Vita na Mataifa Yanayozunguka

1040 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Samweli 8:1–12

1 Baada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, naye akautwaa Metheg-Amma kutoka mikononi mwa Wafilisti.

2 Pia Daudi akawashinda Wamoabu. Akawafanya walale chini kwa mstari akawapima kwa urefu wa kamba. Kila alipopima urefu wa hiyo kamba mara mbili hilo kundi waliuawa na alipopima mara ya tatu aliwaacha hai. Kwa hiyo Wamoabu wakawa chini ya Daudi nao wakamletea kodi.

3 Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kurudisha tena utawala wake kwenye eneo la Mto Frati. 4 Daudi akateka magari yake ya vita 1,000, askari wapanda farasi 7,000 na askari 20,000 watembeao kwa miguu. Daudi akawakata wale farasi wote wakokotao magari mishipa ya miguu, isipokuwa farasi 100 hakuwakata.

5 Waaramu wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua 22,000 miongoni mwao. 6 Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski, nao Waaramu wakawa watumwa wake na kumlipa ushuru. Bwana akampa Daudi ushindi kote alipokwenda.

7 Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa za maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu. 8 Kutoka miji ya Beta na Berothai, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Mfalme Daudi akatwaa shaba nyingi sana.

9 Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri, 10 akamtuma mwanawe Yoramu kwa Mfalme Daudi kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake katika vita dhidi ya Hadadezeri, kwa kuwa Hadadezeri alikuwa amepigana vita na Tou. Yoramu akamletea Daudi vyombo vya fedha, dhahabu na shaba.

11 Mfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa Bwana, kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu kutoka kwa mataifa yote aliyokuwa ameyashinda: 12 yaani Edomu, Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki. Pia akaweka wakfu nyara alizoteka kutoka kwa Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba.

1 Nyakati 18:12

12 Abishai mwana wa Seruya akawaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi.

2 Samweli 8:14–18

14 Akaweka kambi za askari walinzi katika Edomu yote, nao Waedomu wakawa chini ya Daudi. Bwana alimpatia Daudi ushindi kila alipokwenda.

15 Daudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote. 16 Yoabu mwana wa Seruya alikuwa jemadari wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu; 17 Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Seraya alikuwa mwandishi; 18 Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa msimamizi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa washauri wa mfalme.

2 Samweli 8:13

13 Naye Daudi akapata sifa baada ya kurudi kutoka kuwaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi.

Hadadi Anatoroka

1 Wafalme 11:15–20

15 Huko nyuma wakati Daudi alipokuwa akipigana na Edomu, Yoabu jemadari wa jeshi, aliyekuwa amekwenda kuzika waliouawa, alikuwa amewaua wanaume wote waliokuwako Edomu. 16 Yoabu na Waisraeli wote walikaa huko kwa miezi sita, mpaka walipomaliza kuwaangamiza wanaume wote huko Edomu. 17 Lakini Hadadi, akiwa bado mvulana mdogo, alikimbilia Misri akiwa na baadhi ya maafisa wa Kiedomu waliokuwa wakimhudumia baba yake. 18 Wakaondoka Midiani wakaenda Parani. Basi wakichukua pamoja nao wanaume kutoka Parani, wakaenda Misri, kwa Farao mfalme wa Misri, ambaye alimpa Hadadi nyumba, ardhi na akampatia chakula.

19 Farao akapendezwa sana na Hadadi hata akampa ndugu wa mkewe mwenyewe, Malkia Tapenesi, ili aolewe na Hadadi. 20 Huyo ndugu wa Tapenesi akamzalia mwana aliyeitwa Genubathi, ambaye alilelewa na Tapenesi katika jumba la kifalme. Huko Genubathi aliishi pamoja na watoto wa Farao mwenyewe.

Zaburi 60

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Shushani Eduthi.” Utenzi wa Daudi wa kufundisha. Wakati alipopigana na Waaramu kutoka Aramu-Naharaimu na Aramu-Soba, naye Yoabu akarudi nyuma na kuwaua Waedomu 12,000 katika Bonde la Chumvi.

1 Ee Mungu, umetukataa na kutokea ghafula juu yetu,

umekasirika: sasa turejeshe upya!

2 Umetetemesha nchi na kuipasua;

uiponye mavunjiko yake, kwa maana inatetemeka.

3 Umewaonyesha watu wako nyakati za kukata tamaa;

umetunywesha mvinyo unaotuyumbisha.

4 Kwa wale wanaokucha wewe,

umewainulia bendera,

ili iweze kutwekwa dhidi ya upinde.

5 Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume,

ili wale uwapendao wapate kuokolewa.

6 Mungu amenena kutoka patakatifu pake:

“Nitaigawa Shekemu kwa ushindi

na kulipima Bonde la Sukothi.

7 Gileadi ni yangu na Manase ni yangu;

Efraimu ni kofia yangu ya chuma,

nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala.

8 Moabu ni sinia langu la kunawia,

juu ya Edomu natupa kiatu changu;

nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.”

9 Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome?

Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu?

10 Ee Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi,

na hutoki tena na majeshi yetu?

11 Tuletee msaada dhidi ya adui,

kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.

12 Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi,

naye atawaponda adui zetu.