Mpango wa Kumfanya Yesu Mfalme Unazuiwa
Mpango wa kimapinduzi wa kumtangaza Yesu kuwa mfalme (Masiya wa kisiasa) unazuiwa.
29 au 28 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 14:22–23
14:22 Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua watangulie kwenda ngʼambo ya bahari, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale makutano.
23 Baada ya kuwaaga, akaenda zake mlimani peke yake kuomba. Jioni ilipofika, Yesu alikuwa huko peke yake.
Marko 6:45–46
6:45 Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua watangulie kwenda Bethsaida, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale makutano.
46 Baada ya kuwaaga wale watu, akaenda mlimani kuomba.
Yohana 6:14–15
6:14 Baada ya watu kuona muujiza ule Yesu aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!”
15 Yesu akijua kwamba walitaka kuja kumfanya awe mfalme wao, kwa nguvu, akajitenga nao akaenda milimani peke yake.
Kristo Anawajia Wale Kumi na Wawili Juu ya Maji
Wale Kumi na Wawili wako hatarini katika dhoruba baharini, na Kristo anawajia juu ya maji gizani.
Mathayo 14:24–33
14:24 Wakati huo ile mashua ilikuwa mbali kutoka nchi kavu ikisukwasukwa na mawimbi, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho.
25 Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji.
26 Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa.
27 Lakini mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.”
28 Petro akamjibu, “Bwana, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.”
29 Yesu akamwambia, “Njoo.”
Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Yesu. 30 Lakini alipoona upepo mkali aliingiwa na hofu, naye akaanza kuzama, huku akipiga kelele, “Bwana, niokoe!”
31 Mara Yesu akaunyoosha mkono wake na kumshika, akamwambia, “Wewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?”
32 Nao walipoingia ndani ya mashua, upepo ukakoma. 33 Ndipo wote waliokuwa ndani ya ile mashua wakamwabudu Yesu, wakisema, “Hakika, wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”
Marko 6:47–52
6:47 Ilipofika jioni, ile mashua ilikuwa imefika katikati ya bahari, na Yesu alikuwa peke yake katika nchi kavu.
48 Akawaona wanafunzi wake wanahangaika na kupiga makasia kwa nguvu, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake, akiwa anatembea juu ya maji. Alikuwa karibu kuwapita,
49 lakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu. Wakapiga yowe, 50 kwa sababu wote walipomwona waliogopa.
Mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope!”
51 Akapanda ndani ya mashua nao, na ule upepo ukakoma! Wakashangaa kabisa, 52 kwa kuwa walikuwa hawajaelewa kuhusu ile mikate. Mioyo yao ilikuwa migumu.
Yohana 6:16–21
6:16 Ilipofika jioni, wanafunzi wake waliteremka kwenda baharini.
17 Wakaingia kwenye mashua, wakaanza kuvuka bahari kwenda Kapernaumu. Wakati huu kulikuwa tayari giza na Yesu alikuwa hajajumuika nao. 18 Bahari ikachafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma.
19 Wanafunzi walipokuwa wamekwenda mwendo wa karibu maili tatu au nne, walimwona Yesu akitembea juu ya maji akikaribia mashua, nao wakaogopa sana. 20 Lakini Yesu akawaambia, “Ni mimi. Msiogope.”
21 Ndipo wakamkaribisha kwa furaha ndani ya mashua, na mara wakafika ufuoni walikokuwa wakienda.
Yesu Anakaribishwa Genesareti
Mathayo 14:34–36
14:34 Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti.
35 Watu wa eneo lile walipomtambua Yesu, walipeleka habari sehemu zote za jirani. Watu wakamletea wagonjwa wao wote, 36 wakamsihi awaruhusu wagonjwa waguse tu pindo la vazi lake, nao wote waliomgusa, wakaponywa.
Marko 6:53–56
6:53 Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. 54 Mara waliposhuka kutoka mashua yao, watu wakamtambua Yesu. 55 Wakaenda katika vijiji vyote upesi, wakawabeba wagonjwa kwenye mikeka ili kuwapeleka mahali popote waliposikia kuwa Yesu yupo.
56 Kila mahali Yesu alipokwenda, iwe vijijini, mijini au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa wao masokoni. Wakamwomba awaruhusu hao wagonjwa waguse japo upindo wa vazi lake. Nao wote waliomgusa waliponywa.