Ezekieli Anapewa Utume (continued)

595 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ezekieli 2:1–3:21

1 Akaniambia, “Mwanadamu, simama kwa miguu yako nami nitasema nawe.” 2 Alipokuwa akiongea nami, Roho akanijia na kunisimamisha wima, nikamsikia akisema nami.

3 Akaniambia: “Mwanadamu, ninakutuma kwa Waisraeli, kwa taifa asi ambalo limeniasi mimi, wao na baba zao wananikosea mimi hadi leo. 4 Watu ambao ninakutuma kwao ni wapotovu na wakaidi. Waambie, ‘Hivi ndivyo anavyosema Bwana Mwenyezi.’ 5 Kama watasikiliza au hawatasikiliza, kwa kuwa wao ni nyumba ya kuasi, watajua nabii amekuwa miongoni mwao. 6 Nawe mwanadamu, usiwaogope wao wala maneno yao, usiogope, ingawa michongoma na miiba vinakuzunguka na unaishi katikati ya nge. Usiogope yale wasemayo wala usitishwe nao, ingawa wao ni nyumba ya uasi. 7 Wewe lazima uwaambie maneno yangu, ikiwa wanasikiliza au hawasikilizi, kwa kuwa wao ni watu waasi. 8 Lakini wewe mwanadamu, sikiliza ninalokuambia. Usiwe mwenye kuasi kama hiyo nyumba ya kuasi. Fungua kinywa chako na ule nikupacho.”

9 Ndipo nikatazama, nami nikaona mkono ulionyooshwa kunielekea. Nao ulikuwa na ukurasa wa kitabu, 10 ambao aliukunjua mbele yangu. Pande zote mbili ulikuwa umeandikwa maneno ya maombolezo, vilio na ole.

3:1 Naye akaniambia, “Mwanadamu, kula kile kilichoko mbele yako, kula huu ukurasa wa kitabu, kisha uende ukaseme na nyumba ya Israeli.” 2 Ndipo nikafungua kinywa changu, naye akanilisha ule ukurasa wa kitabu.

3 Ndipo akaniambia, “Mwanadamu, kula ukurasa huu wa kitabu ninaokupa ujaze tumbo lako.” Kwa hiyo nikaula, ulikuwa mtamu kama asali kinywani mwangu.

4 Kisha akaniambia, “Mwanadamu, sasa nenda katika nyumba ya Israeli ukaseme nao maneno yangu. 5 Hukutumwa kwa taifa lenye maneno ya kutatiza na lugha ngumu, bali kwa nyumba ya Israeli. 6 Sikukutuma kwa mataifa mengi yenye maneno ya kutatiza na lugha ngumu ambao maneno yao hutayaelewa. Hakika ningekutuma kwa watu hao, wangekusikiliza. 7 Lakini nyumba ya Israeli haitakusikiliza kwa kuwa hawako radhi kunisikiliza mimi, kwa kuwa nyumba yote ya Israeli ni wenye vipaji vya nyuso vigumu na mioyo ya ukaidi. 8 Tazama nimefanya uso wako mgumu dhidi ya nyuso zao na kipaji cha uso wako kigumu dhidi ya vipaji vya nyuso zao. 9 Kama vile almasi ilivyo ngumu kuliko gumegume, ndivyo nilivyokifanya kipaji cha uso wako. Usiwaogope wala usiwahofu, ijapokuwa ni nyumba ya kuasi.”

10 Naye akaniambia, “Mwanadamu, sikiliza kwa makini na uyatie moyoni mwako maneno yote nitakayosema nawe. 11 Kisha nenda kwa watu wa taifa lako walio uhamishoni, ukaseme nao. Waambie, ‘Hivi ndivyo Bwana Mwenyezi asemavyo,’ kwamba watasikiliza au hawatasikiliza.”

12 Ndipo Roho akaniinua, nikasikia sauti kubwa nyuma yangu ya ngurumo. (Utukufu wa Bwana na utukuzwe katika mahali pa makao yake!) 13 Ilikuwa ni sauti ya mabawa ya wale viumbe hai yakisuguana moja kwa jingine, sauti kama ya ngurumo. 14 Ndipo Roho aliponiinua na kunipeleka mbali. Nikaenda nikiwa na uchungu na hasira moyoni mwangu, nao mkono wa Bwana ukiwa juu yangu. 15 Nikafika kwa wale watu waliokuwa uhamishoni huko Tel-Abibu karibu na Mto Kebari. Nikakaa miongoni mwao kwa muda wa siku saba, nikiwa nimejawa na mshangao.

16 Mwishoni mwa hizo siku saba neno la Bwana likanijia kusema: 17 “Mwanadamu, nimekufanya uwe mlinzi wa nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo, ukawape onyo litokalo kwangu. 18 Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ na wewe usipomwonya mtu huyo au kumshauri aache njia zake mbaya ili kuokoa maisha yake, huyo mtu mwovu atakufa katika dhambi yake na damu yake nitaidai mkononi mwako. 19 Lakini ukimwonya mtu mwovu naye akakataa kuacha uovu wake na njia zake mbaya, atakufa katika dhambi yake, lakini wewe utakuwa umejiokoa nafsi yako.

20 “Tena, mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda maovu, nami nikaweka kikwazo mbele yake mtu huyo atakufa. Kwa kuwa hukumwonya, atakufa katika dhambi yake. Mambo ya haki aliyotenda, hayatakumbukwa, damu yake nitaidai mkononi mwako. 21 Lakini ukimwonya mwenye haki asitende dhambi na akaacha kutenda dhambi, hakika ataishi kwa sababu alipokea maonyo na utakuwa umejiokoa nafsi yako.”