Ahazi Anaungana na Tiglath-Pileseri
Ahazi anafanya muungano na Tiglath-Pileseri, mfalme wa Ashuru.
740 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
6 Wakati ule, Resini mfalme wa Aramu akaurudisha Elathi kwa Aramu kwa kuwafukuza watu wa Yuda. Kisha Waedomu wakahamia Elathi, nao wanaishi huko mpaka leo.
7 Ahazi akatuma wajumbe kumwambia Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru kwamba, “Mimi ni mtumishi na mtumwa wako. Njoo na uniokoe kutoka mkononi mwa mfalme wa Aramu na wa mfalme wa Israeli, ambao wananishambulia.” 8 Naye Ahazi akachukua fedha na dhahabu zilizopatikana ndani ya Hekalu la Bwana na katika hazina ya jumba la mfalme, na kuzituma kama zawadi kwa mfalme wa Ashuru. 9 Mfalme wa Ashuru akamwitikia kwa kushambulia Dameski na kuiteka. Akawahamishia wenyeji wake huko Kiri, na kumuua Resini.
1 Ole kwa lile taji la maua, kiburi cha walevi wa Efraimu,
kwa ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake,
uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba:
kwa ule mji, kiburi cha wale walioshushwa na mvinyo!
2 Tazama, Bwana anaye mmoja aliye na uwezo na nguvu.
Kama dhoruba ya mvua ya mawe na upepo uharibuo,
kama mvua inyeshayo kwa nguvu na mafuriko yashukayo,
atakiangusha chini kwa nguvu.
3 Lile taji la maua, kiburi cha walevi cha Efraimu,
kitakanyagwa chini ya nyayo.
4 Lile ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake,
uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba,
litakuwa kama tini iliyoiva kabla ya mavuno:
mara mtu aionapo, huichuma na kuila.
5 Katika siku ile, Bwana Mwenye Nguvu Zote
atakuwa taji la utukufu,
taji zuri la maua
kwa mabaki ya watu wake.
6 Atakuwa roho ya haki
kwa yeye aketiye katika kiti cha hukumu,
chanzo cha nguvu
kwa wale wazuiao vita langoni.
7 Hawa pia wanapepesuka kwa sababu ya mvinyo,
wanayumbayumba kwa sababu ya kileo:
Makuhani na manabii wanapepesuka kwa sababu ya kileo,
wanachanganyikiwa kwa sababu ya mvinyo;
wanapepesuka wanapoona maono,
wanajikwaa wanapotoa maamuzi.
8 Meza zote zimejawa na matapishi
wala hakuna sehemu hata ndogo
isiyokuwa na uchafu.
9 “Yeye anajaribu kumfundisha nani?
Yeye anamwelezea nani ujumbe wake?
Je, ni kwa watoto walioachishwa kunyonya?
Je, ni wale ambao ndipo tu wametolewa matitini?
10 Kwa maana ni:
Amri juu ya amri, amri juu ya amri,
kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni;
hapa kidogo, kule kidogo.”
11 Sawa kabisa, kwa midomo migeni
na kwa lugha ngeni,
Mungu atasema na watu hawa,
12 wale ambao aliwaambia,
“Hapa ni mahali pa kupumzika,
waliochoka na wapumzike,”
na, “Hapa ni mahali pa mapumziko,”
lakini hawakutaka kusikiliza.
13 Hivyo basi, neno la Bwana kwao litakuwa:
Amri juu ya amri, amri juu ya amri,
kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni,
hapa kidogo, kule kidogo:
ili waende na kuanguka chali,
wakijeruhiwa, wakinaswa na kukamatwa.
14 Kwa hiyo sikieni neno la Bwana, enyi watu wenye dharau
mnaotawala watu hawa wa Yerusalemu.
15 Ninyi mnajisifu, “Tumefanya agano na mauti,
tumefanya mapatano na kuzimu.
Wakati pigo lifurikalo litakapopita,
haliwezi kutugusa sisi,
kwa kuwa tumefanya uongo kuwa kimbilio letu
na miungu ya uongo kuwa mahali petu pa kujificha.”
16 Kwa hiyo hivi ndivyo Bwana Mwenyezi asemavyo:
“Tazama, ninaweka jiwe katika Sayuni,
jiwe lililojaribiwa,
jiwe la pembeni la thamani kwa ajili ya msingi thabiti.
Yeye atumainiye kamwe hatatiwa hofu.
17 Nitaifanya haki kuwa kamba ya kupimia
na uadilifu kuwa timazi;
mvua ya mawe itafagia kimbilio lenu, huo uongo,
nayo maji yatafurikia mahali penu pa kujificha.
18 Agano lenu na kifo litabatilishwa,
patano lenu na kuzimu halitasimama.
Wakati pigo lifurikalo litakapowakumba,
litawaangusha chini.
19 Kila mara lijapo litawachukua,
asubuhi baada ya asubuhi,
wakati wa mchana na wakati wa usiku,
litawakumba tangu mwanzo hadi mwisho.”
Kuuelewa ujumbe huu
utaleta hofu tupu.
20 Kitanda ni kifupi mno kujinyoosha juu yake,
nguo ya kujifunikia ni nyembamba mno
mtu hawezi kujifunikia.
21 Bwana atainuka kama alivyofanya kwenye Mlima Perasimu,
ataghadhibika kama alivyofanya katika Bonde la Gibeoni:
ili kufanya kazi yake, kazi yake ya ajabu,
ili kutimiza kazi yake, kazi yake ngeni.
22 Sasa acheni dharau zenu,
la sivyo minyororo yenu itakuwa mizito zaidi.
Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, ameniambia
habari za maangamizi yaliyoamriwa dhidi ya nchi yote.
23 Sikilizeni msikie sauti yangu,
tegeni masikio na msikie niyasemayo.
24 Wakati mkulima alimapo ili apande,
je, hulima siku zote?
Je, huendelea kubomoa ardhi
na kusawazisha udongo?
25 Akiisha kusawazisha shamba,
je, hatapanyi mbegu za bizari na kutawanya jira?
Je, hapandi ngano katika sehemu yake,
shayiri katika eneo lake,
na nafaka nyingine katika shamba lake?
26 Mungu wake humwelekeza
na kumfundisha njia iliyo sahihi.
27 Iliki haipurwi kwa nyundo,
wala gurudumu la gari halivingirishwi juu ya jira;
iliki hupurwa kwa fimbo,
na jira kwa ufito.
28 Nafaka lazima isagwe ili kutengeneza mkate,
kwa hiyo mtu haendelei kuipura daima.
Ingawa huendesha magurudumu ya gari lake la kupuria juu yake,
farasi wake hawasagi.
29 Haya yote pia hutoka kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote,
mwenye mashauri ya ajabu, na anayepita wote kwa hekima.
20 Hivyo Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru akaja kumtesa badala ya kumsaidia. 21 Ahazi akachukua baadhi ya vitu kutoka Hekalu la Bwana, jumba la kifalme na kutoka kwa wakuu wake na kumpa mfalme wa Ashuru kama ushuru, lakini hilo halikumsaidia.
22 Katika wakati wake wa mateso Mfalme Ahazi akazidi kukosa uaminifu kwa Bwana. 23 Akatoa kafara kwa miungu ya Dameski, waliokuwa wamemshinda, kwa kuwa aliwaza, “Kwa kuwa miungu ya mfalme wa Aramu imewasaidia wao, nitaitolea dhabihu ili inisaidie na mimi.” Lakini haya ndiyo yaliyokuwa maangamizi yake na Israeli wote.
10 Kisha Mfalme Ahazi akaenda Dameski kukutana na Tiglath-Pileseri wa Ashuru. Akaona madhabahu huko Dameski, naye akamtumia Uria kuhani mchoro wa hayo madhabahu, pamoja na maelezo ya mpango kamili wa ujenzi wake. 11 Kwa hiyo Uria kuhani akajenga madhabahu kulingana na mipango yote ambayo Mfalme Ahazi alikuwa ameituma kutoka Dameski, na akamaliza ujenzi kabla ya Mfalme Ahazi kurudi. 12 Mfalme aliporudi kutoka Dameski na kuona hayo madhabahu, akayasogelea na kutoa sadaka juu yake. 13 Akatoa sadaka yake ya kuteketezwa na sadaka ya nafaka, akamimina sadaka ya kinywaji na kunyunyizia damu ya sadaka zake za amani juu ya hayo madhabahu. 14 Mfalme Ahazi akayaondoa madhabahu ya zamani ya shaba kutoka hapo mbele ya Hekalu la Bwana, yaliyokuwa yamesimama kati ya ingilio la Hekalu na hayo madhabahu mapya, naye akayaweka upande wa kaskazini mwa hayo madhabahu mapya.
15 Ndipo Mfalme Ahazi akatoa amri zifuatazo kwa Uria kuhani: “Juu ya hayo madhabahu kubwa mapya, toa sadaka ya asubuhi ya kuteketezwa na sadaka ya jioni ya nafaka, sadaka ya mfalme ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya nafaka, sadaka ya kuteketezwa ya watu wote wa nchi, pamoja na sadaka yao ya nafaka na sadaka yao ya kinywaji. Unyunyize juu ya hayo madhabahu damu yote ya sadaka za kuteketezwa na dhabihu. Lakini mimi nitatumia hayo madhabahu ya zamani ya shaba kwa ajili ya kutafuta uongozi.” 16 Naye Uria kuhani akafanya kama Mfalme Ahazi alivyoagiza.
17 Mfalme Ahazi akaondoa mbao za pembeni na kuondoa masinia kwenye vile vishikilio vilivyohamishika. Akaondoa ile Bahari kutoka kwenye mafahali wa shaba walioishikilia, na kuiweka kwenye kitako cha jiwe. 18 Kwa heshima ya mfalme wa Ashuru, akaliondoa pia pazia la Sabato lililokuwa limewekwa ndani ya Hekalu, na akaondoa ile njia ya kifalme ya kuingia kwenye Hekalu la Bwana.
24 Ahazi akakusanya pamoja vyombo vya nyumba ya Mungu na kuvivunja vipande vipande. Akafunga milango ya Hekalu la Bwana na kusimamisha madhabahu katika kila njia panda ya barabara za Yerusalemu. 25 Katika kila mji wa Yuda akajenga mahali pa juu pa kuabudia miungu ili kutolea miungu mingine kafara za kuteketezwa na kuchochea hasira ya Bwana, Mungu wa baba zake.
1 “Sikieni hili, enyi makuhani!
Kuweni wasikivu, enyi Waisraeli!
Sikieni, ee nyumba ya mfalme!
Hukumu hii ni dhidi yenu:
Mmekuwa mtego huko Mispa,
wavu uliotandwa juu ya Tabori.
2 Waasi wamezidisha sana mauaji.
Mimi nitawatiisha wote.
3 Ninajua yote kuhusu Efraimu,
Israeli hukufichika kwangu.
Efraimu, sasa umegeukia ukahaba,
Israeli amenajisika.
4 “Matendo yao hayawaachii
kurudi kwa Mungu wao.
Roho ya ukahaba imo ndani ya mioyo yao,
hawamkubali Bwana.
5 Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yao;
Waisraeli, hata Efraimu,
wanajikwaa katika dhambi zao;
pia Yuda atajikwaa pamoja nao.
6 Wakati wanapokwenda na makundi yao
ya kondoo na ngʼombe
kumtafuta Bwana,
hawatampata;
yeye amejiondoa kutoka kwao.
7 Wao si waaminifu kwa Bwana;
wamezaa watoto haramu.
Sasa sikukuu zao za Mwandamo wa Mwezi
zitawaangamiza wao
pamoja na mashamba yao.
8 “Pigeni tarumbeta huko Gibea,
baragumu huko Rama.
Paza kilio cha vita huko Beth-Aveni,
ongoza, ee Benyamini.
9 Efraimu ataachwa ukiwa
katika siku ya kuadhibiwa.
Miongoni mwa makabila ya Israeli
ninatangaza lile ambalo halina budi kutukia.
10 Viongozi wa Yuda ni kama wale
wanaosogeza mawe ya mpaka.
Nitamwaga ghadhabu yangu juu yao
kama mafuriko ya maji.
11 Efraimu ameonewa,
amekanyagwa katika hukumu
kwa kuwa amekusudia kufuatia sanamu.
12 Mimi ni kama nondo kwa Efraimu,
na kama uozo kwa watu wa Yuda.
13 “Wakati Efraimu alipoona ugonjwa wake,
naye Yuda vidonda vyake,
ndipo Efraimu alipogeukia Ashuru,
na kuomba msaada kwa mfalme mkuu.
Lakini hawezi kukuponya,
wala hawezi kukuponya vidonda vyako.
14 Kwa maana nitakuwa kama simba kwa Efraimu,
kama simba mkubwa kwa Yuda.
Nitawararua vipande vipande na kuondoka;
nitawachukua mbali,
na hakuna wa kuwaokoa.
15 Kisha nitarudi mahali pangu
mpaka watakapokubali kosa lao.
Nao watautafuta uso wangu;
katika taabu yao watanitafuta kwa bidii.”