Kuta za Yerusalemu Zajengwa Upya (continued)

445 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Nehemia 4–5

1 Sanbalati aliposikia kwamba tulikuwa tunajenga ukuta upya, alikasirika na akawa na uchungu sana. Aliwadhihaki Wayahudi 2 mbele ya rafiki zake na jeshi la Samaria, akisema, “Hawa Wayahudi wanyonge wanafanya nini? Je, wataweza kuurudishia ukuta wao? Je, watatoa dhabihu? Je, wataweza kumaliza kuujenga kwa siku moja? Je, wataweza kufufua mawe kutoka malundo ya vifusi yaliyoungua hivyo?”

3 Tobia Mwamoni aliyekuwa upande wake akasema, “Wanachokijenga, hata kama mbweha angepanda juu yake, huo ukuta wao wa mawe angeliubomoa!”

4 Ee Mungu wetu, utusikie, kwa kuwa tumedharauliwa. Warudishie matukano yao kwenye vichwa vyao wenyewe. Uwatoe ili wawe nyara katika nchi ya waliowateka. 5 Usiusitiri uovu wao, wala usifute dhambi zao mbele zako, kwa kuwa wamewatukana wajenzi mbele.

6 Basi tuliujenga upya ukuta mpaka wote ukafikia nusu ya kimo chake, kwa kuwa watu walifanya kazi kwa moyo wote.

7 Lakini wakati Sanbalati, Tobia, Waarabu, Waamoni na watu wa Ashdodi waliposikia kuwa ukarabati wa kuta za Yerusalemu ulikuwa umeendelea na mianya ilikuwa inazibwa, walikasirika sana. 8 Wote walifanya shauri pamoja kuja kupigana dhidi ya Yerusalemu, na kuchochea machafuko dhidi yake. 9 Lakini tulimwomba Mungu wetu, na tukaweka ulinzi usiku na mchana kupambana na tishio hili.

10 Wakati ule ule, watu wa Yuda wakasema, “Nguvu za wafanyakazi zinapungua, nacho kifusi ni kingi mno, kiasi kwamba hatuwezi kuujenga upya ukuta.”

11 Pia adui zetu walisema, “Kabla hawajajua au kutuona, tutakuwa palepale katikati yao, na tutawaua na kuikomesha hiyo kazi.”

12 Kisha Wayahudi ambao waliishi karibu nao walikuja zaidi ya mara kumi na kutuambia, “Popote mtakapoelekea, watatushambulia.”

13 Kwa hiyo nikaweka baadhi ya watu nyuma ya sehemu za chini za ukuta kwenye sehemu zilizo wazi, nikawaweka kufuatana na jamaa zao, wakiwa na panga, mikuki na pinde zao. 14 Baada ya kuona hali ilivyo, nikasimama na kuwaambia wakuu, maafisa na wengine wote, “Msiwaogope. Mkumbukeni Bwana, ambaye ni mkuu mwenye kuogofya. Piganeni kwa ajili ya ndugu zenu, wana wenu na binti zenu, wake zenu na nyumba zenu.”

15 Adui zetu waliposikia kwamba tumetambua hila yao, na kwamba Mungu amevuruga shauri lao, sote tulirudi kwenye ukuta, kila mmoja kwenye kazi yake.

16 Kuanzia siku ile na kuendelea, nusu ya watu wangu walifanya kazi ya ujenzi, na nusu nyingine wakashika mikuki, ngao, pinde na dirii. Maafisa walijipanga nyuma ya watu wote wa Yuda 17 waliokuwa wakijenga ukuta. Wale waliobeba vifaa vya ujenzi walifanya kazi yao kwa mkono mmoja, na kushika silaha kwa mkono mwingine, 18 na kila mjenzi alijifunga upanga wake upande mmoja akiwa anafanya kazi. Lakini mtu wa kupiga baragumu alikaa pamoja nami.

19 Kisha nikawaambia wakuu, maafisa na watu wengine wote, “Kazi hii ni kubwa na imeenea sehemu kubwa, nasi tumetawanyika kila mmoja akiwa mbali na mwenzake juu ya ukuta. 20 Popote mtakaposikia sauti ya baragumu, jiungeni nasi huko. Mungu wetu atatupigania!”

21 Basi tuliendelea na kazi, nusu ya watu wakishikilia mikuki, kuanzia mawio ya jua hadi nyota zilipoonekana. 22 Wakati huo pia niliwaambia watu, “Kila mtu na msaidizi wake wakae ndani ya Yerusalemu wakati wa usiku, ili waweze kutumika kama walinzi wakati wa usiku, na kufanya kazi wakati wa mchana.” 23 Mimi, wala ndugu zangu, wala watu wangu, wala walinzi waliokuwa pamoja nami hatukuvua nguo zetu. Kila mmoja alikuwa na silaha yake, hata alipokwenda kuchota maji.

5:1 Wakati huu wanaume na wake zao wakalia kilio kikuu dhidi ya ndugu zao Wayahudi. 2 Baadhi yao walikuwa wakisema, “Sisi na wana wetu na binti zetu tuko wengi. Ili tuweze kula na kuishi, ni lazima tupate nafaka.”

3 Wengine walikuwa wakisema, “Tunaweka rehani mashamba yetu, mashamba ya mizabibu, na nyumba zetu ili tupate nafaka wakati wa njaa.”

4 Bado kukawa na wengine waliokuwa wakisema, “Ilitubidi tukope fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa ajili ya mashamba yetu na mashamba yetu ya mizabibu. 5 Ingawa sisi ni mwili na damu moja sawa na watu wa nchi yetu, na ijapo wana wetu ni wazuri kama wana wao, bado inatupasa kuwatoa wana wetu na binti zetu kwenye utumwa. Baadhi ya binti zetu wameshakuwa watumwa tayari, lakini hatuna uwezo wa kuwakomboa, kwa sababu mashamba yetu na mashamba ya mizabibu yetu ni mali ya wengine.”

6 Niliposikia kilio chao na malalamiko haya, nilikasirika sana. 7 Nikayatafakari katika akili yangu, nikiwalaumu wakuu na maafisa. Nikawaambia, “Mnawaonea ndugu zenu kwa kuwatoza riba!” Basi nikaitisha mkutano mkubwa ili kuwashughulikia 8 na kusema: “Kulingana na uwezo wetu, tumewakomboa ndugu zetu Wayahudi waliokuwa wameuzwa kwa watu wasioamini. Sasa mnawauza ndugu zenu, ili wauzwe tena kwetu!” Walinyamaza kimya, kwa sababu hawakupata chochote cha kusema.

9 Basi nikaendelea kusema, “Mnachokifanya si sawa. Je, haikuwapasa kutembea katika hofu ya Mungu wetu ili tuepukane na shutuma za adui zetu wasioamini? 10 Mimi na ndugu zangu na watu wangu tunawakopesha watu fedha na nafaka. Lakini jambo hili la kutoza riba likome! 11 Warudishieni mara moja mashamba yao, mashamba yao ya mizabibu, mashamba yao ya mizeituni, na nyumba zao, pia riba yao mnayowatoza na sehemu ya fungu la mia la fedha, nafaka, divai mpya na mafuta.”

12 Wakasema, “Tutawarudishia na hatutataka kitu chochote zaidi kutoka kwao. Tutafanya kama ulivyosema.”

Kisha nikawaita makuhani na kuwafanya wakuu na maafisa kuapa kufanya kile walichoahidi. 13 Pia nikakungʼuta makunjo ya vazi langu na kusema, “Kila mtu ambaye hatatimiza ahadi hii, Mungu na amkungʼute hivi kutoka nyumba yake na katika mali zake. Basi mtu wa namna hiyo akungʼutiwe nje na aachwe bila kitu!”

Waliposikia hili, mkutano wote ukasema, “Amen,” na wakamtukuza Bwana. Nao watu wakafanya kama walivyokuwa wameahidi.

14 Zaidi ya hayo, kutoka mwaka wa ishirini wa Mfalme Artashasta, wakati nilipoteuliwa kuwa mtawala wao katika nchi ya Yuda, mpaka mwaka wake wa thelathini na mbili, yaani miaka kumi na miwili, mimi wala ndugu zangu hatukula chakula ambacho kwa kawaida hupewa watawala. 15 Lakini watawala wa mwanzoni, wale walionitangulia, waliwalemea watu na kuchukua kutoka kwao shekeli arobaini za fedha, pamoja na chakula na mvinyo. Wasaidizi wao pia walijifanya wakuu juu ya watu. Lakini kwa kumheshimu Mungu sikufanya hivyo. 16 Badala yake, nilijitoa kwa bidii katika kazi ya ukuta huu. Watu wangu wote walikutanika pale kwa ajili ya kazi. Hatukujipatia shamba lolote.

17 Zaidi ya hayo, Wayahudi na maafisa 150 walikula mezani pangu, pamoja na wale waliotujia kutoka mataifa jirani. 18 Kila siku niliandaliwa maksai mmoja, kondoo sita wazuri, na kuku, na mvinyo wa kila aina kwa wingi kila baada ya siku kumi. Licha ya mambo haya yote, sikudai chakula kilichokuwa fungu la mtawala, kwa sababu madai yalikuwa mazito sana kwa watu hawa.

19 Unikumbuke kwa fadhili, Ee Mungu wangu, kwa yote niliyofanya kwa ajili ya watu hawa.