Hofu ya Herode Kuhusu Yesu Inayotokana na Hatia
Herode Antipa, akiwa Tiberia, ana hofu kuhusu Yesu inayotokana na hatia yake, kwa sababu alikuwa amemkata kichwa Yohana Mbatizaji huko Machaerus.
27 hadi 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 14:1–12
14:1 Wakati huo, Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za Yesu, 2 akawaambia watumishi wake, “Huyu ni Yohana Mbatizaji; amefufuka kutoka kwa wafu! Hii ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”
3 Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga na kumweka gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake,
4 kwa kuwa Yohana alikuwa amemwambia Herode: “Si halali kwako kuwa na huyo mwanamke.” 5 Herode alitaka sana kumuua Yohana, lakini akaogopa watu, kwa maana walimtambua kuwa ni nabii.
6 Katika siku ya kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti wa Herodia alicheza mbele ya watu waliohudhuria, akamfurahisha sana Herode,
7 kiasi kwamba aliahidi kwa kiapo kumpa huyo binti chochote angeomba. 8 Huyo binti, akiwa amechochewa na mama yake, akasema, “Nipe kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.”
9 Mfalme akasikitika, lakini kwa sababu ya viapo alivyoapa mbele ya wageni, akaamuru kwamba apatiwe ombi lake.
10 Hivyo akaagiza Yohana Mbatizaji akatwe kichwa mle gerezani. 11 Kichwa chake kikaletwa kwenye sinia, akapewa yule binti, naye akampelekea mama yake.
12 Wanafunzi wa Yohana wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika. Kisha wakaenda wakamwambia Yesu.
Marko 6:14–29
6:14 Mfalme Herode akasikia habari hizi, kwa maana jina la Yesu lilikuwa limejulikana sana. Watu wengine walikuwa wakisema, “Yohana Mbatizaji amefufuliwa kutoka kwa wafu, ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”
15 Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.”
Nao wengine wakasema, “Yeye ni nabii, kama mmojawapo wa wale manabii wa zamani.”
16 Lakini Herode aliposikia habari hizi, akasema, “Huyo ni Yohana Mbatizaji, niliyemkata kichwa, amefufuliwa kutoka kwa wafu!”
17 Kwa kuwa Herode alikuwa ameagiza kwamba Yohana Mbatizaji akamatwe, afungwe na kutiwa gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, ambaye Herode alikuwa amemwoa.
18 Yohana alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuwa na mke wa ndugu yako.” 19 Kwa hiyo Herodia alikuwa amemwekea Yohana kinyongo akataka kumuua. Lakini hakuweza, 20 kwa sababu Herode alimwogopa Yohana akijua kwamba ni mtu mwenye haki na mtakatifu, hivyo akamlinda. Herode alifadhaika sana alipomsikia Yohana, lakini bado alipenda kumsikiliza.
21 Mfalme Herode alifanya karamu kubwa wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake. Akawaalika maafisa wake wakuu, majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa Galilaya. Hatimaye Herodia alipata wasaa aliokuwa akiutafuta.
22 Binti yake Herodia alipoingia na kucheza, akamfurahisha Herode pamoja na wageni wake walioalikwa chakulani.
Mfalme Herode akamwambia yule binti, “Niombe kitu chochote utakacho, nami nitakupa.”
23 Tena akamwahidi kwa kiapo, akamwambia, “Chochote utakachoomba nitakupa, hata kama ni nusu ya ufalme wangu.”
24 Yule binti akatoka nje, akaenda kumuuliza mama yake, “Niombe nini?”
Mama yake akamjibu, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.”
25 Yule binti akarudi haraka kwa mfalme, akamwambia, “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.”
26 Mfalme akasikitika sana, lakini kwa sababu alikuwa ameapa viapo mbele ya wageni wake, hakutaka kumkatalia.
27 Mara mfalme akatuma askari mmojawapo wa walinzi wake kukileta kichwa cha Yohana. Akaenda na kumkata Yohana kichwa humo gerezani, 28 akakileta kichwa chake kwenye sinia na kumpa yule msichana, naye yule msichana akampa mama yake.
29 Wanafunzi wa Yohana walipopata habari hizi, wakaja na kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
Luka 9:7–9
9:7 Basi Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za yote yaliyotendeka. Naye akafadhaika, kwa kuwa baadhi ya watu walikuwa wakisema Yohana Mbatizaji amefufuliwa kutoka kwa wafu.
8 Wengine wakasema Eliya amewatokea, na wengine wakasema kwamba mmoja wa manabii wa kale amefufuka.
9 Herode akasema, “Yohana nilimkata kichwa. Lakini ni nani huyu ambaye ninasikia mambo kama haya kumhusu?” Akatamani sana kumwona.