Kuta za Yerusalemu Zajengwa Upya (continued)
445 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Habari zilipofika kwa Sanbalati, Tobia, Geshemu Mwarabu, na adui zetu wengine kwamba nimejenga tena ukuta na hakuna nafasi iliyobakia ndani mwake, ingawa mpaka wakati huo sikuwa nimeweka milango kwenye malango, 2 Sanbalati na Geshemu wakanitumia ujumbe huu: “Njoo, tukutane katika mojawapo ya vijiji katika nchi tambarare ya Ono.”
Lakini walikuwa wakikusudia kunidhuru. 3 Kwa hiyo niliwatuma wajumbe kwao na majibu haya: “Kazi ninayoifanya ni kubwa sana, siwezi kuja. Kwa nini niiache kazi isimame nije kwenu?” 4 Mara nne walinitumia ujumbe wa namna iyo hiyo, na kila mara niliwapa jibu lile lile.
5 Basi, mara ya tano, Sanbalati akamtuma msaidizi wake kwangu akiwa na ujumbe wa aina ile ile, naye alikuwa amechukua mkononi mwake barua isiyofungwa, 6 iliyokuwa imeandikwa:
“Habari imeenezwa miongoni mwa mataifa, naye Geshemu anasema kwamba ni kweli, kuwa wewe na Wayahudi mnafanya hila ya kuasi, ndiyo sababu mnajenga ukuta. Zaidi ya hayo, kufuatana na taarifa hizi, karibuni utakuwa mfalme wao, 7 na hata umewateua manabii wafanye tangazo hili kukuhusu wewe huko Yerusalemu: ‘Yuko mfalme katika Yuda!’ Sasa taarifa hii itarudishwa kwa mfalme. Basi njoo, tufanye shauri pamoja.”
8 Nilimpelekea jibu hili: “Hakuna jambo kama hilo unalosema linalofanyika. Unalitunga tu kwenye kichwa chako.”
9 Wote walikuwa wakijaribu kutuogopesha, wakifikiri hivi: “Mikono ya watu italegea kiasi kwamba hawataweza kufanya kazi, nayo haitakamilika.”
Lakini niliomba, “Ee Mungu, sasa nitie mikono yangu nguvu.”
10 Siku moja nilikwenda nyumbani kwa Shemaya mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, ambaye alikuwa amefungwa ndani ya nyumba yake. Akasema, “Tukutane katika nyumba ya Mungu, ndani ya Hekalu, na tufunge milango ya Hekalu, kwa sababu watu wanakuja kukuua. Naam, wanakuja usiku kukuua.”
11 Lakini nikasema, “Je, mtu kama mimi akimbie? Au mtu kama mimi aende Hekaluni kuokoa maisha yake? Sitakwenda!” 12 Nilitambua kwamba Mungu hakumtuma, bali alitabiri dhidi yangu kwa sababu Tobia na Sanbalati walikuwa wamemwajiri. 13 Alikuwa ameajiriwa kunitisha ili kwa kufanya jambo hili nitende dhambi, kisha waweze kuniharibia jina langu na kuniaibisha.
14 Ee Mungu wangu, wakumbuke Tobia na Sanbalati kwa sababu ya yale waliyotenda. Pia kumbuka nabii mke Noadia na manabii wengine ambao wamekuwa wakijaribu kunitisha.
15 Basi ukuta ukakamilika siku ya ishirini na tano mwezi wa Eluli, kazi ambayo ilichukua siku hamsini na mbili. 16 Adui zetu wote waliposikia kuhusu hili, mataifa yote yaliyotuzunguka yakaogopa na kupoteza ujasiri, kwa sababu yalitambua kuwa kazi hii imefanyika kwa msaada wa Mungu wetu.
17 Pia katika siku hizo wakuu wa Yuda walikuwa wakituma barua nyingi kwa Tobia, nayo majibu yaliyotoka kwa Tobia yaliendelea kuwajia. 18 Kwa kuwa watu wengi katika Yuda walikuwa wamemwapia Tobia, kwani alikuwa mkwewe Shekania mwana wa Ara, na Yehohanani mwanawe alikuwa amemwoa binti wa Meshulamu mwana wa Berekia. 19 Zaidi ya hayo, walikuwa wakiniarifu jinsi Tobia alivyo mtu mwema, nao walimwambia kila kitu nilichosema. Naye Tobia alituma barua za kunitisha.
Ukuta wa Yerusalemu Unawekwa Wakfu
27 Wakati wa kuwekwa wakfu ukuta wa Yerusalemu, Walawi walitafutwa kule walikokuwa wakiishi, nao wakaletwa Yerusalemu kuadhimisha kwa shangwe huko kuweka wakfu kwa nyimbo za shukrani na kwa uimbaji wakitumia matoazi, vinubi na zeze. 28 Pia waimbaji walikusanywa pamoja kutoka maeneo yaliyozunguka Yerusalemu, kutoka vijiji vya Wanetofathi, 29 kutoka Beth-Gilgali, na kutoka eneo la Geba na Azmawethi, kwa kuwa waimbaji walikuwa wamejijengea vijiji kuzunguka Yerusalemu. 30 Wakati makuhani na Walawi walipokuwa wamekwisha kujitakasa kwa kufuatana na desturi, waliwatakasa watu, malango na ukuta.
31 Niliwaagiza viongozi wa Yuda wapande juu ya ukuta. Pia niliagiza makundi mawili makubwa ya waimbaji waimbe nyimbo za kumshukuru Mungu. Kundi moja lilipanda juu ya ukuta upande wa kuume, kuelekea Lango la Samadi. 32 Hoshaya na nusu ya viongozi wa Yuda wakawafuata, 33 pamoja na Azaria, Ezra, Meshulamu, 34 Yuda, Benyamini, Shemaya, Yeremia, 35 pamoja na baadhi ya makuhani wenye tarumbeta, na pia walikuwa na Zekaria mwana wa Yonathani, mwana wa Shemaya, mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu, 36 pamoja na wenzake, Shemaya, Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Nethaneli, Yuda na Hanani, wakiwa na vyombo vya uimbaji, kama ilivyoagizwa na Daudi mtu wa Mungu. Mwandishi Ezra aliongoza maandamano. 37 Kwenye Lango la Chemchemi waliendelea moja kwa moja mpaka kwenye ngazi za Mji wa Daudi, kwenye mwinuko wa ukuta, na kupitia juu ya nyumba ya Daudi mpaka kwenye Lango la Maji upande wa mashariki.
38 Kundi la pili la waimbaji lilielekea upande wa kushoto. Niliwafuata juu ya ukuta, pamoja na nusu ya watu kupitia Mnara wa Tanuru mpaka kwenye Ukuta Mpana, 39 juu ya Lango la Efraimu, Lango la Yeshana, Lango la Samaki, Mnara wa Hananeli, na Mnara wa Mia, mpaka kwenye Lango la Kondoo. Walipofika kwenye Lango la Ulinzi wakasimama.
40 Kisha yale makundi mawili ya waimbaji yaliyoshukuru yakachukua nafasi zao katika nyumba ya Mungu. Nami pia nikafanya hivyo, pamoja na nusu ya maafisa, 41 na makuhani wafuatao: Eliakimu, Maaseya, Miniamini, Mikaya, Elioenai, Zekaria na Hanania wakiwa na tarumbeta zao, 42 na pia Maaseya, Shemaya, Eleazari, Uzi, Yehohanani, Malkiya, Elamu na Ezeri. Makundi haya yaliimba chini ya uongozi wa Yezrahia. 43 Siku hiyo watu walitoa dhabihu nyingi, wakishangilia kwa sababu Mungu aliwapa furaha kuu. Wanawake na watoto walishangilia pia. Sauti ya kushangilia huko Yerusalemu iliweza kusikika mbali sana.
Nehemia Arudi Uajemi
1 Baada ya ukuta kukamilika kujengwa upya na nikaweka milango, mabawabu wa lango, waimbaji, na Walawi waliteuliwa. 2 Nikamweka Hanani ndugu yangu kuwa kiongozi wa Yerusalemu, pamoja na Hanania jemadari wa ngome, kwa kuwa alikuwa mtu mwadilifu na mwenye kumcha Mungu kuliko watu wengine. 3 Nikawaambia, “Malango ya Yerusalemu yasifunguliwe mpaka jua litakapokuwa limepanda. Walinzi wa malango wakiwa bado kwenye zamu, waamuru wafunge milango na waweke makomeo. Pia wateueni wenyeji wa Yerusalemu wawe walinzi, kila mmoja kwenye lindo lake, na wengine karibu na nyumba zao wenyewe.”
4 Mji ulikuwa mkubwa, tena wenye nafasi nyingi, lakini walikuwepo watu wachache ndani yake, nazo nyumba zilikuwa bado ni magofu.