Yesu Anamponya Mtu Aliyepooza Aliyeshushwa Kupitia Paa
Huku makutano yakimsonga huko Kapernaumu, Yesu anamponya mtu aliyepooza aliyeshushwa kupitia paa la nyumba ya Petro.
27 hadi 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 9:1–8
9:1 Yesu akaingia kwenye chombo, akavuka na kufika katika mji wa kwao.
2 Wakati huo huo wakamletea mtu aliyepooza, akiwa amelazwa kwenye mkeka. Yesu alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, jipe moyo mkuu. Dhambi zako zimesamehewa.”
3 Kwa ajili ya jambo hili, baadhi ya walimu wa sheria wakasema mioyoni mwao, “Huyu mtu anakufuru!”
4 Lakini Yesu akiyafahamu mawazo yao, akawaambia, “Kwa nini mnawaza maovu mioyoni mwenu?
5 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? 6 Lakini, ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Ndipo akamwambia yule aliyepooza, “Inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.”
7 Yule mtu akasimama, akaenda nyumbani kwake.
8 Makutano walipoyaona haya, wakajawa na hofu ya Mungu, wakamtukuza Mungu ambaye alikuwa ametoa mamlaka kama haya kwa wanadamu.
Marko 2:1–12
2:1 Baada ya siku kadhaa Yesu alirudi Kapernaumu, watu wakasikia kwamba amerudi nyumbani. 2 Hivyo watu wengi wakakusanyika kiasi kwamba hapakubaki nafasi yoyote hata mlangoni! Naye akawahubiria Neno.
3 Ndipo baadhi ya watu wakaja wakamletea Yesu mtu aliyepooza, akiwa amebebwa na watu wanne. 4 Kwa kuwa walikuwa hawawezi kumfikisha kwa Yesu kwa ajili ya umati wa watu, walitoboa tundu kwenye paa mahali pale alipokuwa Yesu, wakamshusha yule aliyepooza kwa kitanda alichokuwa amelalia.
5 Yesu alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, dhambi zako zimesamehewa.”
6 Basi baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wameketi huko wakawaza mioyoni mwao, 7 “Kwa nini mtu huyu anasema hivi? Huyu anakufuru! Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”
8 Mara moja Yesu akatambua rohoni mwake kile walichokuwa wanawaza mioyoni mwao, naye akawaambia, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu?
9 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uchukue mkeka wako, uende’?
10 Lakini ili mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Yesu akamwambia yule aliyepooza, 11 “Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.”
12 Yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama, akachukua mkeka wake, akatembea machoni pao wote! Jambo hili likawashangaza wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, “Hatujapata kuona jambo kama hili kamwe!”
Luka 5:17–26
5:17 Siku moja Yesu alipokuwa akifundisha, Mafarisayo na walimu wa sheria, waliokuwa wametoka kila kijiji cha Galilaya na kutoka Uyahudi na Yerusalemu, walikuwa wameketi huko. Nao uweza wa Bwana ulikuwa juu yake kuponya wagonjwa.
18 Wakaja watu wamembeba mgonjwa aliyepooza kwenye mkeka. Wakajaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Yesu. 19 Walipokuwa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu ya umati wa watu, wakapanda juu ya paa, wakaondoa baadhi ya matofali, wakamteremsha yule mgonjwa kwa mkeka wake hadi katikati ya ule umati pale mbele ya Yesu.
20 Yesu alipoiona imani yao, akamwambia yule mgonjwa, “Rafiki, dhambi zako zimesamehewa.”
21 Mafarisayo na wale walimu wa sheria wakaanza kuuliza, “Ni nani mtu huyu anayesema maneno ya kukufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”
22 Yesu akijua mawazo yao akawauliza, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu?
23 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi, kumwambia, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’?
24 Lakini ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Akamwambia yule aliyepooza, “Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.”
25 Mara yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama mbele yao wote, akachukua mkeka wake, akaenda zake nyumbani, huku akimtukuza Mungu.
26 Kila mmoja akashangaa na kumtukuza Mungu. Wakajawa na hofu ya Mungu, wakasema, “Leo tumeona mambo ya ajabu.”