Wema wa Daudi kwa Familia ya Sauli
Wema wa Daudi kwa familia ya Sauli. Vita na Waamoni.
1040 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Daudi akauliza, “Je, hakuna mtu hata mmoja wa nyumba ya Sauli aliyebaki ambaye naweza kumtendea wema kwa ajili ya Yonathani?”
2 Basi palikuwepo mtumishi wa nyumba ya Sauli aliyeitwa Siba. Wakamwita aje mbele ya Daudi, naye mfalme akamwambia, “Wewe ndiwe Siba?”
Akamjibu, “Naam, mimi ndiye mtumishi wako.”
3 Mfalme akauliza, “Je, hakuna yeyote ambaye amebaki wa nyumba ya Sauli ninayeweza kumwonyesha wema wa Mungu?”
Siba akamjibu mfalme, “Bado yupo mwana wa Yonathani, yeye ni kiwete miguu yote.”
4 Mfalme akauliza, “Yuko wapi?”
Siba akajibu, “Yuko nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-Debari.”
5 Basi Mfalme Daudi akamtaka aletwe kutoka Lo-Debari, kutoka nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli.
6 Mefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, alipofika kwa Daudi, akainama kumpa mfalme heshima.
Daudi akamwita, “Mefiboshethi!”
Mefiboshethi akajibu, “Ndimi mtumishi wako.”
7 Daudi akamwambia, “Usiogope, kwa maana hakika nitakutendea wema kwa ajili ya baba yako Yonathani. Nitakurudishia ardhi yote iliyokuwa mali ya Sauli baba yako, nawe daima utakula chakula mezani pangu.”
8 Mefiboshethi akasujudu akasema, “Mimi mtumishi wako ni nini hata uangalie mbwa mfu kama mimi?”
9 Ndipo mfalme akamwita Siba mtumishi wa Sauli na kumwambia, “Nimempa mwana wa bwana wako kila kitu kilichokuwa mali ya Sauli na jamaa yake. 10 Wewe, wanao na watumishi wako mtamlimia mashamba Mefiboshethi na kumletea mavuno, ili kwamba mwana wa bwana wako apate mahitaji yake. Naye Mefiboshethi mwana wa bwana wako atakula chakula mezani pangu daima.” (Siba alikuwa na wana kumi na watano, na watumishi ishirini.)
11 Ndipo Siba akamwambia mfalme, “Mtumishi wako atafanya chochote bwana wangu mfalme atakachoagiza mtumishi wake kufanya.” Basi Mefiboshethi akala chakula mezani pa Daudi kama mmoja wa wana wa mfalme.
12 Mefiboshethi alikuwa na mwanawe mdogo aliyeitwa Mika, nao watu wote wa nyumba ya Siba walikuwa watumishi wa Mefiboshethi. 13 Naye Mefiboshethi akaishi huko Yerusalemu, kwa sababu daima alikula mezani pa mfalme, naye alikuwa kiwete miguu yote.
10:1 Baada ya muda, mfalme wa Waamoni akafa, naye Hanuni mwanawe akaingia mahali pake. 2 Daudi akawaza, “Nitamtendea wema Hanuni mwana wa Nahashi, kama vile baba yake alivyonitendea mimi wema.” Hivyo Daudi akatuma wajumbe kuonyesha wema wake kwa Hanuni kuhusu baba yake.
Watu wa Daudi walipofika katika nchi ya Waamoni, 3 wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni bwana wao, “unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kukutumia watu ili kuonyesha masikitiko? Je, Daudi hakuwatuma watu hawa kuchunguza na kuupeleleza mji ili kuupindua?” 4 Basi Hanuni akawakamata watu wa Daudi, akawanyoa kila mmoja ndevu zake nusu, akakata mavazi yao nyuma katikati kwenye matako, akawaacha waende zao.
5 Daudi alipoambiwa jambo hili, akatuma wajumbe ili kwenda kuwalaki, kwa maana walikuwa wamevunjiwa heshima sana. Mfalme akasema, “Kaeni huko Yeriko mpaka ndevu zenu ziote ndipo mje.”
6 Waamoni walipotambua kuwa wamekuwa machukizo kwa Daudi, wakaajiri askari wa miguu 20,000 Waaramu kutoka Beth-Rehobu na Soba, pia mfalme wa Maaka pamoja na watu 1,000, na vilevile watu 12,000 kutoka Tobu.
7 Daudi aliposikia jambo hili, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji. 8 Waamoni wakatoka wakajipanga wakiwa tayari kwa vita langoni la mji wao, wakati Waaramu wa Soba, wa Rehobu, watu wa Tobu na Maaka walikuwa peke yao kwenye eneo la wazi.
9 Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; kwa hiyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli akavipanga dhidi ya Waaramu. 10 Akawaweka waliobaki chini ya uongozi wa Abishai nduguye na kuwapanga dhidi ya Waamoni. 11 Yoabu akasema, “Kama Waaramu watanizidi nguvu, basi itawabidi mje kunisaidia. Lakini kama Waamoni watawazidi nguvu, basi nitakuja kuwasaidia. 12 Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. Bwana atafanya lile lililo jema machoni pake.”
13 Basi Yoabu na vikosi vyake wakasonga mbele kupigana na Waaramu, nao Waaramu wakakimbia mbele yake. 14 Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao wakakimbia mbele ya Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi kutoka kupigana na Waamoni na kufika Yerusalemu.
15 Baada ya Waaramu kuona wameshindwa na Israeli, wakajikusanya tena. 16 Hadadezeri akaagiza Waaramu walioletwa kutoka ngʼambo ya Mto Frati, wakaenda Helamu pamoja na Shobaki jemadari wa jeshi la Hadadezeri akiwaongoza.
17 Daudi alipoambiwa haya, akawakusanya Israeli wote, wakavuka Mto Yordani, wakaenda Helamu. Waaramu wakapanga vikosi vyao vya askari kukabiliana na kupigana dhidi ya Daudi. 18 Lakini Waaramu wakakimbia mbele ya Israeli, naye Daudi akawaua waendesha magari mia saba na askari wao wa miguu 40,000. Vilevile alimpiga Shobaki jemadari wa jeshi lao, naye akafa huko. 19 Wafalme wote waliokuwa wanamtumikia Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, wakafanya amani na Waisraeli na wakawa chini yao.
Hivyo Waaramu wakaogopa kuwasaidia Waamoni tena.
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
1 Bwana na akujibu unapokuwa katika dhiki,
jina la Mungu wa Yakobo na liwe kinga yako.
2 Na akutumie msaada kutoka patakatifu
na akupatie msaada kutoka Sayuni.
3 Na azikumbuke dhabihu zako zote,
na azikubali sadaka zako za kuteketezwa.
4 Na akujalie haja ya moyo wako,
na aifanikishe mipango yako yote.
5 Tutashangilia kwa furaha utakaposhinda,
tutainua bendera zetu kwa jina la Mungu wetu.
Bwana na akupe haja zako zote.
6 Sasa nafahamu kuwa Bwana
humwokoa mpakwa mafuta wake,
humjibu kutoka mbingu yake takatifu
kwa nguvu za wokovu wa mkono wake wa kuume.
7 Wengine wanatumaini magari ya vita, na wengine farasi,
bali sisi tutalitumainia jina la Bwana, Mungu wetu.
8 Wao wameshushwa chini na kuanguka,
bali sisi tunainuka na kusimama imara.
9 Ee Bwana, mwokoe mfalme!
Tujibu tunapokuita!