Yesu Anamwita Mathayo, Ambaye Anamwandalia Karamu ya Mapokezi

Yesu anamwita Mathayo (Lawi), ambaye anaandaa karamu ya mapokezi kwa heshima ya Yesu.

Kapernaumu

27 hadi 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 9:9–13

9:9 Yesu alipokuwa akienda kutoka huko, alimwona mtu mmoja jina lake Mathayo akiwa ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate.” Mathayo akaondoka, akamfuata.

10 Yesu alipokuwa akila chakula ndani ya nyumba ya Mathayo, watoza ushuru wengi na “wenye dhambi” wakaja kula pamoja naye na wanafunzi wake.

11 Mafarisayo walipoona mambo haya, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”

12 Lakini Yesu aliposikia hayo, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, lakini wale walio wagonjwa ndio wanaohitaji tabibu. 13 Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya: ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

Marko 2:13–17

2:13 Yesu akaenda tena kandokando ya Bahari ya Galilaya. Umati mkubwa wa watu ukamfuata, naye akaanza kuwafundisha.

14 Alipokuwa akitembea, akamwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru, akamwambia, “Nifuate.” Lawi akaondoka, akamfuata Yesu.

15 Yesu alipokuwa akila chakula nyumbani mwa Lawi, watoza ushuru wengi pamoja na “wenye dhambi” walikuwa wakila pamoja naye na wanafunzi wake, kwa maana kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakimfuata.

16 Baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa Mafarisayo walipomwona akila pamoja na watoza ushuru na “wenye dhambi,” wakawauliza wanafunzi wake: “Mbona Yesu anakula pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”

17 Yesu aliposikia haya akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

Luka 5:27–32

5:27 Baada ya haya, Yesu alitoka na kumwona mtoza ushuru mmoja jina lake Lawi akiwa amekaa forodhani, mahali pake pa kutoza ushuru. Akamwambia, “Nifuate.”

28 Naye Lawi akaacha kila kitu, akaondoka, akamfuata.

29 Kisha Lawi akamfanyia Yesu karamu kubwa nyumbani kwake, nao umati mkubwa wa watoza ushuru na watu wengine walikuwa wakila pamoja nao.

30 Lakini Mafarisayo na walimu wa sheria waliokuwa wa dhehebu lao wakawalalamikia wanafunzi wa Yesu, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”

31 Yesu akawajibu, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. 32 Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi wapate kutubu.”

Yesu Anawatetea Wanafunzi Wake kwa Kutofunga

Katika mifano mitatu, Yesu anawatetea wanafunzi wake kwa kufanya karamu badala ya kufunga.

Mathayo 9:14–17

9:14 Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji wakaja na kumuuliza Yesu, “Imekuwaje kwamba sisi na Mafarisayo tunafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”

15 Yesu akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kuomboleza wakati angali pamoja nao? Wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.

16 “Hakuna mtu anayeshonea kiraka kipya kwenye nguo iliyochakaa, kwa maana kile kiraka kitachanika kutoka kwenye hiyo nguo, nayo hiyo nguo itachanika zaidi.

17 Wala watu hawaweki divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Kama wakifanya hivyo, viriba vitapasuka nayo divai itamwagika, navyo viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya, na hivyo divai na viriba huwa salama.”

Marko 2:18–22

2:18 Basi wanafunzi wa Yohana pamoja na Mafarisayo walikuwa wakifunga. Baadhi ya watu wakamjia Yesu na kumuuliza, “Mbona wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo hufunga lakini wanafunzi wako hawafungi?”

19 Yesu akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kufunga wakati angali pamoja nao? Wakati bwana arusi bado yuko pamoja nao, hawawezi kufunga.

20 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Siku hiyo ndipo watakapofunga.

21 “Hakuna mtu ashoneaye kiraka cha nguo mpya kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, kile kiraka kipya kitachanika kutoka ile nguo iliyochakaa, nayo itachanika zaidi.

22 Wala hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, ile divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo hiyo divai itamwagika na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya.”

Luka 5:33–39

5:33 Wakamwambia Yesu, “Wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo mara kwa mara hufunga na kuomba, lakini wanafunzi wako wanaendelea kula na kunywa.”

34 Yesu akawajibu, “Je, mnaweza kuwafanya wageni wa bwana arusi kufunga wakati yuko pamoja nao?

35 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.”

36 Yesu akawapa mfano huu, akawaambia: “Hakuna mtu achanaye kiraka kutoka kwenye nguo mpya na kukishonea kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, atakuwa amechana nguo mpya, na kile kiraka hakitalingana na ile nguo iliyochakaa.

37 Hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, hiyo divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo yote itamwagika. 38 Divai mpya lazima iwekwe kwenye viriba vipya. 39 Wala hakuna mtu anayependelea divai mpya baada ya kunywa divai ya zamani, bali husema, ‘Ile ya zamani ni nzuri zaidi.’ ”