Kazi ya Hekalu Yasitishwa na Kuanza Tena
519 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
3 Wakati ule Tatenai mtawala wa ngʼambo ya mto Frati na Shethar-Bozenai na wenzao waliwaendea, wakawauliza, “Ni nani aliyewapa ruhusa ya kujenga tena Hekalu hili na kurudishia upya kama lilivyokuwa?” 4 Pia waliwauliza, “Je, majina ya watu wanaofanya ujenzi huu ni nani?” 5 Lakini jicho la Mungu wao lilikuwa likiwaangalia wazee wa Wayahudi, nao hawakuzuiliwa kujenga mpaka taarifa ikaandikwa kwa Dario na majibu yake kupokelewa.
6 Hii ni nakala ya barua ile Tatenai, mtawala wa ngʼambo ya mto Frati na Shethar-Bozenai na wenzao maafisa wa ngʼambo ya mto Frati waliyompelekea Mfalme Dario. 7 Taarifa waliyompelekea ilisomeka kama ifuatavyo:
Kwa Mfalme Dario:
Salamu kwa moyo mkunjufu.
8 Inampasa Mfalme ajue kwamba tulikwenda katika eneo la Yuda, kwenye Hekalu la Mungu mkuu. Watu wanalijenga kwa mawe makubwa na kuweka mbao kwenye kuta. Kazi inafanyika kwa bidii na inaendelea kwa haraka chini ya uongozi wao.
9 Tuliwauliza viongozi, “Ni nani aliyewapa ruhusa kujenga upya Hekalu hili na kurejeza hali ya jengo kama lilivyokuwa?” 10 Pia tuliwauliza majina yao, ili tukuandikie kukujulisha majina ya viongozi wao.
11 Hili ndilo jibu walilotupa:
“Sisi ni watumishi wa Mungu wa mbingu na nchi, nasi tunalijenga upya Hekalu ambalo lilijengwa miaka mingi iliyopita, lile ambalo mfalme mkuu wa Israeli alilijenga na kulikamilisha. 12 Lakini kwa sababu baba zetu walimkasirisha Mungu wa mbinguni, basi aliwatia mkononi mwa Nebukadneza, Mkaldayo, mfalme wa Babeli, ambaye aliliharibu Hekalu hili na kuwaondoa watu na kuwapeleka uhamishoni huko Babeli.
13 “Pamoja na hayo, katika mwaka wa kwanza wa kutawala Koreshi mfalme wa Babeli, Mfalme Koreshi alitoa amri ya kujengwa upya nyumba hii ya Mungu. 14 Yeye hata aliviondoa vyombo vya dhahabu na fedha vya nyumba ya Mungu, kutoka Hekalu la Babeli ambavyo Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka ndani ya Hekalu huko Yerusalemu na kuvileta katika Hekalu la Babeli.
“Vyombo hivyo Mfalme Koreshi alimkabidhi mtu aliyeitwa Sheshbaza, ambaye Koreshi alikuwa amemteua awe mtawala, 15 naye akamwambia, ‘Chukua vyombo hivi uende ukaviweke ndani ya Hekalu huko Yerusalemu. Nawe uijenge upya nyumba ya Mungu mahali pake.’ 16 Hivyo huyu Sheshbaza alikuja na kuweka misingi ya nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu. Tangu siku hiyo hadi sasa imekuwa ikiendelea kujengwa lakini bado haijamalizika.”
17 Sasa kama ikimpendeza mfalme, uchunguzi na ufanyike katika kumbukumbu za maandishi ya ufalme mjini Babeli, kuona kama kweli Mfalme Koreshi alitoa amri ya kujenga upya nyumba ya Mungu katika Yerusalemu. Kisha tunaomba mfalme na atutumie uamuzi wake kuhusu jambo hili.
6:1 Kisha Mfalme Dario alitoa amri, nao wakafanya uchunguzi katika kumbukumbu zilizohifadhiwa katika hazina huko Babeli. 2 Karatasi moja ndefu ya maandishi ilipatikana huko Ekbatana katika jimbo la Umedi. Haya ndiyo yaliyokuwa yameandikwa humo:
Kumbukumbu:
3 Katika mwaka wa kwanza wa kutawala Mfalme Koreshi, mfalme alitoa amri kuhusu Hekalu la Mungu katika Yerusalemu:
Hekalu na lijengwe tena mahali palepale Wayahudi walipokuwa wakitoa dhabihu, kwenye msingi ule ule. Iwe na kimo cha mikono sitini, upana wa mikono sitini, 4 kuta zijengwe kwa safu tatu za mawe makubwa kisha ifuate safu moja ya mbao. Gharama zitalipwa kutoka hazina ya mfalme. 5 Pia, vyombo vya dhahabu na vya fedha vya nyumba ya Mungu, ambavyo Nebukadneza alivichukua kutoka kwenye Hekalu huko Yerusalemu akavileta Babeli, yapasa virudishwe mahali pake ndani ya Hekalu huko Yerusalemu, yapasa viwekwe ndani ya nyumba ya Mungu.
6 Sasa basi, Tatenai, mtawala wa Ngʼambo ya Mto Frati na Shethar-Bozenai pamoja na ninyi, maafisa wenzao wa jimbo hilo kaeni mbali na mahali hapo. 7 Msiingilie kazi ya Hekalu hili la Mungu. Mwacheni mtawala wa Wayahudi na viongozi Wayahudi wajenge upya nyumba hii ya Mungu mahali pake.
8 Zaidi ya hayo, hapa natoa amri kuhusu mtakalofanya kwa ajili ya wazee wa Wayahudi katika ujenzi wa nyumba hii ya Mungu:
Gharama za watu hawa zitalipwa kikamilifu kutoka hazina ya mfalme, kutoka kwenye mapato ya Ngʼambo ya Mto Frati, ili ujenzi usisimame. 9 Chochote kinachohitajika kama mafahali wachanga, kondoo dume, wana-kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa Mungu wa mbinguni, ngano, chumvi, divai na mafuta kama vitakavyohitajika na makuhani huko Yerusalemu, lazima wapewe kila siku pasipo kukosa, 10 ili waweze kutoa dhabihu inayompendeza Mungu wa mbinguni na kumwombea mfalme na wanawe hali njema.
11 Zaidi ya hayo, ninaamuru kwamba mtu yeyote atakayebadilisha amri hii, boriti itangʼolewa kutoka nyumba yake, ichongwe upande mmoja na atumbuliwe nayo. Kwa ajili ya kosa hili nyumba yake ifanywe lundo la taka. 12 Naye Mungu, aliyeliweka Jina lake huko, amwangushe mfalme yeyote au watu watakaoinua mikono kubadili amri hii au kuharibu Hekalu hili lililoko Yerusalemu.
Mimi Dario nimetoa amri hii. Nayo itekelezwe kwa bidii na kwa makini.
13 Kwa sababu ya amri aliyotoa Mfalme Dario, Tatenai mtawala wa Ngʼambo ya Mto Frati na Shethar-Bozenai na wenzao wakaitekeleza kwa bidii na kwa makini.
Zaburi ya Daudi.
1 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kwa moyo wangu wote,
mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako.
2 Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu,
nami nitalisifu jina lako
kwa ajili ya upendo wako
na uaminifu,
kwa kuwa umelikuza jina lako na neno lako
juu ya vitu vyote.
3 Nilipoita, ulinijibu;
ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari.
4 Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Bwana,
wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako.
5 Wao na waimbe kuhusu njia za Bwana,
kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu.
6 Ingawa Bwana yuko juu,
humwangalia mnyonge,
bali mwenye kiburi
yeye anamjua kutokea mbali.
7 Nijapopita katikati ya shida,
wewe unayahifadhi maisha yangu,
unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu,
kwa mkono wako wa kuume unaniokoa.
8 Bwana atatimiza kusudi lake kwangu,
Ee Bwana, upendo wako wadumu milele:
usiziache kazi za mikono yako.