Ufalme wa Israeli

Vifo vya Yeroboamu na Mwanawe

955 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Wafalme 14:1–20

1 Wakati ule Abiya mwana wa Yeroboamu akaugua, 2 naye Yeroboamu akamwambia mke wake, “Nenda ukajibadilishe, ili watu wasijue kwamba wewe ni mke wa Yeroboamu. Kisha uende Shilo. Nabii Ahiya yuko huko, yule aliyeniambia kuwa nitakuwa mfalme juu ya watu hawa. 3 Chukua mikate kumi, maandazi kadhaa na gudulia la asali na umwendee. Atakuambia kitakachotokea kwa kijana.” 4 Basi mke wa Yeroboamu akafanya kama alivyosema mumewe, akaenda kwenye nyumba ya Ahiya huko Shilo.

Wakati huu Ahiya alikuwa kipofu naye alishindwa kuona kwa sababu ya umri wake. 5 Lakini Bwana alikuwa amemwambia Ahiya, “Mke wa Yeroboamu anakuja kukuuliza kuhusu mwanawe, kwa kuwa ni mgonjwa, nawe utamjibu hivi na hivi. Atakapowasili, atajifanya kuwa ni mtu mwingine.”

6 Hivyo Ahiya aliposikia kishindo cha hatua zake mlangoni, akasema, “Karibu ndani, mke wa Yeroboamu. Kwa nini kujibadilisha? Nimetumwa kwako nikiwa na habari mbaya. 7 Nenda, ukamwambie Yeroboamu kwamba hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Nilikuinua miongoni mwa watu na kukufanya kiongozi juu ya watu wangu Israeli. 8 Nikararua ufalme kutoka kwa nyumba ya Daudi na kukupa wewe, lakini hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, ambaye aliyashika maagizo yangu na kunifuata kwa moyo wake wote, akifanya tu lile lililokuwa sawa machoni pangu. 9 Umefanya maovu mengi kuliko wote waliokutangulia. Umejitengenezea miungu mingine, sanamu za chuma, umenighadhibisha na kunitupa nyuma yako.

10 “ ‘Kwa sababu ya hili, nitaleta maafa juu ya nyumba ya Yeroboamu. Nitakatilia mbali kutoka kwa Yeroboamu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, mtumwa au mtu huru. Nitachoma nyumba ya Yeroboamu mpaka iteketee yote kama mtu achomaye kinyesi. 11 Mbwa watawala wale walio wa nyumba ya Yeroboamu watakaofia ndani ya mji na ndege wa angani watajilisha kwa wale watakaofia mashambani. Bwana amesema!’

12 “Kukuhusu wewe, rudi nyumbani. Wakati utakapotia mguu katika mji wako, kijana atakufa. 13 Israeli yote itamwombolezea na kumzika. Kwa sababu ni yeye pekee wa nyumba ya Yeroboamu atakayezikwa, kwa sababu ni yeye peke yake ndani ya nyumba ya Yeroboamu ambaye Bwana, Mungu wa Israeli, ameona kitu chema kwake.

14 “Bwana atajiinulia mwenyewe mfalme juu ya Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu. Siku ndiyo hii! Nini? Naam, hata sasa hivi. 15 Naye Bwana ataipiga Israeli, hata iwe kama unyasi unaosukwasukwa juu ya maji. Ataingʼoa Israeli kutoka nchi hii nzuri aliyowapa baba zao na kuwatawanya ngʼambo ya Mto Frati, kwa sababu wamemghadhibisha Bwana kwa kutengeneza nguzo za Ashera 16 Naye atawaacha Israeli kwa ajili ya makosa ya Yeroboamu aliyoyatenda na kusababisha Israeli kuyatenda.”

17 Kisha mke wa Yeroboamu akainuka, akaondoka kwenda Tirsa. Mara alipokanyaga kizingiti cha mlango, kijana akafa. 18 Wakamzika na Israeli yote ikamwombolezea, kama Bwana alivyokuwa amesema kupitia mtumishi wake, nabii Ahiya.

19 Matukio mengine ya utawala wa Yeroboamu, vita vyake na jinsi alivyotawala, vimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli. 20 Yeroboamu akawatawala kwa miaka ishirini na miwili, kisha akalala na baba zake. Naye Nadabu mwanawe akawa mfalme baada yake.

Utawala wa Nadabu 953 KK

1 Wafalme 15:25–31

25 Nadabu mwana wa Yeroboamu akawa mfalme wa Israeli katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Asa wa Yuda, naye akatawala Israeli kwa miaka miwili. 26 Akafanya maovu machoni pa Bwana, akienenda katika njia za baba yake na katika dhambi yake, ambayo alisababisha Israeli kuifanya.

27 Baasha mwana wa Ahiya wa nyumba ya Isakari akafanya shauri baya dhidi yake, naye akamuua huko Gibethoni, mji wa Wafilisti, wakati Nadabu na Israeli yote walipokuwa wameuzingira. 28 Baasha akamuua Nadabu katika mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, naye Baasha akaingia mahali pake kuwa mfalme.

29 Mara tu alipoanza kutawala, aliua jamaa yote ya Yeroboamu. Hakumwachia Yeroboamu yeyote aliyekuwa hai, bali aliwaangamiza wote, kulingana na neno la Bwana lililotolewa kupitia kwa mtumishi wake Ahiya Mshiloni, 30 kwa sababu ya dhambi alizokuwa amezitenda Yeroboamu na kusababisha Israeli kuzitenda, tena kwa sababu alimkasirisha Bwana, Mungu wa Israeli.

31 Kwa matukio mengine ya utawala wa Nadabu na yote aliyofanya, je hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?

Utawala wa Baasha 930 KK

1 Wafalme 15:32–16:7

32 Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli wakati wote wa utawala wao.

33 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Baasha mwana wa Ahiya akawa mfalme wa Israeli yote huko Tirsa, naye akatawala kwa miaka ishirini na minne. 34 Akatenda maovu machoni pa Bwana, akienenda katika njia za Yeroboamu na dhambi yake, ambayo alikuwa amesababisha Israeli kuitenda.

16:1 Ndipo neno la Bwana likamjia Yehu mwana wa Hanani dhidi ya Baasha, kusema: 2 “Nilikuinua kutoka mavumbini na kukufanya kiongozi wa watu wangu Israeli, lakini ukaenenda katika njia za Yeroboamu na kusababisha watu wangu Israeli kutenda dhambi na kunikasirisha kwa dhambi zao. 3 Basi nitamwangamiza Baasha pamoja na nyumba yake, nami nitaifanya nyumba yako kama ile ya Yeroboamu mwanawe Nebati. 4 Mbwa watawala watu wa Baasha watakaofia mjini na ndege wa angani watajilisha kwa wale watakaofia mashambani.”

5 Kwa matukio mengine ya utawala wa Baasha, aliyoyafanya na mafanikio yake, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 6 Baasha akalala na baba zake naye akazikwa huko Tirsa. Naye Ela mwanawe akawa mfalme baada yake.

7 Zaidi ya hayo, neno la Bwana likamjia Baasha pamoja na nyumba yake kupitia kwa nabii Yehu mwana wa Hanani, kwa sababu ya maovu yote aliyokuwa ametenda machoni pa Bwana, akamkasirisha kwa mambo aliyotenda, na kuwa kama nyumba ya Yeroboamu, na pia kwa sababu aliiangamiza.