Shishaki Anavamia Yuda

970 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Nyakati 12:2–16

2 Kwa sababu hawakuwa waaminifu kwa Bwana, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu. 3 Akiwa na magari ya vita 1,200 na wapanda farasi 60,000 na idadi isiyohesabika ya majeshi ya Walibia, Wasukii na Wakushi yaliyokuja pamoja naye kutoka Misri. 4 Akateka miji ya Yuda yenye ngome akaendelea mpaka Yerusalemu.

5 Ndipo nabii Shemaya akaja kwa Rehoboamu na kwa viongozi wa Yuda waliokuwa wamekusanyika huko Yerusalemu kwa ajili ya hofu ya Shishaki naye akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana, ‘Ninyi mmeniacha mimi, kwa hiyo, mimi nami sasa ninawaacha ninyi mkononi mwa Shishaki.’ ”

6 Viongozi wa Israeli na mfalme wakajinyenyekeza na kusema, “Bwana Mungu ni mwenye haki.”

7 Bwana Mungu alipoona kwamba wamejinyenyekeza, neno hili la Bwana likamjia Shemaya: “Maadamu wamejinyenyekeza, sitawaangamiza bali hivi karibuni nitawapatia wokovu. Ghadhabu yangu haitamwagwa juu ya Yerusalemu kwa kupitia Shishaki. 8 Hata hivyo, watamtumikia Shishaki ili wapate kujifunza tofauti kati ya kunitumikia mimi na kuwatumikia wafalme wa nchi nyingine.”

9 Shishaki mfalme wa Misri alipoishambulia Yerusalemu, alichukua hazina za Hekalu la Bwana na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao za dhahabu ambazo Solomoni alikuwa amezitengeneza. 10 Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme. 11 Kila wakati mfalme alipokwenda katika Hekalu la Bwana walinzi walikwenda pamoja naye wakiwa wamebeba hizo ngao na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi.

12 Kwa sababu Rehoboamu alijinyenyekeza, hasira ya Bwana ikageukia mbali naye, hakuangamizwa kabisa. Kukawa na hali nzuri katika Yuda.

13 Mfalme Rehoboamu akajiweka imara katika Yerusalemu na akaendelea kuwa mfalme. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na mmoja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na saba, mji ambao Bwana alikuwa ameuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli ili aliweke Jina lake humo. Mama yake aliitwa Naama, alikuwa Mwamoni. 14 Rehoboamu akatenda maovu kwa sababu hakuuelekeza moyo wake katika kumtafuta Bwana Mungu.

15 Kwa habari ya matukio katika utawala wa Rehoboamu, tangu mwanzo mpaka mwisho, je, hayakuandikwa katika kumbukumbu za nabii Shemaya na mwonaji Ido zinazohusiana na vizazi? Kulikuwako na vita mara kwa mara kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. 16 Rehoboamu akalala na baba zake, akazikwa katika Mji wa Daudi. Naye Abiya mwanawe akawa mfalme baada yake.

2 Nyakati 10:1–11:4

1 Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Waisraeli wote walikuwa wamekwenda huko kumfanya yeye kuwa mfalme. 2 Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia hili (alikuwa bado yuko Misri alikokuwa amekimbilia awe mbali na Mfalme Solomoni), akarudi kutoka Misri. 3 Kwa hiyo wakatuma watu kumwita Yeroboamu, yeye na kusanyiko lote la Israeli wakamwendea Rehoboamu na kumwambia, 4 “Baba yako aliweka nira nzito, lakini sasa tupunguzie kazi za kikatili na nira nzito aliyoweka juu yetu, nasi tutakutumikia.”

5 Rehoboamu akajibu, “Nendeni kwa muda wa siku tatu na kisha mnirudie.” Basi watu wakaenda zao.

6 Kisha Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee ambao walimtumikia Solomoni baba yake wakati wa uhai wake akawauliza, “Mnanishauri nini katika kuwajibu watu hawa?”

7 Wakajibu, “Kama leo utakuwa mtumishi wa watu hawa na kuwahudumia na kuwapa jibu linaloridhisha, watakuwa watumishi wako daima.”

8 Lakini Rehoboamu akakataa shauri alilopewa na wazee na akataka ushauri kwa vijana wanaume rika lake waliokuwa wakimtumikia. 9 Akawauliza, “Ninyi ushauri wenu ni nini? Tutawajibuje watu hawa wanaoniambia, ‘Ifanye nyepesi nira baba yako aliyoweka juu yetu?’ ”

10 Wale vijana wa rika lake wakamjibu, “Waambie watu hawa waliokuambia, ‘Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini ifanye nira yetu nyepesi,’ kuwa, ‘Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. 11 Baba yangu aliweka nira nzito juu yenu, mimi nitaifanya hata iwe nzito zaidi. Baba yangu aliwachapa kwa mijeledi; mimi nitawachapa kwa nge.’ ”

12 Siku tatu baadaye, Yeroboamu na watu wote wakamrudia Rehoboamu, kama mfalme alivyokuwa amesema, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.” 13 Mfalme akawajibu watu kwa ukatili. Akikataa shauri alilopewa na wazee, 14 akafuata shauri la vijana wa rika lake na kusema, “Baba yangu alifanya nira yenu kuwa nzito, mimi nitaifanya kuwa nzito zaidi. Baba yangu aliwachapa kwa mijeledi, mimi nitawachapa kwa nge.” 15 Kwa hiyo mfalme hakuwasikiliza watu, kwa kuwa jambo hili lilitoka kwa Mungu ili kutimiza neno ambalo Bwana alikuwa amenena kwa Yeroboamu mwana wa Nebati kupitia Ahiya Mshiloni.

16 Israeli wote walipoona kuwa mfalme amekataa kuwasikiliza, wakamjibu mfalme:

“Tuna fungu gani kwa Daudi?

Sisi hatuna urithi kwa mwana wa Yese.

Nendeni kwenye mahema yenu, ee Israeli,

angalia nyumba yako mwenyewe, ee Daudi!”

Hivyo Waisraeli wakaenda kwenye mahema yao. 17 Lakini kwa habari ya Waisraeli waliokuwa wakiishi katika miji ya Yuda, Rehoboamu akaendelea kuwatawala bado.

18 Mfalme Rehoboamu akamtuma Adoniramu aliyekuwa msimamizi wa wale waliofanya kazi ngumu kwa kulazimishwa, lakini Israeli wote wakampiga kwa mawe hadi akafa. Hata hivyo, Mfalme Rehoboamu, akafanikiwa kuingia kwenye gari lake na kutorokea Yerusalemu. 19 Hivyo Israeli wakaasi dhidi ya nyumba ya Daudi hadi leo.

11:1 Ikawa Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba ya Yuda na ya Benyamini, wanaume wapiganaji 180,000, kufanya vita dhidi ya nyumba ya Israeli na kuurudisha tena ufalme kwa Rehoboamu mwana wa Solomoni.

2 Lakini neno hili la Bwana likamjia Shemaya mtu wa Mungu: 3 “Mwambie Rehoboamu mwana wa Solomoni mfalme wa Yuda, na Israeli wote walioko Yuda na Benyamini, 4 ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Msipande kupigana dhidi ya ndugu zenu. Nendeni nyumbani, kila mmoja wenu, kwa kuwa hili nimelitenda mimi.’ ” Kwa hiyo wakalitii neno la Bwana na wakaacha kwenda kupigana dhidi ya Yeroboamu.

1 Wafalme 14:25–31

25 Katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu. 26 Akachukua hazina za Hekalu la Bwana na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao zote za dhahabu ambazo Solomoni alikuwa amezitengeneza. 27 Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme. 28 Kila wakati mfalme alipokwenda katika Hekalu la Bwana, walinzi walizichukua hizo ngao, na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi.

29 Kwa matukio mengine ya utawala wa Rehoboamu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 30 Kulikuwa na vita vinavyoendelea kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. 31 Naye Rehoboamu akalala na baba zake, na akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama, ambaye alikuwa Mwamoni. Naye Abiya mwanawe akawa mfalme baada yake.