Matokeo ya Kufufuliwa kwa Lazaro
Athari za kufufuliwa kwa Lazaro kwa watu, kwa baraza, na kwa safari za Yesu.
Yerusalemu na Efraimu huko Uyahudi
29 hadi 30 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Yohana 11:45–54
11:45 Hivyo Wayahudi wengi waliokuwa wamekuja kumfariji Maria, walipoona yale Yesu aliyoyatenda wakamwamini. 46 Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo na kuwaambia mambo Yesu aliyoyafanya. 47 Kwa hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaita mkutano wa baraza.
Wakaulizana, “Tufanyeje? Huyu mtu anafanya ishara nyingi. 48 Kama tukimwacha aendelee hivi, kila mtu atamwamini, nao Warumi watakuja na kupaharibu mahali petu patakatifu na taifa letu.”
49 Mmoja wao aliyeitwa Kayafa, ambaye alikuwa kuhani mkuu mwaka huo, akasema, “Ninyi hamjui kitu chochote! 50 Hamjui kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa lote liangamie?”
51 Hakusema haya kutokana na mawazo yake mwenyewe bali kama kuhani mkuu mwaka huo, alitabiri kuwa Yesu angelikufa kwa ajili ya taifa la Wayahudi, 52 wala si kwa ajili ya taifa hilo pekee, bali pia kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika, ili kuwaleta pamoja na kuwafanya wawe wamoja. 53 Hivyo tangu siku hiyo wakawa wanafanya mipango ili wamuue Yesu.
54 Kwa hiyo Yesu akawa hatembei hadharani miongoni mwa Wayahudi, bali alijitenga akaenda sehemu iliyo karibu na jangwa kwenye kijiji kiitwacho Efraimu. Akakaa huko na wanafunzi wake.
Yesu Anaanza Safari Yake ya Mwisho Kwenda Yerusalemu
Yesu anaanza safari ya mwisho kwenda Yerusalemu, akipitia Samaria na Galilaya.
Huko Samaria au Galilaya
Anawaponya wenye ukoma kumi na kuwaeleza Mafarisayo na wanafunzi jinsi ufalme wa Mungu ulivyo.
Luka 17:11–37
17:11 Yesu alipokuwa njiani akienda Yerusalemu, alipitia mpakani mwa Samaria na Galilaya. 12 Alipokuwa akiingia kwenye kijiji kimoja, watu kumi waliokuwa na ukoma wakakutana naye. Wakasimama mbali, 13 wakapaza sauti, wakasema, “Yesu, Bwana, tuhurumie!”
14 Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.” Nao walipokuwa njiani wakienda, wakatakasika.
15 Mmoja wao alipoona kwamba amepona, akarudi kwa Yesu, akimsifu Mungu kwa sauti kuu. 16 Akajitupa miguuni mwa Yesu akamshukuru. Yeye alikuwa Msamaria.
17 Yesu akauliza, “Je, hawakutakaswa wote kumi? Wako wapi wale wengine tisa? 18 Hakuna hata mmoja aliyeonekana kurudi ili kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?” 19 Yesu akamwambia, “Inuka na uende zako, imani yako imekuponya.”
20 Yesu alipoulizwa na Mafarisayo Ufalme wa Mungu utakuja lini, yeye akawajibu, “Ufalme wa Mungu hauji kwa kuchunguza kwa bidii, 21 wala watu hawatasema, ‘Huu hapa,’ au ‘Ule kule,’ kwa maana Ufalme wa Mungu umo ndani yenu.”
22 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Wakati utafika ambapo mtatamani kuiona moja ya siku ya Mwana wa Adamu, lakini hamtaiona. 23 Watu watawaambia, ‘Yule kule!’ Au, ‘Huyu hapa!’ Msiwakimbilie. 24 Kwa maana kama vile umeme wa radi umulikavyo katika anga kuanzia mwisho mmoja hadi mwingine, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake. 25 Lakini kwanza itampasa kuteseka katika mambo mengi na kukataliwa na kizazi hiki.
26 “Kama ilivyokuwa siku za Noa, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Adamu. 27 Watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia katika safina. Ndipo gharika ikaja na kuwaangamiza wote.
28 “Ndivyo ilivyokuwa katika siku za Loti: Watu walikuwa wakila na kunywa, wakinunua na kuuza, wakilima na kujenga. 29 Lakini siku ile Loti alipoondoka Sodoma, ikanyesha mvua ya moto na kiberiti kutoka mbinguni ukawaangamiza wote.
30 “Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Adamu atakapofunuliwa. 31 Siku hiyo, mtu yeyote aliye juu ya dari ya nyumba yake, hata vitu vyake vikiwa ndani ya hiyo nyumba, asishuke kuvichukua. Vivyo hivyo mtu aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua chochote. 32 Mkumbukeni mke wa Loti! 33 Mtu yeyote anayejaribu kuyaokoa maisha yake atayapoteza, na yeyote atakayeyapoteza maisha yake atayaokoa. 34 Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa wamelala kitanda kimoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. 35 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. [ 36 Wanaume wawili watakuwa wanafanya kazi pamoja shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.]”
37 Kisha wakamuuliza, “Haya yatatukia wapi Bwana?”
Akawaambia, “Pale ulipo mzoga, huko ndiko tai watakapokusanyika.”