Baragumu la Saba: Kanisa Linafurahi

Baragumu la saba linapigwa. Kanisa la ulimwengu wote linafurahia ushindi unaotarajiwa wa mashahidi mwishoni mwa miaka 1260.

96 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ufunuo 11:15–18

15 Yule malaika wa saba akaipiga tarumbeta yake, pakawa na sauti kubwa mbinguni iliyosema:

“Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake,

naye atatawala milele na milele.”

16 Nao wale wazee ishirini na wanne, waliokuwa wameketi mbele za Mungu, kwenye viti vyao vya enzi, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, 17 wakisema:

“Tunakushukuru, Bwana Mungu Mwenyezi,

uliyeko na uliyekuwako,

kwa kuwa umetwaa uweza wako mkuu

na ukaanza kutawala.

18 Mataifa walikasirika nao

wakati wa ghadhabu yako umewadia.

Wakati umewadia wa kuwahukumu waliokufa

na kuwapa thawabu watumishi wako manabii

na watakatifu wako pamoja na wale wote

wanaoliheshimu Jina lako,

wakubwa kwa wadogo:

na kuwaangamiza wale wanaoiangamiza dunia.”

Joka Linalitesa Kanisa

Sehemu ya pili ya hati ndogo ya kukunjwa. Kwa mifano ya mwanamke anayejifungua mtoto wa kiume kwa uchungu, na kufukuzwa kwenda nyikani na joka lenye vichwa saba na pembe kumi, inatabiri kuteswa kwa kanisa la Kristo, linalowazaa Wakristo wa kweli na waaminifu, na roho mbaya iliyoleta uovu duniani kwa mara ya kwanza. Pambano hili pia linadumu miaka 1260, kuanzia 606 hadi 1866.

Ufunuo 11:19–12:17

19 Ndipo hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana humo ndani. Kukatokea mianga ya umeme wa radi, ngurumo, sauti za radi, tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.

12:1 Kukaonekana ishara kuu mbinguni: Palikuwa na mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ukiwa chini ya miguu yake, na taji ya nyota kumi na mbili ilikuwa kichwani mwake. 2 Alikuwa na mimba naye akilia kwa uchungu kwa kuwa alikuwa anakaribia kuzaa. 3 Kisha ishara nyingine ikaonekana mbinguni: Likaonekana joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na pembe kumi na taji saba katika vichwa vyake. 4 Mkia wake ukakokota theluthi ya nyota zote angani na kuziangusha katika nchi. Ndipo lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa ili lipate kumla huyo mtoto mara tu atakapozaliwa. 5 Yule mwanamke akazaa mtoto mwanaume, atakayeyatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya utawala ya chuma. Lakini huyo mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu kwenye kiti chake cha enzi. 6 Yule mwanamke akakimbilia jangwani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali ili apate kutunzwa huko kwa muda wa siku 1,260.

7 Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao. 8 Lakini joka na malaika zake wakashindwa, na hapakuwa tena na nafasi yao huko mbinguni. 9 Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwengu wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake.

10 Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema:

“Sasa wokovu na uweza na Ufalme wa Mungu wetu umekuja

na mamlaka ya Kristo wake.

Kwa kuwa ametupwa chini

mshtaki wa ndugu zetu,

anayewashtaki mbele za Mungu

usiku na mchana.

11 Nao wakamshinda

kwa damu ya Mwana-Kondoo

na kwa neno la ushuhuda wao.

Wala wao hawakuyapenda maisha yao

hata kufa.

12 Kwa hiyo, furahini ninyi mbingu

na wote wakaao humo!

Lakini ole wenu nchi na bahari,

kwa maana huyo ibilisi ameshuka kwenu,

akiwa amejaa ghadhabu,

kwa sababu anajua ya kuwa

muda wake ni mfupi!”

13 Lile joka lilipoona kuwa limetupwa chini duniani, lilimfuatilia yule mwanamke aliyekuwa amezaa mtoto mwanaume. 14 Lakini huyo mwanamke akapewa mabawa mawili ya tai mkubwa, kusudi aweze kuruka mpaka mahali palipotayarishwa kwa ajili yake huko jangwani, ambako atatunzwa kwa wakati na nyakati na nusu, ya wakati ambako yule joka hawezi kufika. 15 Ndipo lile joka likamwaga maji kama mto kutoka kinywani mwake, ili kumfikia huyo mwanamke na kumkumba kama mafuriko. 16 Lakini nchi ikamsaidia huyo mwanamke kwa kufungua kinywa na kuumeza huo mto ambao huyo joka alikuwa ameutoa kinywani mwake. 17 Kisha lile joka likapatwa na hasira kali kwa ajili ya huyo mwanamke na likaondoka ili kupigana vita na watoto waliosalia wa huyo mwanamke, yaani, wale wanaozitii amri za Mungu na kuushika ushuhuda wa Yesu Kristo. Lile joka likasimama kwenye mchanga wa bahari.

Wakala wa Roho Mbaya Ni Mamlaka ya Rumi

Sehemu ya tatu ya gombo dogo, inayoeleza wakala wa roho mwovu aliyelitesa kanisa la kweli la Mungu kwa miaka 1260, kwa alama zinazolingana na mamlaka ya Rumi pekee.

Ufunuo 13:1–10

1 Yule joka akajikita katika mchanga ulioko ufuoni mwa bahari.

Nami nikamwona mnyama akitoka ndani ya bahari. Mnyama huyo alikuwa na pembe kumi na vichwa saba, akiwa na taji kumi kwenye hizo pembe zake, na juu ya kila kichwa kulikuwa na jina la kukufuru. 2 Mnyama yule niliyemwona alifanana na chui, lakini miguu yake ilikuwa kama ya dubu na kichwa chake kama cha simba. Lile joka likampa huyo mnyama nguvu zake, kiti chake cha enzi na mamlaka makubwa. 3 Kimojawapo ya vichwa vya huyo mnyama kilikuwa kama kilichokwisha kupata jeraha la mauti, lakini jeraha hilo la mauti likapona. Ulimwengu wote ukashangaa ukamfuata huyo mnyama. 4 Watu wakaliabudu lile joka kwa sababu lilikuwa limempa huyo mnyama mamlaka yake, pia wakamwabudu huyo mnyama na kuuliza, “Ni nani aliye kama huyu mnyama? Ni nani awezaye kupigana vita naye?”

5 Huyo mnyama akapewa kusema maneno ya kiburi na kukufuru na kutumia mamlaka yake kwa muda wa miezi arobaini na miwili. 6 Akafungua kinywa chake ili kumkufuru Mungu, akilitukana Jina lake na mahali aishipo na wale wakaao mbinguni. 7 Pia akaruhusiwa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda. Akapewa uwezo juu ya watu wa kila kabila, jamaa, lugha na taifa. 8 Nao watu wote waishio duniani watamwabudu huyo mnyama, yaani, wale wote ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo aliyechinjwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

9 Yeye aliye na sikio na asikie.

10 Ikiwa mtu ni wa kuchukuliwa mateka,

atachukuliwa mateka.

Ikiwa mtu ni wa kuuawa kwa upanga,

atauawa kwa upanga.

Hapa ndipo penye wito wa subira na imani ya watakatifu.

Utawala wa Kiroho wa Kanisa la Rumi

Sehemu ya nne ya gombo dogo, inayoonyesha utawala wa kiroho wa Kanisa la Rumi, ulioungwa mkono na kuidhinishwa na mamlaka za kilimwengu za Ulaya katika kipindi cha miaka 1260.

Ufunuo 13:11–18

11 Kisha nikamwona mnyama mwingine, akipanda juu kutoka dunia. Alikuwa na pembe mbili kama mwana-kondoo, lakini akanena kama joka. 12 Akatumia mamlaka yote ya yule mnyama wa kwanza kwa niaba yake, naye akawafanya wote wakaao duniani kumwabudu yule mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona. 13 Naye akafanya ishara kuu na za ajabu, hata kusababisha moto kushuka toka mbinguni kuja duniani watu wakiona waziwazi. 14 Kwa sababu ya zile ishara alizokuwa amepewa uwezo wa kuzifanya kwa niaba ya yule mnyama wa kwanza, akawadanganya wakaao duniani. Akawaamuru wasimamishe sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi. 15 Akapewa uwezo wa kuipa pumzi ile sanamu ya yule mnyama wa kwanza, ili iweze kusema na kuwasababisha wale wote waliokataa kuiabudu hiyo sanamu kuuawa. 16 Pia alimlazimisha kila mmoja, mdogo na mkubwa, tajiri na maskini, mtu huru na mtumwa, atiwe chapa kwenye mkono wake wa kuume au kwenye kipaji chake cha uso, 17 ili kwamba mtu yeyote asiweze kununua wala kuuza isipokuwa amekuwa na hiyo chapa, ambayo ni jina la huyo mnyama au tarakimu za jina lake.

18 Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na ufahamu na ahesabu tarakimu za huyo mnyama, kwa maana ni tarakimu za kibinadamu. Tarakimu zake ni 666.