Mateso na Maangamizi ya Yerusalemu Yanatabiriwa (continued)

595 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ezekieli 6–7

1 Neno la Bwana likanijia kusema, 2 “Mwanadamu, elekeza uso wako kukabili milima ya Israeli, utabiri dhidi yake 3 na useme: ‘Ee milima ya Israeli, sikia neno la Bwana Mwenyezi. Hili ndilo Bwana Mwenyezi aliambiayo milima na vilima, magenge na mabonde: Ninakaribia kuleta upanga dhidi yenu, nami nitapaharibu mahali penu pote pa juu pa kuabudia miungu. 4 Madhabahu yenu yatabomolewa na madhabahu yenu ya kufukizia uvumba yatavunjavunjwa, nami nitawachinja watu wenu mbele ya sanamu zenu. 5 Nitazilaza maiti za Waisraeli mbele ya sanamu zao, nami nitatawanya mifupa yenu kuzunguka madhabahu yenu. 6 Popote mnapoishi, miji hiyo itafanywa ukiwa na mahali pa juu pa kuabudia miungu patabomolewa, ili madhabahu yenu ifanywe ukiwa na kuharibiwa, sanamu zenu zitavunjavunjwa na kuharibiwa, madhabahu yenu ya kufukizia uvumba yatabomolewa na kila mlichokifanya kitakatiliwa mbali. 7 Watu wenu watachinjwa katikati yenu, nanyi mtatambua Mimi ndimi Bwana.

8 “ ‘Lakini nitawabakiza hai baadhi yenu, kwa kuwa baadhi yenu watanusurika kuuawa watakapokuwa wametawanyika katika nchi na mataifa. 9 Ndipo katika mataifa ambamo watakuwa wamechukuliwa mateka, wale ambao watanusurika watanikumbuka, jinsi ambavyo nimehuzunishwa na mioyo yao ya uzinzi, ambayo imegeukia mbali nami na macho yao ambayo yametamani sanamu zao. Watajichukia wenyewe kwa ajili ya uovu walioutenda na kwa ajili ya desturi zao za kuchukiza. 10 Nao watajua kuwa Mimi ndimi Bwana, sikuwaonya bure kuwa nitaleta maafa hayo yote juu yao.

11 “ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Piga makofi, kanyaga chini kwa mguu na upige kelele, “Ole!” kwa sababu ya maovu yote na machukizo yote yanayofanywa na nyumba ya Israeli, kwa kuwa wataanguka kwa upanga, njaa na tauni. 12 Yeye aliye mbali sana atakufa kwa tauni, naye aliye karibu atauawa kwa upanga, naye yule atakayenusurika na kubaki atakufa kwa njaa. Hivyo ndivyo nitakavyotimiza ghadhabu yangu dhidi yao. 13 Nao watajua kwamba Mimi ndimi Bwana, wakati maiti za watu wao zitakapokuwa zimelala katikati ya sanamu zao kuzunguka madhabahu yao, juu ya kila kilima kilichoinuka na juu ya vilele vyote vya milima, chini ya kila mti uliotanda na kila mwaloni wenye majani, yaani, sehemu walizofukizia uvumba kwa sanamu zao zote. 14 Nami nitanyoosha mkono wangu dhidi yao na kuifanya nchi yao ukiwa, kuanzia jangwani hadi Dibla, kila mahali wanapoishi. Ndipo watakapojua ya kwamba Mimi ndimi Bwana.’ ”

7:1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo kwa nchi ya Israeli: Mwisho! Mwisho umekuja juu ya pembe nne za nchi. 3 Sasa mwisho umekuja juu yenu nami nitamwaga hasira yangu dhidi yenu. Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za kuchukiza. 4 Sitawaonea huruma wala sitawarehemu, hakika nitalipiza kwa ajili ya matendo yenu na desturi zenu za machukizo miongoni mwenu. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.

5 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Maafa! Maafa ambayo hayajasikiwa yanakuja. 6 Mwisho umewadia! Mwisho umewadia! Umejiinua wenyewe dhidi yenu. Umewadia! 7 Maangamizi yamekuja juu yenu, ninyi mnaoishi katika nchi. Wakati umewadia, siku imekaribia, kuna hofu kuu ya ghafula, wala si furaha, juu ya milima. 8 Ninakaribia kumwaga ghadhabu yangu juu yenu na kumaliza hasira yangu dhidi yenu, nitawahukumu sawasawa na matendo yenu na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za machukizo. 9 Sitawaonea huruma wala sitawarehemu; nitawalipiza sawasawa na matendo yenu na desturi zenu za machukizo miongoni mwenu. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana ambaye huwapiga kwa mapigo.

10 “Siku imefika! Imewadia! Maangamizi yamezuka ghafula, fimbo imechanua majivuno yamechipua! 11 Jeuri imeinuka kuwa fimbo ya kuadhibu uovu, hakuna hata mmoja wa hao watu atakayeachwa, hata mmoja wa kundi lile, hakuna utajiri, hakuna chenye thamani. 12 Wakati umewadia, siku imefika. Mnunuzi na asifurahi wala muuzaji asihuzunike, kwa maana ghadhabu iko juu ya kundi lote. 13 Muuzaji hatajipatia tena ardhi aliyoiuza wakati wote wawili wangali hai, kwa kuwa maono kuhusu kundi lote hayatatanguka. Kwa sababu ya dhambi zao, hakuna hata mmoja atakayeokoa maisha yake. 14 Wajapopiga tarumbeta na kuweka kila kitu tayari, hakuna hata mmoja atakayekwenda vitani, kwa maana ghadhabu yangu iko juu ya kundi lote.

15 “Nje ni upanga, ndani ni tauni na njaa, wale walioko shambani watakufa kwa upanga, nao wale waliomo mjini njaa na tauni vitawala. 16 Wale wote watakaopona na kutoroka watakuwa milimani, wakiomboleza kama hua wa mabondeni, kila mmoja kwa sababu ya dhambi zake. 17 Kila mkono utalegea na kila goti litakuwa dhaifu kama maji. 18 Watavaa nguo ya gunia na kufunikwa na hofu. Nyuso zao zitafunikwa na aibu na nywele za vichwa vyao zitanyolewa. 19 Watatupa fedha yao barabarani, nayo dhahabu yao itakuwa najisi. Fedha yao na dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Bwana. Hawatashibisha njaa yao au kujaza matumbo yao kwa hiyo fedha wala dhahabu, kwa sababu imewaponza wajikwae dhambini. 20 Walijivunia vito vyao vizuri na kuvitumia kufanya sanamu za machukizo na vinyago vya upotovu. Kwa hiyo nitavifanya vitu hivyo kuwa najisi kwao. 21 Nitavitia vyote mikononi mwa wageni kuwa nyara na kuwa vitu vilivyotekwa mikononi mwa watu waovu wa dunia, nao watavinajisi. 22 Nitageuza uso wangu mbali nao, nao waovu wa dunia watapanajisi mahali pangu pa thamani, wanyangʼanyi watapaingia na kupanajisi.

23 “Andaa minyororo, kwa sababu nchi imejaa umwagaji wa damu na mji umejaa udhalimu. 24 Nitaleta taifa ovu kuliko yote ili kumiliki nyumba zao, nitakomesha kiburi cha wenye nguvu na mahali pao patakatifu patatiwa unajisi. 25 Hofu ya ghafula itakapokuja, watatafuta amani, lakini haitakuwepo. 26 Maafa juu ya maafa yatakuja, tetesi ya mabaya juu ya tetesi ya mabaya. Watajitahidi kupata maono kutoka kwa nabii, mafundisho ya sheria toka kwa kuhani yatapotea, vivyo hivyo shauri kutoka kwa wazee. 27 Mfalme ataomboleza, mwana wa mfalme atavikwa kukata tamaa, nayo mikono ya watu wa nchi itatetemeka. Nitawashughulikia sawasawa na matendo yao na kwa kanuni zao wenyewe nitawahukumu. Ndipo watajua kwamba Mimi ndimi Bwana.”