Sehemu ya 8: Yesu Anawafundisha Wale Kumi na Wawili Katika Maeneo Yanayozunguka Galilaya

Mafunzo maalumu ya wale Kumi na Wawili katika wilaya zinazozunguka Galilaya.

Yaelekea kuanzia Pasaka ya mwaka wa 29 BK hadi karibu na Sikukuu ya Vibanda ya mwaka wa 29 BK, au mwaka mmoja mapema (miezi sita, kuanzia majira ya kuchipua hadi majira ya kupukutika kwa majani). Mwaka mmoja tu kutoka mwanzo wa kipindi hiki hadi Kusulubiwa. Sasa mkazo uko kwa Mfalme wa Ufalme (nafsi ya Masiya)

Kuondoka Galilaya katika nyakati nne tofauti kunaelezwa. Ona kwamba kila mara anakaa nje ya eneo la Herode, na kila mara anaenda milimani.

Yesu Anawalisha Watu Elfu Tano

Kuondoka kwa kwanza kwenda faraghani: wale Kumi na Wawili wanarudi, na Yesu anaondoka nao kwenda ng'ambo ya ziwa ili kupumzika. Kulishwa kwa watu elfu tano.

29 au 28 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 14:13–21

14:13 Yesu aliposikia yaliyokuwa yametukia, aliondoka kwa chombo akaenda mahali pasipo na watu ili awe peke yake. Lakini watu walipopata habari, wakamfuata kwa miguu kupitia nchi kavu kutoka miji.

14 Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao.

15 Ilipofika jioni, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na muda sasa umekwisha. Waage makutano ili waende zao vijijini wakajinunulie chakula.”

16 Yesu akawaambia, “Hakuna sababu ya wao kuondoka. Ninyi wapeni chakula.”

17 Wakamjibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu.”

18 Akawaambia, “Nileteeni hivyo vitu hapa.”

19 Yesu akaagiza makutano wakae chini kwenye nyasi. Akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi, nao wanafunzi wakawagawia makutano.

20 Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili.

21 Idadi ya watu waliokula walikuwa wanaume wapatao 5,000, bila kuhesabu wanawake na watoto.

Marko 6:30–44

6:30 Wale mitume wakakusanyika kwa Yesu na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha. 31 Basi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika.”

32 Hivyo wakaondoka kwa mashua peke yao, wakaenda mahali pasipo na watu.

33 Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakaenda haraka kwa miguu kutoka miji yote, nao wakatangulia kufika. 34 Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.

35 Mchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, nazo saa zimekwenda sana.

36 Waage watu ili waende mashambani na vijijini jirani, wakajinunulie chakula.”

37 Lakini Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”

Wakamwambia, “Je, twende tukanunue mikate ya dinari 200 ili tuwape watu hawa wale?”

38 Akawauliza, “Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.”

Walipokwisha kujua wakarudi, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.”

39 Kisha Yesu akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani,

40 nao wakaketi kwenye makundi ya watu mia mia na wengine hamsini hamsini.

41 Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili.

42 Watu wote wakala, wakashiba. 43 Nao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili.

44 Idadi ya wanaume waliokula walikuwa 5,000.

Luka 9:10–17

9:10 Mitume wake waliporudi, wakamweleza Yesu yote waliyofanya. Akawachukua, akaenda nao faraghani mpaka mji uitwao Bethsaida.

11 Lakini umati wa watu ukafahamu alikokwenda, ukamfuata. Akawakaribisha na kunena nao kuhusu Ufalme wa Mungu na kuwaponya wale wote waliokuwa wanahitaji uponyaji.

12 Ilipokaribia jioni, wale mitume kumi na wawili wakaenda kwa Yesu na kumwambia, “Waage makutano ili waende vijijini jirani na mashambani, ili wapate chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tuko nyikani.”

13 Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”

Nao wakajibu, “Hatuna zaidi ya mikate mitano na samaki wawili. Labda twende tukanunue chakula cha kuwatosha watu hawa wote.”

14 Walikuwako wanaume wapatao 5,000.

Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Waketisheni katika makundi ya watu hamsini hamsini.”

15 Wanafunzi wakafanya hivyo, wakawaketisha wote.

16 Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akavibariki na kuvimega. Kisha akawapa wanafunzi ili wawagawie watu.

17 Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili.

Yohana 6:1–13

6:1 Baada ya haya, Yesu alikwenda ngʼambo ya Bahari ya Galilaya, ambayo pia huitwa Bahari ya Tiberia.

2 Umati mkubwa wa watu uliendelea kumfuata, kwa sababu waliona ishara nyingi za miujiza alizofanya kwa wagonjwa. 3 Kisha Yesu akapanda mlimani akaketi huko pamoja na wanafunzi wake.

4 Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.

5 Yesu alipotazama na kuuona ule umati mkubwa wa watu ukimjia, akamwambia Filipo, “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?”

6 Aliuliza swali hili kumpima, kwa maana alishajua la kufanya.

7 Filipo akamjibu, “Hata fedha kiasi cha dinari mia mbili, hazitoshi kununua mikate ya kuwapa watu hawa ili kila mtu apate kidogo.”

8 Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, ndugu yake Simoni Petro, akamwambia,

9 “Hapa kuna mvulana mmoja mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Lakini hivi vitatosha nini kwa umati huu wote?”

10 Yesu akasema, “Waketisheni watu chini.” Palikuwa na majani mengi katika eneo lile, nao watu wakaketi. Palikuwa na wanaume wapatao 5,000.

11 Ndipo Yesu akachukua ile mikate, akamshukuru Mungu na kuwagawia wale watu waliokuwa wameketi. Akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Kila mtu akapata kadiri alivyotaka.

12 Watu wote walipokwisha kula na kushiba, akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki vya ile mikate, kisipotee chochote.”

13 Hivyo wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vya ile mikate mitano ya shayiri na samaki wale wawili wadogo vilivyobakishwa na waliokula.