Kipindi cha 6: Kutoka kwa Rehoboamu hadi Uhamishoni Babeli

Tangu Rehoboamu alipotwaa kiti cha enzi hadi utumwani Babeli.

Sehemu ya 1: Utawala wa Rehoboamu

Ufalme wa Yuda

Makabila Kumi Yanaasi

975 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Wafalme 14:21

21 Rehoboamu mwana wa Solomoni alikuwa mfalme wa Yuda. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji ambao Bwana alikuwa ameuchagua kutoka makabila yote ya Israeli ili apate kuliweka humo Jina lake. Mama yake aliitwa Naama, ambaye alikuwa Mwamoni.

1 Wafalme 12:1–24

1 Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Waisraeli wote walikuwa wamekwenda huko kumfanya yeye kuwa mfalme. 2 Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia hili (alikuwa bado yuko Misri alikokuwa amekimbilia awe mbali na Mfalme Solomoni), akarudi kutoka Misri. 3 Kwa hiyo wakatuma watu kumwita Yeroboamu, yeye na kusanyiko lote la Israeli wakamwendea Rehoboamu na kumwambia, 4 “Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini sasa tupunguzie kazi za kikatili na nira nzito aliyoweka juu yetu, nasi tutakutumikia.”

5 Rehoboamu akajibu, “Nendeni kwa muda wa siku tatu na kisha mnirudie.” Basi watu wakaenda zao.

6 Kisha Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee ambao walimtumikia Solomoni baba yake wakati wa uhai wake akawauliza, “Mnanishauri nini katika kuwajibu watu hawa?”

7 Wakajibu, “Kama leo utakuwa mtumishi wa watu hawa na kuwahudumia na kuwapa jibu linaloridhisha, watakuwa watumishi wako daima.”

8 Lakini Rehoboamu akakataa shauri alilopewa na wazee na akataka ushauri kwa vijana wanaume rika lake waliokuwa wakimtumikia. 9 Akawauliza, “Ninyi ushauri wenu ni nini? Tutawajibuje watu hawa wanaoniambia, ‘Ifanye nyepesi nira baba yako aliyoweka juu yetu?’ ”

10 Wale vijana wa rika lake wakamjibu, “Waambie watu hawa waliokuambia, ‘Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini ifanye nira yetu nyepesi,’ kuwa, ‘Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. 11 Baba yangu aliweka nira nzito juu yenu, mimi nitaifanya hata iwe nzito zaidi. Baba yangu aliwachapa kwa mijeledi, mimi nitawachapa kwa nge.’ ”

12 Siku tatu baadaye, Yeroboamu na watu wote wakamrudia Rehoboamu, kama mfalme alivyokuwa amesema, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.” 13 Mfalme akawajibu watu kwa ukatili. Akikataa shauri alilopewa na wazee, 14 akafuata shauri la vijana wa rika lake na kusema, “Baba yangu alifanya nira yenu kuwa nzito, mimi nitaifanya kuwa nzito zaidi. Baba yangu aliwachapa kwa mijeledi, mimi nitawachapa kwa nge.” 15 Kwa hiyo mfalme hakuwasikiliza watu, kwa kuwa jambo hili lilitoka kwa Bwana, ili kutimiza neno ambalo Bwana alikuwa amenena kwa Yeroboamu mwana wa Nebati kupitia Ahiya Mshiloni.

16 Israeli wote walipoona kuwa mfalme amekataa kuwasikiliza, wakamjibu mfalme:

“Tuna fungu gani kwa Daudi?

Sisi hatuna urithi kwa mwana wa Yese.

Nendeni kwenye mahema yenu, ee Israeli!

Angalia nyumba yako mwenyewe, ee Daudi!”

Hivyo Waisraeli wakaenda kwenye mahema yao. 17 Lakini kwa habari ya Waisraeli waliokuwa wakiishi katika miji ya Yuda, Rehoboamu akaendelea kuwatawala bado.

18 Mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, aliyekuwa msimamizi wa wale waliofanya kazi ngumu kwa kulazimishwa, lakini Israeli wote wakampiga kwa mawe hadi akafa. Hata hivyo, Mfalme Rehoboamu, akafanikiwa kuingia kwenye gari lake na kutorokea Yerusalemu. 19 Hivyo Israeli wakaasi dhidi ya nyumba ya Daudi hadi leo.

20 Waisraeli wote waliposikia kwamba Yeroboamu amerudi, wakatuma watu na kumwita kwenye kusanyiko na kumfanya mfalme juu ya Israeli yote. Ni kabila la Yuda peke yake lililobaki kuwa tiifu kwa nyumba ya Daudi.

21 Ikawa Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba yote ya Yuda na kabila la Benyamini, wanaume wapiganaji 180,000, kufanya vita dhidi ya nyumba ya Israeli na kuurudisha tena ufalme kwa Rehoboamu mwana wa Solomoni.

22 Lakini neno hili la Mungu likamjia Shemaya mtu wa Mungu: 23 “Mwambie Rehoboamu mwana wa Solomoni mfalme wa Yuda, na nyumba yote ya Yuda na Benyamini, na watu wengine wote, 24 ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Msipande kupigana dhidi ya ndugu zenu, Waisraeli. Nendeni nyumbani, kila mmoja wenu, kwa kuwa hili nimelitenda mimi.’ ” Kwa hiyo wakalitii neno la Bwana na kurudi nyumbani, kama Bwana alivyokuwa ameagiza.

Rehoboamu Anatawala Yuda 973 KK

2 Nyakati 11:5–12:1

5 Rehoboamu akaishi Yerusalemu akajenga miji yenye ngome katika Yuda: 6 Akajenga Bethlehemu, Etamu, Tekoa, 7 Beth-Suri, Soko, Adulamu, 8 Gathi, Maresha, Zifu, 9 Adoraimu, Lakishi, Azeka, 10 Sora, Aiyaloni na Hebroni. Hii ndiyo iliyokuwa miji iliyojengewa ngome katika Yuda na Benyamini. 11 Akaimarisha ulinzi wake na kuweka majemadari ndani yake, pamoja na ghala za mahitaji ya vyakula, mafuta ya zeituni na divai. 12 Akaweka ngao na mikuki katika miji na kuifanya iwe imara sana. Kwa hiyo Yuda na Benyamini zikawa zake.

13 Makuhani na Walawi kutoka sehemu zote za Israeli wakawa upande wake. 14 Pia Walawi wakaacha maeneo yao ya malisho na mali zao, wakaja Yuda na Yerusalemu kwa sababu Yeroboamu na wanawe walikuwa wamewakataa wasiwe makuhani wa Bwana. 15 Naye akawa amechagua makuhani wake mwenyewe kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia sanamu za mbuzi na za ndama ambazo alikuwa ametengeneza. 16 Wale waliotoka katika kila kabila la Israeli ambao walielekeza mioyo yao kumtafuta Bwana, Mungu wa Israeli, wakawafuata Walawi huko Yerusalemu kumtolea Bwana dhabihu, Mungu wa baba zao. 17 Wakaimarisha ufalme wa Yuda na kumuunga mkono Rehoboamu mwana wa Solomoni miaka mitatu, wakienenda katika njia za Daudi na Solomoni katika wakati huu.

18 Rehoboamu alimwoa Mahalati ambaye alikuwa binti Yeremothi mwana wa Daudi, mamaye alikuwa Abihaili binti Eliabu mwana wa Yese. 19 Mahalati alimzalia Rehoboamu wana: Yeushi, Shemaria na Zahamu. 20 Kisha akamwoa Maaka binti Absalomu, ambaye alimzalia: Abiya, Atai, Ziza na Shelomithi. 21 Rehoboamu akampenda Maaka binti Absalomu zaidi kuliko wakeze wengine na masuria wake. Kwa jumla alikuwa na wake kumi na wanane na masuria sitini, wana ishirini na wanane na binti sitini.

22 Rehoboamu akamweka Abiya mwana wa Maaka, kuwa mkuu wa wana wa mfalme miongoni mwa ndugu zake ili amfanye mfalme. 23 Akatenda kwa busara, akiwasambaza baadhi ya wanawe katika wilaya zote za Yuda na Benyamini, pamoja na miji yote yenye ngome. Akawapa mahitaji tele na kuwaoza wake wengi.

12:1 Baada ya nafasi ya Rehoboamu kuimarika na kuwa na nguvu, yeye na Israeli yote waliiacha sheria ya Bwana Mungu.

1 Wafalme 14:22–24

22 Yuda wakatenda maovu machoni pa Bwana. Kwa dhambi walizotenda wakachochea hasira yake yenye wivu zaidi kuliko baba zao walivyofanya. 23 Pia wakajijengea mahali pa juu pa kuabudia miungu, mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kilichoinuka na kila mti uliotanda. 24 Walikuwepo hata wanaume mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu katika nchi; watu wakajiingiza katika kutenda machukizo ya mataifa ambayo Bwana aliyafukuza mbele ya Waisraeli.