Mateso na Maangamizi ya Yerusalemu Yanatabiriwa
595 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
22 Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu huko, naye akaniambia, “Simama uende mpaka sehemu tambarare, nami nitasema nawe huko.” 23 Kwa hiyo niliinuka nikaenda mpaka mahali pa tambarare. Utukufu wa Bwana ulikuwa umesimama huko, kama utukufu ule niliouona kando ya Mto Kebari, nami nikaanguka kifudifudi.
24 Ndipo Roho akaja ndani yangu akanisimamisha kwa miguu yangu. Akasema nami akaniambia: “Nenda ukajifungie ndani ya nyumba yako. 25 Nawe, ee mwanadamu, watakufunga kwa kamba, watakufunga ili usiweze kutoka na kuwaendea watu. 26 Nitaufanya ulimi wako ushikamane kwenye kaa la kinywa chako, ili uwe kimya usiweze kuwakemea, wajapokuwa ni nyumba ya kuasi. 27 Lakini nitakaposema nawe, nitafungua kinywa chako nawe utawaambia, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo.’ Yeyote atakayesikiliza na asikilize, na yeyote atakayekataa na akatae; kwa kuwa wao ni nyumba ya kuasi.
4:1 “Mwanadamu, sasa chukua tofali, uliweke mbele yako na uchore juu yake ramani ya mji wa Yerusalemu. 2 Kisha uuzingire: Simamisha askari dhidi yake kuuzunguka, uzunguke kwa majeshi, weka kambi dhidi yake pande zote pamoja na magogo ya kubomolea boma vitani. 3 Kisha chukua bamba la chuma, ukalisimamishe liwe kama ukuta wa chuma kati yako na huo mji, nawe uuelekeze uso wako. Huo mji utakuwa katika hali ya kuzingirwa, nawe utauzingira. Hii itakuwa ishara kwa nyumba ya Israeli.
4 “Kisha ulale kwa upande wako wa kushoto na uweke dhambi za nyumba ya Israeli juu yake. Utazibeba dhambi zao kwa idadi ya siku utakazolala kwa huo upande mmoja. 5 Nimekupangia idadi ya siku kama miaka ya dhambi yao. Kwa hiyo kwa siku 390 utabeba dhambi za nyumba ya Israeli.
6 “Baada ya kumaliza hili, lala chini tena, wakati huu ulale chini kwa upande wa kuume, uchukue dhambi za nyumba ya Yuda. Nimekupangia siku arobaini, siku moja kwa kila mwaka mmoja. 7 Geuza uso wako uelekeze kwenye kuzingirwa kwa Yerusalemu na mkono wako ambao haukuvikwa nguo tabiri dhidi yake. 8 Nitakufunga kwa kamba ili usiweze kugeuka kutoka upande mmoja hadi upande mwingine, mpaka hapo utakapokuwa umetimiza siku za kuzingirwa kwako.
9 “Chukua ngano na shayiri, maharagwe na dengu, mtama na mawele, uviweke na kuvihifadhi vyote kwenye gudulia la kuhifadhia, na uvitumie kujitengenezea mkate. Utaula mkate huo kwa hizo siku 390 utakazokuwa umelala kwa upande mmoja. 10 Pima shekeli ishirini za chakula utakachokula kwa kila siku, nawe utakula kwa wakati uliopangwa. 11 Pia pima maji moja ya sita ya hini, nawe utakunywa kwa wakati uliopangwa. 12 Nawe utakula chakula kama vile ambavyo ungekula mkate wa shayiri, uoke mkate mbele ya macho ya watu, ukitumia kinyesi cha mwanadamu.” 13 Bwana akasema, “Hivi ndivyo watu wa Israeli watakavyokula chakula kilicho najisi miongoni mwa mataifa ninakowapeleka.”
14 Ndipo nikasema, “Sivyo Bwana Mwenyezi! Kamwe mimi sijajitia unajisi. Tangu ujana wangu hadi sasa sijala kamwe kitu chochote kilichokufa au kilichoraruliwa na wanyama wa mwituni. Hakuna nyama yeyote najisi iliyoingia kinywani mwangu.”
15 Akasema, “Vema sana, basi nitakuruhusu uoke mkate wako kwa kutumia kinyesi cha ngʼombe badala ya kinyesi cha mwanadamu.”
16 Ndipo Mungu akaniambia, “Mwanadamu, mimi nitakatilia mbali upatikanaji wa chakula katika Yerusalemu. Watu watakula chakula cha kupimwa kwa wasiwasi pamoja na maji ya kupimiwa kwa kukata tamaa, 17 kwa kuwa chakula na maji vitakuwa adimu. Watastajabiana kila mmoja, nao watadhoofika kwa sababu ya dhambi yao.
5:1 “Mwanadamu, sasa chukua upanga mkali na uutumie kama wembe wa kinyozi ili kunyolea nywele za kichwa chako na ndevu zako. Kisha uchukue mizani ya kupimia ukazigawanye nywele hizo. 2 Wakati siku zako za kuzingirwa zitakapokwisha, choma theluthi moja ya hizo nywele zako kwa moto ndani ya mji. Chukua theluthi nyingine ya hizo nywele uzipige kwa upanga kuuzunguka mji wote na theluthi nyingine ya mwisho utaitawanya kwa upepo. Kwa kuwa nitawafuatia kwa upanga uliofutwa. 3 Lakini chukua nywele chache uzifungie ndani ya pindo la vazi lako. 4 Tena chukua nywele nyingine chache uzitupe motoni uziteketeze. Moto utaenea kutoka humo na kufika katika nyumba yote ya Israeli.
5 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Huu ndio Yerusalemu ambao nimeuweka katikati ya mataifa ukiwa umezungukwa na nchi pande zote. 6 Lakini katika uovu wake umeasi sheria na amri zangu kuliko mataifa na nchi zinazouzunguka. Umeasi sheria zangu wala haukufuata amri zangu.
7 “Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ninyi mmekuwa wakaidi kuliko mataifa yanayowazunguka na hamkufuata amri zangu wala kuzishika sheria zangu. Wala hamkuweza hata kuzifuata kawaida za mataifa yanayowazunguka.
8 “Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo, Mimi mwenyewe, niko kinyume nanyi Yerusalemu, nitawapiga kwa adhabu yangu mbele ya mataifa. 9 Kwa ajili ya sanamu zenu zote za machukizo, nitawafanyia kile ambacho kamwe sijawafanyia kabla wala kamwe sitawafanyia tena. 10 Kwa hiyo katikati yenu baba watakula watoto wao na watoto watakula baba zao. Nitawapiga kwa adhabu, nami nitawatawanya watu wenu walionusurika pande zote za dunia. 11 Kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, kwa kuwa mmenajisi mahali pangu patakatifu kwa sanamu zenu mbaya sana na desturi zenu za machukizo, mimi mwenyewe nitaondoa fadhili zangu kwenu. 12 Theluthi ya watu wako watakufa kwa tauni au kwa njaa humu ndani yako, theluthi nyingine itaanguka kwa upanga nje ya kuta zako, nayo theluthi nyingine nitaitawanya kwenye pande nne kuwafuatia kwa upanga uliofutwa.
13 “Ndipo hasira yangu itakapokoma na ghadhabu yangu dhidi yao itatulia, nami nitakuwa nimelipiza kisasi. Baada ya kuimaliza ghadhabu yangu juu yao, watajua kuwa mimi Bwana nimenena katika wivu wangu.
14 “Nitakuangamiza na kukufanya kitu cha kudharauliwa miongoni mwa mataifa yanayokuzunguka, machoni pa watu wote wapitao karibu nawe. 15 Utakuwa kitu cha kudharauliwa na cha aibu, cha dhihaka, ovyo na kitu cha kutisha kwa mataifa yanayokuzunguka, nitakapokupiga kwa adhabu yangu katika hasira na ghadhabu yangu kwa kukukemea kwa ukali. Mimi Bwana nimesema. 16 Nitakapokupiga kwa mishale yangu ya kufisha na yenye kuharibu ya njaa, nitaipiga ili kukuangamiza. Nitaleta njaa zaidi na zaidi juu yako na kukomesha upatikanaji wa chakula kwako. 17 Nitapeleka njaa na wanyama wa mwituni dhidi yenu, navyo vitawaacha bila watoto. Tauni na umwagaji wa damu utapita katikati yenu, nami nitaleta upanga juu yenu. Mimi Bwana nimenena haya.”