Mifano Miwili Kuhusu Maombi
Mifano miwili kuhusu maombi: mjane mwenye kusisitiza, na Farisayo na mtoza ushuru.
29 hadi 30 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Luka 18:1–14
18:1 Kisha Yesu akawapa wanafunzi wake mfano ili kuwaonyesha kuwa yawapasa kuomba pasipo kukata tamaa. 2 Akawaambia, “Katika mji mmoja alikuwepo hakimu ambaye hakumwogopa Mungu wala kumjali mtu. 3 Katika mji huo alikuwako mjane mmoja ambaye alikuwa akija kwake mara kwa mara akimwomba, ‘Tafadhali nipatie haki kati yangu na adui yangu.’
4 “Kwa muda mrefu yule hakimu alikataa. Lakini hatimaye akasema moyoni mwake, ‘Ijapokuwa simwogopi Mungu wala simjali mwanadamu, 5 lakini kwa kuwa huyu mjane ananisumbuasumbua, nitahakikisha amepata haki yake ili asiendelee kunichosha kwa kunijia mara kwa mara!’ ”
6 Bwana akasema, “Sikilizeni asemavyo huyu hakimu dhalimu. 7 Je, Mungu hatawatendea haki wateule wake wanaomlilia usiku na mchana? Je, atakawia kuwasaidia? 8 Ninawaambia, atawapatia haki upesi. Lakini je, Mwana wa Adamu atakapokuja ataikuta imani duniani?”
9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine: 10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. 11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. 12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’
13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’
14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”
Yesu Anafundisha Kuhusu Talaka
Akitoka Galilaya na kupitia Perea, Yesu anafundisha kuhusu talaka.
Pereya
Mathayo 19:1–12
19:1 Yesu alipomaliza kusema maneno haya, aliondoka Galilaya, akaenda sehemu za Uyahudi, ngʼambo ya Mto Yordani. 2 Umati mkubwa wa watu ukamfuata, naye akawaponya huko.
3 Baadhi ya Mafarisayo wakamjia ili kumjaribu, wakamuuliza, “Ni halali mtu kumwacha mke wake kwa sababu yoyote?”
4 Akawajibu, “Je, hamkusoma kwamba hapo mwanzo Muumba aliwaumba mwanaume na mwanamke,
5 naye akasema, ‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’?
6 Hivyo si wawili tena, bali mwili mmoja. Kwa hiyo alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”
7 Wakamuuliza, “Kwa nini basi Mose aliagiza mtu kumpa mkewe hati ya talaka na kumwacha?”
8 Yesu akawajibu, “Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo.
9 Mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa sababu ya uasherati naye akaoa mke mwingine, anazini. Naye amwoaye yule mwanamke aliyeachwa pia anazini.”
10 Wanafunzi wake wakamwambia, “Kama hali ndiyo hii kati ya mume na mke, ni afadhali mtu asioe!”
11 Yesu akawaambia, “Si watu wote wanaoweza kupokea neno hili, isipokuwa wale tu waliojaliwa na Mungu. 12 Kwa maana wengine ni matowashi kwa sababu wamezaliwa hivyo; wengine wamefanywa matowashi na wanadamu; na wengine wamejifanya matowashi kwa ajili ya Ufalme wa Mbinguni. Yeye awezaye kulipokea neno hili na alipokee.”
Marko 10:1–12
10:1 Yesu akaondoka huko, akavuka Mto Yordani, akaenda sehemu za Uyahudi. Umati mkubwa wa watu ukaenda kwake tena, naye kama ilivyokuwa desturi yake, akawafundisha.
2 Baadhi ya Mafarisayo wakaja ili kumjaribu kwa kumuuliza, “Je, ni halali mtu kumwacha mke wake?”
3 Yesu akawajibu, “Je, Mose aliwaamuru nini?”
4 Wakajibu, “Mose aliruhusu kwamba mume anaweza kumwandikia mkewe hati ya talaka na kumwacha.”
5 Yesu akawaambia, “Mose aliwaandikia sheria hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu.
6 Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mwanaume na mwanamke.
7 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.’
8 Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena, bali mwili mmoja. 9 Basi, alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”
10 Walipokuwa tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza kuhusu jambo hili.
11 Akawajibu, “Mtu yeyote amwachaye mkewe na kuoa mke mwingine, anazini naye. 12 Naye mwanamke amwachaye mumewe na kuolewa na mume mwingine, anazini.”
Kristo na Watoto
Kristo na watoto, na kushindwa kwa wanafunzi kuelewa mtazamo wa Yesu.
Pereya
Mathayo 19:13–15
19:13 Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Yesu ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wale waliowaleta.
14 Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mbinguni ni wa wale walio kama hawa.”
15 Naye akaweka mikono yake juu yao, na akaondoka huko.
Marko 10:13–16
10:13 Watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wake wakawakemea.
14 Yesu alipoona yaliyokuwa yakitukia, akachukizwa. Akawaambia wanafunzi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa.
15 Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”
16 Akawachukua watoto mikononi mwake, akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.
Luka 18:15–17
18:15 Pia, watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wachanga ili awaguse. Wanafunzi wake walipoona hivyo, wakawakemea.
16 Lakini Yesu akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa.
17 Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”