Wema wa Daudi kwa Familia ya Sauli (continued)
Wema wa Daudi kwa familia ya Sauli. Vita na Waamoni.
1040 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
1 Ee Bwana, mfalme huzifurahia nguvu zako.
Tazama jinsi ilivyo kuu furaha yake
kwa ushindi unaompa!
2 Umempa haja ya moyo wake
na hukumzuilia maombi ya midomo yake.
3 Ulimkaribisha kwa baraka tele
na kumvika taji ya dhahabu safi kichwani pake.
4 Alikuomba maisha, nawe ukampa,
wingi wa siku milele na milele.
5 Kutokana na ushindi uliompa, utukufu wake ni mkubwa,
umeweka juu yake fahari na utukufu.
6 Hakika umempa baraka za milele,
umemfanya awe na furaha
kwa shangwe ya uwepo wako.
7 Kwa kuwa mfalme anamtumaini Bwana;
kwa upendo usiokoma wa Aliye Juu Sana hatatikiswa.
8 Mkono wako utawashika adui zako wote,
mkono wako wa kuume utawakamata adui zako.
9 Wakati utakapojitokeza
utawafanya kama tanuru ya moto.
Katika ghadhabu yake Bwana atawameza,
moto wake utawateketeza.
10 Utawaangamiza wazao wao kutoka duniani,
uzao wao kutoka wanadamu.
11 Ingawa watapanga mabaya dhidi yako
na kutunga hila, hawawezi kufanikiwa,
12 kwa kuwa utawafanya wakimbie
utakapowalenga usoni pao
kwa mshale kutoka kwenye upinde wako.
13 Ee Bwana, utukuzwe katika nguvu zako,
tutaimba na kusifu nguvu zako.
1 Baada ya muda, Nahashi mfalme wa Waamoni akafa, mwanawe akaingia mahali pake. 2 Daudi akawaza, “Nitamtendea wema Hanuni mwana wa Nahashi, kwa sababu baba yake alinitendea wema.”
Hivyo Daudi akatuma wajumbe ili kumfariji Hanuni kwa ajili ya kifo cha baba yake. Watu wa Daudi walipofika kwa Hanuni katika nchi ya Waamoni ili kumfariji, 3 wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni, “Hivi unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kuwatuma wajumbe kukufariji? Je, hawa watu hawakuja kuipeleleza na kuidadisi nchi ili waishinde?” 4 Kwa hiyo Hanuni akawakamata watu wa Daudi, akawanyoa ndevu akakata nguo zao katikati kwenye matako, akawaacha waende zao.
5 Mtu mmoja alipofika na kumpasha Daudi habari za watu hawa, akawatuma wajumbe wengine kuwalaki, kwa maana walikuwa wamevunjiwa heshima sana. Mfalme akasema, “Kaeni huko Yeriko mpaka ndevu zenu ziote, ndipo mje.”
6 Waamoni walipotambua kuwa wamekuwa machukizo kwa Daudi, Hanuni na Waamoni wakatuma talanta 1,000 za fedha ili kukodisha magari ya vita pamoja na waendeshaji wa hayo magari ya kukokotwa na farasi, kutoka Aramu-Naharaimu, Aramu-Maaka na Soba. 7 Wakakodisha magari ya vita 32,000 yakiwa na waendeshaji wake, pamoja na mfalme wa Maaka na vikosi vyake, wakaja na kupiga kambi karibu na Medeba. Waamoni nao wakakusanyika toka miji yao, wakatoka ili kupigana vita.
8 Daudi aliposikia jambo hili, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji. 9 Waamoni wakatoka wakajipanga wakiwa tayari kwa vita langoni la mji wao, wakati wale wafalme wengine waliokuja nao walijipanga kwa vita uwanjani.
10 Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; kwa hiyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli akavipanga dhidi ya Waaramu. 11 Akawaweka wale wanajeshi wengine waliobaki chini ya amri ya Abishai ndugu yake, nao wakapangwa ili wakabiliane na Waamoni. 12 Yoabu akasema, “Kama Waaramu watanizidi nguvu, basi itakupasa wewe unisaidie; lakini kama Waamoni watakuzidi nguvu, basi mimi nitakusaidia. 13 Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. Bwana atafanya lile lililo jema machoni pake.”
14 Basi Yoabu na vikosi vyake wakasonga mbele kupigana na Waaramu, nao Waaramu wakakimbia mbele yake. 15 Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao pia wakakimbia mbele ya nduguye Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi Yerusalemu.
16 Baada ya Waaramu kuona kwamba wameshindwa na Israeli, wakapeleka wajumbe na kuwataka Waaramu wengine kutoka ngʼambo ya Mto Frati, wakiongozwa na Shofaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri.
17 Daudi alipoambiwa haya, akawakusanya Israeli wote na kuvuka Yordani. Akasonga mbele dhidi yao na akajipanga kuwakabili. Daudi akapanga vita ili kupigana na Waaramu, nao wakapigana dhidi yake. 18 Lakini Waaramu wakakimbia mbele ya Israeli, naye Daudi akawaua waendesha magari 7,000 na askari wao wa miguu 40,000. Pia akamuua Shofaki, jemadari wa jeshi lao.
19 Raiya wa Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, wakafanya mapatano ya amani na Daudi, wakawa watumishi wake.
Hivyo Waaramu hawakukubali kuwasaidia Waamoni tena.