Hadadi Anatoroka (continued)
1040 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Wimbo. Zaburi ya Daudi.
1 Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti;
nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote.
2 Amka, kinubi na zeze!
Nitayaamsha mapambazuko.
3 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, katikati ya mataifa;
nitaimba habari zako, katikati ya jamaa za watu.
4 Kwa maana upendo wako ni mkuu, ni juu kuliko mbingu;
uaminifu wako unazifikia anga.
5 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
utukufu wako na uenee duniani kote.
6 Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume,
ili wale uwapendao wapate kuokolewa.
7 Mungu amenena kutoka patakatifu pake:
“Nitaigawa Shekemu kwa ushindi
na kulipima Bonde la Sukothi.
8 Gileadi ni yangu, Manase ni yangu,
Efraimu ni kofia yangu ya chuma,
nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala.
9 Moabu ni sinia langu la kunawia,
juu ya Edomu natupa kiatu changu;
nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.”
10 Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome?
Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu?
11 Ee Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi,
na hutoki tena na majeshi yetu?
12 Tuletee msaada dhidi ya adui,
kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.
13 Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi,
naye atawaponda adui zetu.
1 Baada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, naye akautwaa Gathi pamoja na vijiji vinavyouzunguka kutoka utawala wa Wafilisti.
2 Pia Daudi akawashinda Wamoabu, wakawa watumishi wake, nao wakawa wanamletea ushuru.
3 Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mfalme wa Soba, hadi Hamathi, wakati alikwenda kuimarisha utawala wake katika Mto Frati. 4 Daudi akateka magari ya vita 1,000 miongoni mwa magari yake, waendesha hayo magari ya kukokotwa na farasi 7,000 na askari wa miguu 20,000. Daudi akakata mishipa ya miguu ya nyuma ya farasi wote wakokotao magari, ila akabakiza 100.
5 Waaramu wa Dameski, walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua 22,000 miongoni mwao. 6 Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski. Basi Waaramu wakawa watumwa wa Daudi, na kumlipa ushuru. Bwana akampa Daudi ushindi kote alipokwenda.
7 Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa za maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu. 8 Kutoka miji ya Tibhathi na Kuni, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi sana, ambayo Solomoni aliitumia kutengenezea ile Bahari ya shaba, zile nguzo na vifaa mbalimbali vya shaba.
9 Tou mfalme wa Hamathi aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri mfalme wa Soba, 10 akamtuma mwanawe, Hadoramu kwa Mfalme Daudi ili kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake katika vita dhidi ya Mfalme Hadadezeri, kwa kuwa alikuwa amepigana vita mara nyingi na Tou. Hadoramu akamletea Daudi vifaa mbalimbali vya dhahabu, fedha na shaba.
11 Mfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa Bwana kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu aliyokuwa ameitwaa katika mataifa yote haya: Edomu na Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki.
13 Akaweka kambi za askari walinzi huko Edomu, nao Waedomu wote wakawa watumishi wa Daudi. Bwana akampa Daudi ushindi kila alipokwenda.
14 Daudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote. 15 Yoabu mwana wa Seruya alikuwa jemadari wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu; 16 Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Shausha alikuwa mwandishi; 17 naye Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa msimamizi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa maafisa wakuu katika utumishi wa mfalme.