Uzinzi wa Daudi
1035 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Mwanzoni mwa mwaka mpya, wakati ambapo wafalme huenda vitani, Yoabu aliliongoza jeshi. Aliangamiza nchi ya Waamoni, na akaenda Raba na kuuzingira, lakini Daudi alibaki Yerusalemu. Yoabu akashambulia Raba na kuuacha ukiwa magofu.
1 Katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati wafalme watokapo kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu pamoja na watu wa mfalme na jeshi lote la Israeli. Wakawaangamiza Waamoni na kuuzunguka kwa jeshi mji wa Raba. Lakini Daudi akabaki Yerusalemu.
2 Ikawa siku moja wakati wa jioni Daudi aliinuka kitandani mwake na kutembeatembea juu ya paa la jumba lake la kifalme. Kutokea kule kwenye paa, akamwona mwanamke akioga. Mwanamke huyo alikuwa mzuri sana wa sura, 3 naye Daudi akatuma mtu mmoja kuuliza habari za huyo mwanamke. Huyo mtu akamwambia Daudi, “Je, huyu si Bathsheba binti Eliamu, naye ni mke wa Uria, Mhiti?” 4 Ndipo Daudi akatuma wajumbe kumleta. Huyo mwanamke akaja kwa Daudi, Daudi akakutana naye kimwili. (Huyo mwanamke ndipo tu alikuwa amejitakasa kutoka siku zake za hedhi.) Kisha akarudi nyumbani kwake. 5 Huyo mwanamke akapata mimba akampelekea Daudi ujumbe, kusema, “Mimi ni mjamzito.”
6 Ndipo Daudi akapeleka ujumbe kwa Yoabu, “Unipelekee Uria, Mhiti.” Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi. 7 Uria alipofika, Daudi akamuuliza habari za Yoabu, hali za askari na vita kwamba inaendeleaje. 8 Kisha Daudi akamwambia Uria, “Teremka nyumbani kwako ukanawe miguu yako.” Basi Uria akaondoka kutoka kwenye jumba la kifalme, tena zawadi zikamfuata kutoka kwa mfalme. 9 Lakini Uria akalala kwenye ingilio la jumba la kifalme pamoja na watumishi wote wa bwana wake, na hakuteremka kwenda nyumbani kwake.
10 Daudi alipoambiwa kwamba, “Uria hakwenda nyumbani,” Daudi akamuuliza, “Je, si ndiyo tu umefika kutoka safari ya mbali? Kwa nini hukwenda nyumbani?”
11 Uria akamwambia Daudi, “Sanduku la Mungu, na Israeli na Yuda wanakaa kwenye mahema, naye bwana wangu Yoabu na watu wa bwana wangu wamepiga kambi mahali pa wazi. Ningewezaje kwenda nyumbani kwangu ili nile, ninywe na kukutana na mke wangu? Hakika kama uishivyo sitafanya jambo la namna hiyo!”
12 Ndipo Daudi akamwambia, “Kaa hapa siku moja zaidi, nami kesho nitakutuma urudi.” Kwa hiyo Uria akakaa Yerusalemu siku ile na siku iliyofuata. 13 Kwa ukaribisho wa Daudi, Uria akala na kunywa pamoja naye, Daudi akamlevya. Lakini jioni Uria alitoka kwenda kulala juu ya mkeka wake miongoni mwa watumishi wa bwana wake, hakwenda nyumbani.
14 Asubuhi yake Daudi akamwandikia Yoabu barua, akamtuma Uria kuipeleka. 15 Ndani ya barua aliandika, “Mweke Uria mstari wa mbele mahali ambapo mapigano ni makali sana. Kisha wewe uondoke ili Uria aangushwe chini na kuuawa.”
16 Hivyo Yoabu alipokuwa ameuzingira mji kwa jeshi, akamweka Uria mahali ambapo alijua kuwa ulinzi wa adui ulikuwa imara sana. 17 Wakati watu wa mjini walipotoka kwenda kupigana dhidi ya Yoabu, baadhi ya watu katika jeshi la Daudi wakauawa, zaidi ya hayo, Uria, Mhiti, akafa.
18 Yoabu akampelekea Daudi maelezo yote ya vita. 19 Akamwagiza mjumbe hivi, “Utakapokuwa umemaliza kumpa mfalme maelezo ya vita, 20 hasira ya mfalme yaweza kuwaka, naye aweza kukuuliza, ‘Kwa nini mlisogea karibu hivyo na mji kupigana? Hamkujua kuwa wangeweza kuwapiga mishale kutoka ukutani? 21 Ni nani aliyemuua Abimeleki mwana wa Yerub-Besheth? Je, mwanamke hakutupa juu yake jiwe la juu la kusagia kutoka ukutani, kwa hiyo akafa huko Thebesi? Kwa nini mlisogea hivyo karibu ya ukuta?’ Ikiwa atakuuliza hivi, ndipo umwambie, ‘Pia mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa.’ ”
22 Mjumbe akaondoka. Alipowasili akamwambia Daudi kila kitu alichokuwa ametumwa na Yoabu kusema. 23 Mjumbe akamwambia Daudi, “Watu walituzidi nguvu wakatoka nje ya mji dhidi yetu kwenye eneo la wazi, lakini tuliwarudisha nyuma mpaka kwenye ingilio la mji. 24 Ndipo wapiga upinde walitupa mishale kwa watumishi wako kutoka ukutani, na baadhi ya watu wa mfalme wakafa. Zaidi ya hayo, Uria, Mhiti, mtumishi wako amekufa.”
25 Daudi akamwambia mjumbe, “Ukamwambie Yoabu hivi, ‘Jambo hili lisikutie wasiwasi, upanga hula huyu sawa na ulavyo mwingine. Zidisha mashambulizi dhidi ya mji na uangamize.’ Mwambie Yoabu hivi ili kumtia moyo.”
26 Mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe amekufa, akamwombolezea. 27 Baada ya muda wa maombolezo kwisha, Daudi akamtaka aletwe nyumbani kwake, naye akawa mkewe, na akamzalia mwana. Lakini jambo alilokuwa amefanya Daudi lilimchukiza Bwana.
12:1 Bwana akamtuma Nathani kwa Daudi. Alipofika kwake akamwambia, “Katika mji mmoja kulikuwepo na watu wawili, mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa maskini. 2 Yule mtu tajiri alikuwa na idadi kubwa sana ya kondoo na ngʼombe, 3 lakini yule maskini hakuwa na chochote ila kondoo jike mdogo aliyekuwa amemnunua. Akamtunza kondoo huyo, akakulia kwake pamoja na watoto wake. Kondoo huyo alishiriki chakula cha bwana wake na kunywea kikombe chake hata pia huyo kondoo alilala mikononi mwa bwana wake. Kwake alikuwa kama binti yake.
4 “Siku moja yule tajiri akafikiwa na mgeni, lakini huyo tajiri akaacha kuchukua mmoja wa kondoo au ngʼombe wake mwenyewe amwandalie mgeni. Badala yake akachukua yule kondoo jike mdogo aliyekuwa mali ya yule maskini na kumwandalia yule mgeni wake.”
5 Daudi akawakwa na hasira dhidi ya mtu huyo tajiri na kumwambia Nathani, “Hakika kama Bwana aishivyo, mtu huyo aliyefanya hivyo anastahili kufa! 6 Lazima alipe mara nne zaidi, kwa ajili ya kondoo huyo, kwa sababu amefanya jambo kama hilo na hakuwa na huruma.”
7 Ndipo Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli, nilikuokoa kutokana na mkono wa Sauli. 8 Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake za bwana wako mikononi mwako. Nikakupa nyumba ya Israeli na Yuda. Kama haya yote yalikuwa madogo sana, ningekupa hata zaidi. 9 Kwa nini ulilidharau neno la Bwana kwa kufanya lililo ovu machoni pake? Ulimuua Uria, Mhiti kwa upanga na kumchukua mke wake awe mkeo. Ulimuua kwa upanga wa Waamoni. 10 Basi kwa hiyo, upanga hautaondoka nyumbani mwako kamwe kwa sababu ulinidharau mimi na kumchukua mke wa Uria, Mhiti kuwa mkeo.’
11 “Hili ndilo asemalo Bwana: ‘Kutoka kwa nyumba yako mwenyewe nitaleta maafa juu yako. Mbele ya macho yako mwenyewe nitatwaa wake zako na kumpa yeye aliye wa karibu nawe, naye atakutana kimwili na wake zako mchana mwangavu. 12 Ulifanya kwa siri, lakini nitalifanya jambo hili wakati wa mchana mwangavu mbele ya Israeli yote.’ ”
13 Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi ya Bwana.”
Nathani akamjibu, “Bwana amekuondolea dhambi yako. Hutakufa. 14 Lakini kwa sababu kwa kufanya hili umefanya adui za Bwana kuonyesha dharau kabisa, mwana atakayezaliwa kwako atakufa.”
15 Baada ya Nathani kurudi nyumbani kwake, Bwana akampiga yule mtoto ambaye mke wa Uria alikuwa amemzalia Daudi, akaugua.
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Baada ya kukemewa na nabii Nathani kwa kuzini na Bathsheba.
1 Ee Mungu, unihurumie,
kwa kadiri ya upendo wako usiokoma,
kwa kadiri ya huruma yako kuu,
uyafute makosa yangu.
2 Unioshe na uovu wangu wote
na unitakase dhambi yangu.
3 Kwa maana ninajua makosa yangu,
na dhambi yangu iko mbele yangu daima.
4 Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi
na kufanya yaliyo mabaya machoni pako,
ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo,
na kuwa na haki utoapo hukumu.
5 Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi,
mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba kwa mama yangu.
6 Hakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni,
ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima.
7 Nioshe kwa hisopo, nami nitakuwa safi,
unisafishe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.
8 Unipe kusikia furaha na shangwe,
mifupa uliyoiponda na ifurahi.
9 Ufiche uso wako usizitazame dhambi zangu,
na uufute uovu wangu wote.
10 Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu.
11 Usinitupe kutoka mbele zako
wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu.
12 Unirudishie tena furaha ya wokovu wako,
unipe roho ya utii, ili initegemeze.
13 Ndipo nitakapowafundisha wakosaji njia zako,
na wenye dhambi watakugeukia wewe.
14 Ee Mungu, Mungu uniokoaye,
niokoe na hatia ya kumwaga damu,
nao ulimi wangu utaimba juu ya haki yako.
15 Ee Bwana, fungua midomo yangu,
na kinywa changu kitatangaza sifa zako.
16 Wewe hupendezwi na dhabihu, au ningaliileta,
hufurahii sadaka za kuteketezwa.
17 Bali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika,
moyo uliovunjika wenye toba,
Ee Mungu, hutaudharau.
18 Kwa wema wa radhi yako uifanye Sayuni istawi,
ukazijenge upya kuta za Yerusalemu.
19 Hapo ndipo kutakapokuwa na dhabihu za haki,
sadaka nzima za kuteketezwa za kukupendeza sana,
pia mafahali watatolewa
madhabahuni mwako.