo Yesu akaja tena mpaka Kana ya Galilaya, kule alikokuwa amebadili maji kuwa divai. Huko kulikuwepo na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. 47 Huyo mtu aliposikia kwamba Yesu alikuwa amewasili Galilaya kutoka Uyahudi, alimwendea na kumwomba ili aje kumponya mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa.

48 Yesu akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.”

49 Yule afisa wa mfalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.”

50 Yesu akamjibu, “Enenda zako, mwanao yu hai.”

Yule afisa akaamini yale maneno Yesu aliyomwambia, akaondoka akaenda zake. 51 Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima. 52 Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana yapata saa saba, homa ilimwacha.”

53 Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati ambapo Yesu alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye pamoja na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Yesu.

54 Hii ilikuwa ishara ya pili ambayo Yesu alifanya aliporudi Galilaya kutoka Uyahudi.

Nazareti Inamkataa Yesu kwa Mara ya Kwanza

Luka 4:16–31

4:16 Yesu akaenda Nazareti, alipolelewa, na siku ya Sabato alikwenda katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome, 17 naye akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na kukuta mahali palipoandikwa:

18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,

kwa sababu amenitia mafuta

kuwahubiria maskini habari njema.

Amenituma kuwatangazia wafungwa

kufunguliwa kwao,

na vipofu kupata kuona tena,

kuwaweka huru wanaoonewa,

19 na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika.”

20 Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. 21 Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo Andiko hili limetimia mkiwa mnasikia.”

22 Wote waliokuwako wakamsifu na kuyastaajabia maneno yake yaliyojaa neema, wakaulizana, “Je, huyu si mwana wa Yosefu?”

23 Yesu akawaambia, “Bila shaka mtatumia mithali hii: ‘Tabibu, jiponye mwenyewe! Mambo yale tuliyosikia kwamba uliyafanya huko Kapernaumu, yafanye na hapa kwenye mji wako.’ ”

24 Yesu akasema, “Amin, nawaambia, hakuna nabii anayekubalika katika mji wake mwenyewe. 25 Lakini ukweli ni kwamba palikuwa na wajane wengi katika Israeli wakati wa Eliya, mbingu zilipofungwa kwa miaka mitatu na miezi sita pakawa na njaa kuu katika nchi nzima. 26 Hata hivyo Eliya hakutumwa hata kwa mmoja wao, bali kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. 27 Pia palikuwa na wengi wenye ukoma katika Israeli katika siku za nabii Elisha, lakini hakuna hata mmoja wao aliyetakaswa, isipokuwa Naamani mtu wa Shamu.”

28 Watu wote katika sinagogi waliposikia maneno haya, wakakasirika sana. 29 Wakasimama, wakamtoa nje ya mji, wakamchukua hadi kwenye kilele cha mlima mahali ambapo mji huo ulikuwa umejengwa, ili wamtupe chini kutoka kwenye mteremko mkali. 30 Lakini yeye akapita papo hapo katikati ya huo umati wa watu akaenda zake.

31 Kisha Yesu akashuka kwenda Kapernaumu, mji wa Galilaya, na katika siku ya Sabato akawa anafundisha.

Yesu Anaweka Makazi Yake Kapernaumu

Mathayo 4:13–16

4:13 Akaondoka Nazareti akaenda kuishi Kapernaumu, mji ulioko karibu na bahari, katika mipaka ya nchi ya Zabuloni na Naftali, 14 ili kutimiza unabii wa nabii Isaya, kama alivyosema:

15 “Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali,

kwenye njia ya kuelekea baharini,

ngʼambo ya Yordani,

Galilaya ya watu wa Mataifa:

16 watu wale waliokaa gizani

wameona nuru kuu;

nao wale walioishi katika nchi ya uvuli wa mauti,

nuru imewazukia.”