Sehemu ya 3: Utawala wa Asa

Ufalme wa Yuda

Kujitoa kwa Asa kwa Mungu

955 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Nyakati 14:1

1 Naye Abiya akalala na baba zake, akazikwa katika Mji wa Daudi. Asa mwanawe akawa mfalme baada yake. Katika siku zake, nchi ikawa na amani kwa miaka kumi.

1 Wafalme 15:9–11

9 Katika mwaka wa ishirini wa utawala wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Asa akawa mfalme wa Yuda, 10 naye akatawala katika Yerusalemu miaka arobaini na mmoja. Bibi yake aliitwa Maaka binti Abishalomu.

11 Asa akatenda yaliyo mema machoni mwa Bwana, kama alivyokuwa ametenda Daudi baba yake.

2 Nyakati 14:2–3

2 Asa akatenda yaliyo mema na haki machoni pa Bwana Mungu wake. 3 Akaziondoa madhabahu za kigeni na mahali pa juu pa kuabudia miungu, akayavunja yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Maashera.

1 Wafalme 15:12–15

12 Akawafukuza mahanithi wa mahali pa kuabudia miungu kutoka nchi na kuondoa sanamu zote ambazo baba zake walikuwa wametengeneza. 13 Hata akamwondoa bibi yake Maaka kwenye wadhifa wake kama mama malkia, kwa sababu alikuwa ametengeneza nguzo ya Ashera ya kuchukiza. Asa akaikata hiyo nguzo na kuiteketeza kwa moto katika Bonde la Kidroni. 14 Ijapokuwa hakuondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu, moyo wa Asa ulikuwa umejiweka kwa Bwana kikamilifu maisha yake yote. 15 Akaleta ndani ya Hekalu la Bwana fedha na dhahabu na vile vyombo ambavyo yeye na baba yake walikuwa wameviweka wakfu.

2 Nyakati 14:4–15

4 Akawaamuru Yuda kumtafuta Bwana, Mungu wa baba zao na kutii sheria zake na amri zake. 5 Akaondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu na madhabahu za kufukizia uvumba kwenye kila mji katika Yuda, nao ufalme ulikuwa na amani katika utawala wake. 6 Akajenga miji yenye ngome katika Yuda, wakati nchi ikiwa na amani. Hakuna mtu yeyote aliyepigana vita naye katika miaka hiyo, kwa kuwa Bwana alimstarehesha.

7 Mfalme akawaambia Yuda, “Tuijenge hii miji na tuizungushie kuta, pamoja na minara, malango na makomeo. Nchi bado ni yetu, kwa sababu tumemtafuta Bwana Mungu wetu, tulimtafuta naye ametupa raha kila upande.” Hivyo wakajenga na wakafanikiwa.

8 Asa alikuwa na jeshi la watu 300,000 kutoka Yuda, wenye ngao kubwa na mikuki na jeshi la watu 280,000 kutoka Benyamini, wenye ngao ndogo na pinde. Watu hawa wote walikuwa wapiganaji mashujaa.

9 Zera Mkushi akatoka kupigana dhidi yao akiwa na jeshi la watu maelfu ya maelfu na magari ya vita 300, nao wakaja mpaka Maresha. 10 Asa akatoka kumkabili, nao wakapanga vita katika Bonde la Sefatha karibu na Maresha.

11 Kisha Asa akamlilia Bwana Mungu wake na kusema, “Ee Bwana, hakuna yeyote aliye kama wewe wa kuwasaidia wasio na nguvu dhidi ya wenye nguvu. Utusaidie, Ee Bwana, wewe ndiwe Mungu wetu, kwa kuwa tunakutumainia wewe, nasi kwa jina lako tumekuja dhidi ya jeshi hili kubwa. Ee Bwana, wewe ndiwe Mungu wetu, usiwaache wanadamu wakushinde wewe.”

12 Bwana akawapiga Wakushi mbele ya Asa na Yuda. Wakushi wakakimbia, 13 naye Asa na jeshi lake wakawafuatia mpaka Gerari. Idadi kubwa ya Wakushi ilianguka hata wasiweze kuinuka tena, wakapondapondwa mbele za Bwana na majeshi yake. 14 Watu wa Yuda wakachukua nyara nyingi sana, wakaangamiza vijiji vyote vinavyoizunguka Gerari, kwa kuwa hofu ya Bwana ilikuwa imewaangukia. Wakateka nyara vijiji hivi vyote, kwani kulikuwepo nyara nyingi huko. 15 Pia wakashambulia kambi za wachunga makundi ya wanyama wakachukua na kuyaswaga makundi ya kondoo, mbuzi na ngamia. Kisha wakarudi Yerusalemu.

Asa Afanya Agano na Mungu

2 Nyakati 15:1–15

1 Roho wa Bwana akamjia Azaria mwana wa Odedi. 2 Akatoka ili kumlaki Asa na kumwambia, “Nisikilizeni, Asa na Yuda wote na Benyamini. Bwana yu pamoja nanyi mkiwa pamoja naye. Kama mkimtafuta, ataonekana kwenu, lakini kama mkimwacha yeye, naye atawaacha ninyi. 3 Kwa muda mrefu Israeli walikuwa hawana Mungu wa kweli, walikuwa hawana kuhani wa kuwafundisha na wala hawakuwa na sheria. 4 Lakini katika taabu yao walimrudia Bwana, Mungu wa Israeli na kumtafuta, naye akaonekana kwao. 5 Katika siku hizo hapakuwa na amani kwa yeyote aliyesafiri, kutoka wala kuingia, kwa kuwa wakazi wote wa nchi walikuwa katika machafuko makubwa. 6 Taifa moja lilipigana na taifa lingine na mji mmoja ukapigana na mji mwingine, kwa sababu Mungu alikuwa anawahangaisha kwa taabu za kila aina. 7 Lakini kwa habari yenu ninyi, kuweni hodari wala msikate tamaa, kwa kuwa mtapata thawabu kwa kazi yenu.”

8 Asa aliposikia maneno haya na unabii wa Azaria mwana wa Odedi nabii, akajipa moyo. Akaziondoa sanamu zote zilizokuwa machukizo katika nchi yote ya Yuda na Benyamini na kutoka miji aliyoiteka ya vilima vya Efraimu. Akakarabati madhabahu ya Bwana iliyokuwa mbele ya ukumbi wa Hekalu la Bwana.

9 Kisha akakutanisha Yuda wote, Benyamini na watu kutoka Efraimu, watu wa Manase na Simeoni waliokuwa wanaishi miongoni mwao, kwa maana idadi kubwa walikuwa wamemjia kutoka Israeli walipoona kwamba Bwana Mungu wake alikuwa pamoja naye.

10 Basi wakakusanyika huko Yerusalemu mwezi wa tatu katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Asa. 11 Wakati huo wakamtolea Bwana dhabihu za ngʼombe 700, kondoo na mbuzi 7,000 kutoka zile nyara walizoteka. 12 Wakafanya agano kumtafuta Bwana, Mungu wa baba zao kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote. 13 Wale wote ambao hawangemtafuta Bwana, Mungu wa Israeli wangelazimika kuuawa, akiwa mdogo au mkubwa, mwanaume au mwanamke. 14 Wakamwapia Bwana kwa sauti kuu, kwa kupiga kelele, tarumbeta na kwa mabaragumu. 15 Yuda wote wakafurahia kile kiapo kwa sababu walikuwa wameapa kwa moyo wao wote. Wakamtafuta Mungu kwa bidii, naye akaonekana kwao. Kwa hiyo Bwana akawastarehesha pande zote.

2 Nyakati 15:18–19

18 Akaleta ndani ya Hekalu la Mungu fedha na dhahabu na vile vyombo ambavyo yeye na baba yake walikuwa wameviweka wakfu.

19 Hapakuwepo vita tena mpaka mwaka wa thelathini na tano wa utawala wake Asa.