Kazi ya Hekalu Yaanza Tena (continued)

520 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Zekaria 2–6

1 Kisha nikatazama juu: pale mbele yangu alikuwepo mtu mwenye kamba ya kupimia mkononi mwake! 2 Nikamuuliza, “Unakwenda wapi?”

Akanijibu, “Kupima Yerusalemu, kupata urefu na upana wake.”

3 Kisha malaika aliyekuwa akizungumza nami akaondoka, malaika mwingine akaja kukutana naye 4 na kumwambia: “Kimbia, umwambie yule kijana, ‘Yerusalemu utakuwa mji usio na kuta kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo. 5 Mimi mwenyewe nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka,’ asema Bwana, ‘nami nitakuwa utukufu wake ndani yake.’

6 “Njooni! Njooni! Kimbieni mtoke katika nchi ya kaskazini,” asema Bwana, “Kwa kuwa nimewatawanya kwenye pande nne za mbingu,” asema Bwana.

7 “Njoo, ee Sayuni! Kimbia, wewe ukaaye ndani ya Binti Babeli!” 8 Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Baada ya yeye kuniheshimu na kunituma mimi dhidi ya mataifa yaliyokuteka nyara, kwa kuwa yeyote awagusaye ninyi, anaigusa mboni ya jicho lake, 9 hakika nitauinua mkono wangu dhidi yao ili watumwa wao wawateke nyara. Ndipo mtakapojua ya kwamba Bwana Mwenye Nguvu Zote amenituma.

10 “Piga kelele na ufurahie, ee Binti Sayuni, kwa maana ninakuja, nami nitaishi miongoni mwenu,” asema Bwana. 11 “Mataifa mengi yataunganishwa na Bwana siku hiyo, nao watakuwa watu wangu. Nitaishi miongoni mwenu nanyi mtajua kwamba Bwana Mwenye Nguvu Zote amenituma kwenu. 12 Bwana atairithi Yuda kama fungu lake katika nchi takatifu na atachagua tena Yerusalemu. 13 Tulieni mbele za Bwana, enyi watu wote, kwa sababu ameinuka kutoka makao yake matakatifu.”

3:1 Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, akiwa amesimama mbele ya malaika wa Bwana, naye Shetani amesimama upande wake wa kuume ili amshtaki. 2 Bwana akamwambia Shetani, “Bwana akukemee Shetani! Bwana, ambaye ameichagua Yerusalemu, akukemee! Je, mtu huyu siyo kijinga kinachowaka kilichonyakuliwa kwenye moto?”

3 Wakati huu, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu alipokuwa amesimama mbele ya malaika. 4 Malaika akawaambia wale waliokuwa wamesimama mbele yake, “Mvueni hizo nguo zake chafu.”

Kisha akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeiondoa dhambi yako, nami nitakuvika mavazi ya kitajiri.”

5 Kisha nikasema, “Mvike kilemba kilicho safi kichwani mwake.” Kwa hiyo wakamvika kilemba safi kichwani na kumvika yale mavazi mengine, wakati malaika wa Bwana akiwa amesimama karibu.

6 Malaika wa Bwana akamwamuru Yoshua: 7 “Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Ikiwa utakwenda katika njia zangu na kushika masharti yangu, basi utaitawala nyumba yangu na kuwa na amri juu ya nyua zangu, nami nitakupa nafasi miongoni mwa hawa wasimamao hapa.

8 “ ‘Sikiliza, ee Yoshua kuhani mkuu, pamoja na wenzako walioketi mbele yako, ambao ni watu walio ishara ya mambo yatakayokuja: Ninakwenda kumleta mtumishi wangu, Tawi. 9 Tazama, jiwe nililoliweka mbele ya Yoshua! Kuna macho saba juu ya jiwe lile moja, nami nitachora maandishi juu yake,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, ‘nami nitaiondoa dhambi ya nchi hii kwa siku moja.

10 “ ‘Katika siku hiyo kila mmoja wenu atamwalika jirani yake akae chini ya mzabibu wake na mtini wake,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.”

4:1 Kisha malaika aliyezungumza nami akarudi na kuniamsha, kama mtu aamshwavyo kutoka usingizi wake. 2 Akaniuliza, “Unaona nini?”

Nikajibu, “Ninaona kinara cha taa cha dhahabu tupu, nacho kina bakuli juu yake na taa zake saba juu yake, tena iko mirija saba ya kuleta mafuta, kwenye taa zote zilizo juu yake. 3 Pia kuna mizeituni miwili karibu yake, mmoja upande wa kuume wa bakuli na mwingine upande wa kushoto.”

4 Nikamuuliza malaika aliyezungumza nami, “Hivi ni vitu gani, bwana wangu?”

5 Akanijibu, “Hujui kuwa hivi ni vitu gani?”

Nikajibu, “Hapana, bwana wangu.”

6 Kisha akaniambia, “Hili ni neno la Bwana kwa Zerubabeli: ‘Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa Roho yangu,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

7 “Wewe ni kitu gani, ee mlima mkubwa sana? Mbele ya Zerubabeli wewe utakuwa ardhi tambarare. Kisha ataweka jiwe la juu kabisa la mwisho na watu wakipiga kelele wakisema, ‘Mungu libariki! Mungu libariki!’ ”

8 Kisha neno la Bwana likanijia: 9 “Mikono ya Zerubabeli iliweka msingi wa Hekalu hili, mikono yake pia italimalizia. Kisha mtajua ya kuwa Bwana Mwenye Nguvu Zote amenituma mimi kwenu.

10 “Ni nani anayeidharau siku ya mambo madogo? Watu watashangilia watakapoona timazi mkononi mwa Zerubabeli.

“(Hizi saba ni macho ya Bwana ambayo huzunguka duniani kote.)”

11 Kisha nikamuuliza yule malaika, “Hii mizeituni miwili iliyoko upande wa kuume na wa kushoto wa kinara cha taa ni nini?”

12 Tena nikamuuliza, “Haya matawi mawili ya mizeituni karibu na hiyo mirija miwili ya dhahabu inayomimina mafuta ya dhahabu ni nini?”

13 Akajibu, “Hujui kuwa haya ni nini?”

Nikamjibu, “Hapana, bwana wangu.”

14 Kwa hiyo akasema, “Hawa ni wawili ambao wamepakwa mafuta ili kumtumikia Bwana wa dunia yote.”

5:1 Nikatazama tena: na hapo mbele yangu kulikuwa na kitabu kilichoruka!

2 Akaniuliza, “Unaona nini?”

Nikamjibu, “Naona kitabu kinachoruka chenye, urefu wa dhiraa ishirini na upana wa dhiraa kumi.”

3 Akaniambia, “Hii ni laana inayotoka kwenda juu ya nchi yote, kwa kuwa kufuatana na yale yaliyoandikwa katika upande mmoja, kila mwizi atafukuziwa mbali, pia kufuatana na yaliyo upande wa pili, kila aapaye kwa uongo atafukuziwa mbali. 4 Bwana Mwenye Nguvu Zote asema, ‘Nitaituma hiyo laana, nayo itaingia katika nyumba ya mwizi na nyumba ya huyo aapaye kwa uongo kwa Jina langu. Itabaki katika nyumba yake na kuiharibu, pamoja na mbao zake na mawe yake.’ ”

5 Kisha yule malaika aliyekuwa akizungumza nami akanijia na kuniambia, “Tazama juu uone ni nini kile kinachojitokeza.”

6 Nikamuuliza, “Ni kitu gani?”

Akanijibu, “Ni kikapu cha kupimia.” Kisha akaongeza kusema, “Huu ni uovu wa watu katika nchi nzima.”

7 Kisha kifuniko kilichotengenezwa kwa madini ya risasi kilichokuwa kimefunika kile kikapu, kiliinuliwa na ndani ya kile kikapu alikuwako mwanamke ameketi! 8 Akasema, “Huu ni uovu,” tena akamsukumia ndani ya kikapu na kushindilia kifuniko juu ya mdomo wa kikapu.

9 Kisha nikatazama juu: na pale mbele yangu, walikuwepo wanawake wawili, wakiwa na upepo katika mabawa yao! Walikuwa na mabawa kama ya korongo, nao wakainua kile kikapu na kuruka nacho kati ya mbingu na nchi.

10 Nikamuuliza yule malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Wanakipeleka wapi hicho kikapu?”

11 Akanijibu, “Wanakipeleka katika nchi ya Babeli na kujenga nyumba kwa ajili yake. Itakapokuwa tayari, kikapu kitawekwa pale mahali pake.”

6:1 Nikatazama juu tena: nikaona mbele yangu magari manne ya vita yakija kutoka kati ya milima miwili, milima ya shaba! 2 Gari la kwanza lilivutwa na farasi wekundu, la pili lilivutwa na farasi weusi, 3 la tatu lilivutwa na farasi weupe na gari la nne lilivutwa na farasi wa madoadoa ya kijivu, wote wenye nguvu. 4 Nikamuuliza malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Hawa ni nani bwana wangu?”

5 Malaika akanijibu, “Hizi ni roho nne za mbinguni zisimamazo mbele ya uwepo wa Bwana wa dunia yote, zinatoka kwenda kufanya kazi yake. 6 Gari linalovutwa na farasi weusi linaelekea katika nchi ya kaskazini, la farasi weupe linaelekea magharibi na la farasi wa madoadoa ya kijivu linaelekea kusini.”

7 Wakati hao farasi wenye nguvu walipokuwa wakitoka, walikuwa wakijitahidi kwenda duniani kote. Akasema, “Nenda duniani kote!” Kwa hiyo wakaenda duniani kote.

8 Kisha akaniita, “Tazama, wale wanaokwenda kuelekea nchi ya kaskazini wamepumzisha Roho yangu katika nchi ya kaskazini.”

9 Neno la Bwana likanijia kusema: 10 “Chukua fedha na dhahabu kutoka kwa watu waliohamishwa, yaani Heldai, Tobia na Yedaya ambao wamefika kutoka Babeli. Siku iyo hiyo nenda nyumbani kwa Yosia mwana wa Sefania. 11 Chukua fedha na dhahabu utengeneze taji, nawe uiweke kichwani mwa kuhani mkuu Yoshua, mwana wa Yehosadaki. 12 Umwambie, hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Huyu ndiye mtu ambaye jina lake ni Tawi, naye atachipua kutoka mahali pake na kujenga Hekalu la Bwana. 13 Ni yeye atakayejenga Hekalu la Bwana, naye atavikwa utukufu na ataketi kumiliki katika kiti cha enzi naye atakuwa kuhani katika kiti chake cha enzi. Hapo patakuwa amani kati ya hao wawili.’ 14 Taji itatolewa kwa Heldai, Tobia, Yedaya na Heni mwana wa Sefania kama kumbukumbu ndani ya Hekalu la Bwana. 15 Wale walio mbali sana watakuja na kusaidia kulijenga Hekalu la Bwana, nanyi mtajua ya kwamba Bwana Mwenye Nguvu Zote amenituma kwenu. Hili litatokea ikiwa mtamtii Bwana Mungu wenu kwa bidii.”