Vita vya Asa na Baasha

955 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Wafalme 15:16–22

16 Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli siku zote za utawala wao. 17 Mfalme Baasha wa Israeli akashambulia Yuda na kuweka ngome mji wa Rama ili kumzuia yeyote asitoke wala kuingia nchi ya Mfalme Asa wa Yuda.

18 Kisha Asa akachukua fedha yote na dhahabu iliyokuwa imeachwa katika hazina za Hekalu la Bwana na za jumba lake mwenyewe la kifalme. Akawakabidhi maafisa wake na kuwatuma kwa Ben-Hadadi mwana wa Tabrimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Aramu, aliyekuwa akitawala Dameski. 19 “Akasema na pawepo mkataba kati yangu na wewe, kama ulivyokuwepo kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, nimekuletea zawadi ya fedha na dhahabu. Sasa vunja mkataba wako na Baasha mfalme wa Israeli ili aniondokee mimi.”

20 Ben-Hadadi akakubaliana na Mfalme Asa na kutuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Akaishinda miji ya Iyoni, Dani, Abel-Beth-Maaka na Kinerethi yote, pamoja na Naftali. 21 Wakati Baasha aliposikia hili, akaacha kuijenga Rama na akaenda kuishi Tirsa. 22 Kisha Mfalme Asa akatoa amri kwa Yuda yote, pasipo kumbagua hata mmoja, kubeba mawe na mbao kutoka Rama, ambazo Baasha alikuwa akitumia huko. Mfalme Asa akazitumia kujengea Geba iliyoko Benyamini na Mispa pia.

Kifo cha Asa

2 Nyakati 16:7–14

7 Ikawa wakati huo mwonaji Hanani akamjia Mfalme Asa wa Yuda na kumwambia: “Kwa sababu ulimtegemea mfalme wa Aramu nawe hukumtegemea Bwana Mungu wako, jeshi la mfalme wa Aramu limeponyoka mkononi mwako. 8 Je, hukumbuki lililotendeka kwa Wakushi na Walibia, hawakuwa jeshi lenye nguvu na magari mengi ya vita na wapanda farasi? Hata hivyo, ulipomtegemea Bwana yeye aliwatia mkononi mwako. 9 Kwa kuwa macho ya Bwana hukimbiakimbia duniani kote ili kujionyesha mwenye nguvu kwa ajili ya wale ambao mioyo yao inamtegemea kwa ukamilifu. Umefanya jambo la upumbavu na kuanzia sasa na kuendelea utakuwa na vita.”

10 Asa akamkasirikia mwonaji kwa sababu ya jambo hili. Alikuwa ameghadhibika sana hata akamweka gerezani. Wakati huo huo Asa akaanza kuwatesa na kuwaonea baadhi ya watu kwa ukatili.

11 Matukio ya utawala wa Asa, kuanzia mwanzo mpaka mwisho, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli. 12 Katika mwaka wa thelathini na tisa wa utawala wake, Asa alipatwa na ugonjwa kwenye miguu yake. Ingawa ugonjwa wake ulimzidia sana, hata katika kuugua kwake hakutafuta msaada kutoka kwa Bwana bali kwa matabibu tu. 13 Katika mwaka wa arobaini na moja wa utawala wa Asa, alikufa na kulala na baba zake. 14 Nao wakamzika katika kaburi lile alilokuwa amejichongea mwenyewe katika Mji wa Daudi. Wakamzika kwa jeneza lililowekwa vikolezi na mchanganyiko wa manukato ya aina mbalimbali yaliyotengenezwa kwa utaalamu wa mtengeneza marashi, nao wakawasha moto mkubwa kwa heshima yake.

1 Wafalme 15:23–24

23 Kwa matukio yote ya utawala wa Asa, mafanikio yake yote, yote aliyofanya na miji aliyoijenga, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Katika uzee wake, hata hivyo, alipata ugonjwa wa miguu. 24 Kisha Asa akalala pamoja na baba zake na kuzikwa pamoja nao katika mji wa Daudi baba yake. Naye Yehoshafati mwanawe akawa mfalme baada yake.

2 Nyakati 16:1–6

1 Katika mwaka wa thelathini na sita wa utawala wa Asa, Mfalme Baasha wa Israeli akashambulia Yuda na kuweka ngome mji wa Rama ili kumzuia yeyote asitoke wala kuingia nchi ya Mfalme Asa wa Yuda.

2 Ndipo Asa akachukua fedha na dhahabu kutoka hazina ya Hekalu la Bwana na kutoka jumba lake mwenyewe la kifalme na kumpelekea Ben-Hadadi mfalme wa Aramu, ambaye alikuwa anatawala huko Dameski. 3 Akasema, “Pawepo na mkataba kati yangu na wewe, kama ulivyokuwepo kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, nimekuletea fedha na dhahabu. Sasa vunja mkataba wako na Baasha mfalme wa Israeli ili aniondokee mimi.”

4 Ben-Hadadi akakubaliana na Mfalme Asa na kutuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Wakashinda Iyoni, Dani, Abel-Maimu na miji yote ya hazina ya Naftali. 5 Baasha aliposikia jambo hili, akasimamisha kujenga Rama na kuacha kazi yake. 6 Ndipo Mfalme Asa akawaleta watu wote wa Yuda, nao wakachukua mawe na miti ambayo Baasha alikuwa anavitumia huko Rama. Kwa vitu hivyo akajenga Geba na Mispa.

2 Nyakati 15:16–17

16 Mfalme Asa akamwondolea Maaka mama yake wadhifa wake kama mama malkia kwa sababu alikuwa ametengeneza nguzo ya Ashera ya kuchukiza. Asa akaikata hiyo nguzo, akaivunjavunja na kuiteketeza kwa moto katika Bonde la Kidroni. 17 Ijapokuwa hakuondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu katika Israeli, moyo wa Asa ulikuwa umejiweka kwa Bwana kikamilifu maisha yake yote.