Peka Anaiharibu Yuda
741 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
4 Akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia miungu, juu ya vilima, na chini ya kila mti uliotanda.
5 Kwa hiyo Bwana Mungu wake akamtia mikononi mwa mfalme wa Aramu. Waaramu wakamshinda, wakachukua watu wake wengi mateka na kuwaleta mpaka Dameski.
Tena alitiwa mikononi mwa mfalme wa Israeli, ambaye aliwaua watu wake wengi. 6 Kwa siku moja Peka mwana wa Remalia aliwaua askari 120,000 katika Yuda, kwa kuwa Yuda walikuwa wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao. 7 Zikri, askari shujaa Mwefraimu, akamuua Maaseya mwana wa mfalme, Azrikamu mkuu wa jumba la kifalme na Elikana aliyekuwa wa pili kwa mfalme. 8 Waisraeli wakawachukua mateka kutoka ndugu zao, watu wapatao 200,000 hawa wakiwa ni wanawake, watoto wa kiume na wa kike. Wakachukua pia kiasi kikubwa cha nyara, ambazo walirudi nazo Samaria.
9 Lakini kulikuwako huko nabii wa Bwana aliyeitwa Odedi, akaondoka ili kukutana na jeshi liliporejea Samaria. Akawaambia, “Kwa kuwa Bwana, Mungu wa baba zenu, aliwakasirikia Yuda, aliwatia mikononi mwenu. Lakini mmewachinja kwa hasira ambayo imefika hadi mbinguni. 10 Nanyi sasa mnakusudia kuwafanya wanaume na wanawake wa Yuda na Yerusalemu watumwa wenu. Lakini ninyi je, hamna pia hatia ya dhambi mliyotenda dhidi ya Bwana Mungu wenu? 11 Basi nisikilizeni! Mkawarudishe mateka mliowachukua kutoka kwa ndugu zenu, kwa kuwa hasira kali ya Bwana iko juu yenu.”
12 Ndipo baadhi ya viongozi katika Efraimu, yaani, Azaria mwana wa Yehohanani, Berekia mwana wa Meshilemothi, Yehizkia mwana wa Shalumu na Amasa mwana wa Hadlai, wakakubaliana na huyo nabii, hivyo wakawapinga wale waliokuwa wanawasili kutoka vitani. 13 Wakamwambia, “Hamna ruhusa kuwaleta hao wafungwa hapa, ama sivyo tutakuwa na hatia mbele za Bwana. Je, mnataka kuongezea dhambi yetu na hatia yetu? Kwa sababu hatia yetu tayari ni kubwa, nayo hasira kali ya Bwana iko juu ya Israeli.”
14 Hivyo wale askari wakawaacha wale mateka pamoja na nyara mbele ya hao maafisa na kusanyiko lote. 15 Kisha watu waliotajwa kwa majina wakawachukua wale mateka na kutoka zile nyara, wakachukua mavazi wakawavika wale wafungwa wote waliokuwa uchi. Wakawapatia nguo na viatu, chakula na cha kunywa, wakawapa matibabu, wote waliokuwa dhaifu miongoni mwao wakawapandisha juu ya punda, wakawaleta ndugu zao mpaka Yeriko, ndio Mji wa Mitende, kisha wakarudi Samaria.
16 Wakati ule, Mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru kuomba msaada. 17 Waedomu walikuwa wamekuja tena na kuwashambulia Yuda na kuchukua mateka. 18 Pia Wafilisti walikuwa wameshambulia miji iliyokuwa chini ya vilima na katika miji ya Negebu ya Yuda. Nao wakawa wametwaa Beth-Shemeshi, Aiyaloni, Gederothi, Soko pamoja na vijiji vyake, Timna pamoja na vijiji vyake, Gimzo pia pamoja na vijiji vyake na kuishi humo. 19 Bwana aliishusha Yuda kwa sababu ya Ahazi mfalme wa Israeli, kwa kuwa alikuwa ameongeza uovu katika Yuda na kumkosea Bwana mno.
1 Maono ya Obadia.
Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi kuhusu Edomu:
Tumesikia ujumbe kutoka kwa Bwana:
Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema,
“Inukeni, twendeni tukapigane vita dhidi yake.”
2 “Angalieni, nitawafanya wadogo miongoni mwa mataifa,
mtadharauliwa kabisa.
3 Kiburi cha moyo wako kimekudanganya,
wewe unayeishi katika majabali ya miamba
na kufanya makao yako juu,
wewe unayejiambia mwenyewe,
‘Ni nani awezaye kunishusha chini?’
4 Ingawa unapaa juu kama tai
na kufanya kiota chako kati ya nyota,
nitakushusha chini kutoka huko,”
asema Bwana.
5 “Ikiwa wevi wangekuja kwako,
ikiwa wanyangʼanyi wangekujia usiku:
Lo! Tazama ni maafa kiasi gani yangekuwa yanakungojea:
je, si wangeiba tu kiasi ambacho wangehitaji?
Kama wachuma zabibu wangekuja kwako,
je, wasingebakiza zabibu chache?
6 Lakini tazama jinsi Esau atakavyotekwa,
jinsi hazina zake zilizofichwa zitatekwa nyara!
7 Wote ulioungana nao watakufukuza hadi mpakani,
rafiki zako watakudanganya na kukushinda,
wale wanaokula mkate wako watakutegea mtego,
lakini hutaweza kuugundua.
8 “Katika siku hiyo,” asema Bwana,
“je, sitaangamiza watu wenye hekima wa Edomu,
watu wenye ufahamu katika milima ya Esau?
9 Ee Temani, mashujaa wako watatiwa hofu,
kila mmoja katika milima ya Esau
ataangushwa chini kwa kuchinjwa.
10 Kwa sababu ya jeuri uliyofanya dhidi ya ndugu yako Yakobo,
aibu itakufunika;
utaangamizwa milele.
11 Siku ile ulisimama mbali ukiangalia
wakati wageni walipojichukulia utajiri wake
na watu wa nchi nyingine walipoingia malango yake
wakipiga kura kwa ajili ya Yerusalemu,
ulikuwa kama mmoja wao.
12 Usingemdharau ndugu yako
katika siku ya msiba wake,
wala kufurahia juu ya watu wa Yuda
katika siku ya maangamizi yao,
wala kujigamba sana
katika siku ya taabu yao.
13 Usingeingia katika malango ya watu wangu
katika siku ya maafa yao,
wala kuwadharau katika janga lao
katika siku ya maafa yao,
wala kunyangʼanya mali zao
katika siku ya maafa yao.
14 Usingengoja kwenye njia panda
na kuwaua wakimbizi wao,
wala kuwatoa watu wake waliosalia
katika siku ya shida yao.
15 “Siku ya Bwana iko karibu
kwa mataifa yote.
Kama ulivyofanya, nawe utafanyiwa vivyo hivyo,
matendo yako yatakurudia juu ya kichwa chako.
16 Kama vile ulivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu,
vivyo hivyo mataifa yote watakunywa mfululizo,
watakunywa na kunywa,
nao watatoweka kana kwamba hawajawahi kuwepo.
17 Lakini katika Mlima Sayuni kutakuwepo
na wale watakaookoka;
nao utakuwa mtakatifu,
nayo nyumba ya Yakobo
itamiliki urithi wake.
18 Nyumba ya Yakobo itakuwa moto,
na nyumba ya Yosefu itakuwa mwali wa moto;
nayo nyumba ya Esau itakuwa bua kavu,
nao wataiwasha moto na kuiteketeza.
Hakutakuwa na watakaosalimika
kutoka nyumba ya Esau.”
Bwana amesema.
19 Watu kutoka nchi ya Negebu
wataikalia milima ya Esau,
na watu kutoka miteremko ya vilima
watamiliki nchi ya Wafilisti.
Watayakalia mashamba ya Efraimu na Samaria,
naye Benyamini atamiliki Gileadi.
20 Kundi la Waisraeli walioko uhamishoni Kanaani
watarudi na kumiliki nchi mpaka Sarepta.
Walioko uhamishoni Sefaradi kutoka Yerusalemu
watamiliki miji ya Negebu.
21 Waokoaji watakwea juu ya Mlima Sayuni
kutawala milima ya Esau.
Nao ufalme utakuwa wa Bwana.
2 Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia!
Kwa maana Bwana amesema:
“Nimewalisha watoto na kuwalea,
lakini wameniasi mimi.
3 Ngʼombe anamjua bwana wake,
naye punda anajua hori la mmiliki wake,
lakini Israeli hajui,
watu wangu hawaelewi.”
4 Lo! Taifa lenye dhambi,
watu waliolemewa na uovu,
uzao wa watenda mabaya,
watoto waliozoelea upotovu!
Wamemwacha Bwana,
Wamemkataa kwa dharau
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli
na kumgeuzia kisogo.
5 Kwa nini mzidi kupigwa?
Kwa nini kudumu katika uasi?
Kichwa chako chote kimejeruhiwa,
moyo wako wote ni mgonjwa.
6 Kutoka wayo wako wa mguu hadi kwenye utosi wa kichwa chako
hakuna uzima:
ni majeraha matupu na makovu
na vidonda vitokavyo damu,
havikusafishwa au kufungwa
wala kulainishwa kwa mafuta.
7 Nchi yenu imekuwa ukiwa,
miji yenu imeteketezwa kwa moto;
nchi yenu imeachwa tupu na wageni
mbele ya macho yenu,
imeharibiwa kama vile imepinduliwa na wageni.
8 Binti Sayuni ameachwa kama kipenu
katika shamba la mizabibu,
kama kibanda katika shamba la matikitimaji,
kama mji uliohusuriwa.
9 Kama Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote
asingelituachia walionusurika,
tungelikuwa kama Sodoma,
tungelifanana na Gomora.
10 Sikieni neno la Bwana,
ninyi watawala wa Sodoma;
sikilizeni sheria ya Mungu wetu,
enyi watu wa Gomora!
11 Bwana anasema, “Wingi wa sadaka zenu,
ni kitu gani kwangu?
Ninazo sadaka za kuteketezwa nyingi kupita kiasi,
za kondoo dume na mafuta ya wanyama walionona.
Sipendezwi na damu za mafahali
wala za wana-kondoo na mbuzi.
12 Mnapokuja kujihudhurisha mbele zangu,
ni nani aliyewataka ninyi mfanye hivyo,
huku kuzikanyaga nyua zangu?
13 Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana!
Uvumba wenu ni chukizo kwangu.
Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada:
siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu.
14 Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi, na sikukuu zenu zilizoamriwa:
moyo wangu unazichukia.
Zimekuwa mzigo kwangu,
nimechoka kuzivumilia.
15 Mnaponyoosha mikono yenu katika maombi,
nitaficha macho yangu nisiwaone;
hata mkiomba maombi mengi
sitasikiliza.
Mikono yenu imejaa damu;
16 jiosheni na mkajitakase.
Yaondoeni matendo yenu maovu
mbele zangu!
Acheni kutenda mabaya,
17 jifunzeni kutenda mema!
Tafuteni haki,
watieni moyo walioonewa.
Teteeni shauri la yatima,
wateteeni wajane.
18 “Njooni basi tuhojiane,”
asema Bwana.
“Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu,
zitakuwa nyeupe kama theluji;
ingawa ni nyekundu sana kama damu,
zitakuwa nyeupe kama sufu.
19 Kama mkikubali na kutii,
mtakula mema ya nchi,
20 lakini kama mkikataa na kuasi,
mtaangamizwa kwa upanga.”
Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena.
21 Tazama jinsi mji uliokuwa mwaminifu
umekuwa kahaba!
Mwanzoni ulikuwa umejaa unyofu,
haki ilikuwa inakaa ndani yake,
lakini sasa ni wauaji!
22 Fedha yenu imekuwa takataka,
divai yenu nzuri imechanganywa na maji.
23 Watawala wenu ni waasi,
rafiki wa wevi,
wote wanapenda rushwa
na kukimbilia hongo.
Hawatetei yatima,
shauri la mjane haliletwi mbele yao lisikilizwe.
24 Kwa hiyo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote,
Mwenye Nguvu wa Israeli, asema hivi:
“Lo, nitapata faraja kutoka kwa adui zangu
na kujilipizia kisasi juu ya watesi wangu.
25 Nitauelekeza mkono wangu dhidi yenu,
nitawasafisha takataka zenu zote
na kuwaondolea unajisi wenu wote.
26 Nitawarudishia waamuzi wenu kama ilivyokuwa siku za zamani,
nao washauri wenu kama ilivyokuwa mwanzoni.
Baadaye utaitwa,
Mji wa Haki,
Mji Mwaminifu.”
27 Sayuni itakombolewa kwa haki,
wale waliomo ndani yake waliotubu kwa uaminifu.
28 Lakini waasi na wenye dhambi wote wataangamizwa,
nao wanaomwacha Bwana wataangamia.
29 “Mtaaibika kwa sababu ya hiyo mialoni
ambayo mlifurahia,
mtafadhaika kwa sababu ya bustani
mlizozichagua.
30 Mtakuwa kama mwaloni wenye majani yanayonyauka,
kama bustani isiyokuwa na maji.
31 Mtu mwenye nguvu atatoweka kama majani makavu yawakayo moto,
na kazi yake kama cheche ya moto;
vyote vitaungua pamoja,
wala hakuna wa kuuzima huo moto.”