Bakuli la Saba: Vita vya Armagedoni
Bakuli la saba linamiminwa. Miaka 1260 sasa imepita. Mavuno ya zabibu za ghadhabu ya Mungu, yaliyotabiriwa zamani sana na manabii wa kale, sasa yanaanza, yakiambatana na misukosuko mikubwa na vita vya muda mrefu duniani kote. Sasa unafika wakati wa kuamuliwa kwa pambano la muda mrefu kati ya wema na uovu. Dini za uongo za upapa na kutokuamini zinaungana dhidi ya mabaki ya kanisa, dhidi ya Wayahudi wanaokusanyika kwa ajili ya kurejeshwa kwao kulikokuwa kumeahidiwa tangu zamani, na dhidi ya taifa kubwa lenye nguvu za baharini, ambalo yaelekea ni Uingereza (Isaya 17:18), hadi vita vya Armagedoni vinapotokea sasa huko Palestina. Huenda bakuli hili likahusisha kipindi cha miaka mingi.
96 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
17 Malaika wa saba akamimina bakuli lake angani na sauti kubwa ikatoka mle hekaluni katika kile kiti cha enzi, ikisema, “Imekwisha kuwa!” 18 Kukawa na mianga ya umeme wa radi, ngurumo, radi na tetemeko kubwa la ardhi. Hapajawa kamwe na tetemeko la ardhi kama hilo tangu mwanadamu awepo duniani, hivyo lilikuwa tetemeko kubwa ajabu. 19 Ule mji mkubwa ukagawanyika katika sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikaanguka. Mungu akaukumbuka Babeli Mkuu na kumpa kikombe kilichojaa mvinyo wa ghadhabu ya hasira yake. 20 Kila kisiwa kikatoweka wala milima haikuonekana. 21 Mvua kubwa ya mawe yenye uzito wa talanta moja ikashuka kutoka mbinguni, ikawaangukia wanadamu. Nao wanadamu wakamlaani Mungu kwa ajili ya hayo mapigo ya mvua ya mawe, kwa sababu pigo hilo lilikuwa la kutisha.
Upapa Kabla ya Kuanguka Kwake
Baada ya tangazo la jumla la matukio haya makubwa, nabii anaonyeshwa historia na hali ya upapa kabla ya kuangushwa kwake kwa mwisho.
1 Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba akaja akaniambia, “Njoo, nitakuonyesha adhabu ya yule kahaba mkuu, aketiye juu ya maji mengi. 2 Yule ambaye wafalme wa dunia walizini naye na watu wakaao duniani walilewa kwa mvinyo wa uzinzi wake.”
3 Kisha yule malaika akanichukua katika Roho akanipeleka jangwani. Huko nikamwona mwanamke mmoja ameketi juu ya mnyama mwekundu aliyejaa majina ya kumkufuru Mungu mwili mzima. Mnyama huyo alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. 4 Huyo mwanamke alikuwa amevaa mavazi ya rangi ya zambarau na nyekundu, akimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu kilichojaa mambo ya machukizo na uchafu wa uzinzi wake. 5 Kwenye kipaji chake cha uso palikuwa pameandikwa jina:
“Siri,
Babeli Mkuu,
Mama wa makahaba
na wa machukizo ya dunia.”
6 Nikaona kuwa huyo mwanamke alikuwa amelewa kwa damu ya watakatifu, yaani, damu ya wale watu waliouawa kwa ushuhuda wa Yesu.
Nilipomwona huyo mwanamke, nilistaajabu sana. 7 Ndipo yule malaika akaniambia, “Kwa nini unastaajabu? Nitakufafanulia siri ya huyo mwanamke na huyo mnyama aliyempanda, mwenye vichwa saba na pembe kumi. 8 Huyo mnyama ambaye ulimwona, wakati fulani alikuwepo, lakini sasa hayupo, naye atapanda kutoka lile Shimo na kwenda kwenye maangamizo yake. Watu waishio duniani ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima tangu kuumbwa kwa ulimwengu watastaajabu kumwona huyo mnyama, kwa maana alikuwepo wakati fulani, na sasa hayupo, lakini atakuwepo.
9 “Hapa ndipo penye wito wa akili pamoja na hekima. Vile vichwa saba ni vilima saba ambavyo huyo mwanamke amevikalia. 10 Pia hivyo vichwa saba ni wafalme saba ambao miongoni mwao watano wamekwisha kuanguka, yupo mwingine hajaja bado, lakini atakapokuja, atalazimika kukaa kwa muda mfupi. 11 Yule mnyama aliyekuwepo wakati fulani na ambaye sasa hayupo, yeye ni mfalme wa nane. Ni miongoni mwa wale saba, naye anakwenda kwenye maangamizi yake.
12 “Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi ambao bado hawajapokea ufalme, lakini watapokea mamlaka kuwa wafalme kwa saa moja pamoja na yule mnyama. 13 Hawa wana nia moja, nao watamwachia yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao. 14 Watafanya vita na Mwana-Kondoo, lakini Mwana-Kondoo atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme. Yeye atakuwa pamoja na watu wake walioitwa ambao ni wateule wake na wafuasi wake waaminifu.”
15 Kisha yule malaika akaniambia, “Yale maji uliyoyaona yule kahaba akiwa ameketi juu yake ni jamaa, makutano, mataifa na lugha. 16 Zile pembe kumi ulizoziona, pamoja na huyo mnyama, watamchukia huyo kahaba, watamfilisi na kumwacha uchi, watamla nyama yake na kumteketeza kwa moto. 17 Kwa maana Mungu ameweka mioyoni mwao kutimiza kusudi lake kwa kukubali kumpa yule mnyama mamlaka yao ya utawala mpaka maneno ya Mungu yatakapotimia. 18 Yule mwanamke uliyemwona ni ule mji mkubwa unaotawala juu ya wafalme wa dunia.”
Kuanguka kwa Upapa na Kutokuwa na Dini
Kuanguka kwa upapa na kwa kutokuwa na dini kunaelezwa kwa kina.
1 Baada ya haya nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni, akiwa na mamlaka makuu na dunia ikamulikiwa na mngʼao wake. 2 Naye akalia kwa nguvu kwa sauti kubwa, akisema:
“Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu!
Umekuwa makao ya mashetani
na makazi ya kila pepo mchafu,
makazi ya kila ndege na kila mnyama achukizaye.
3 Kwa maana mataifa yote yamekunywa
mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.
Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi nao,
nao wafanyabiashara wa dunia
wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.”
4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema:
“Tokeni katikati yake, enyi watu wangu,
ili msije mkashiriki dhambi zake,
ili msije mkapatwa na pigo lake lolote;
5 kwa kuwa dhambi zake zimelundikana hadi mbinguni,
naye Mungu ameukumbuka uhalifu wake.
6 Mtendee kama yeye alivyotenda;
umlipe mara mbili kwa ajili ya yale aliyotenda.
Katika kikombe chake mchanganyie
mara mbili ya kile alichochanganya.
7 Mpatie mateso na huzuni nyingi sawa na
utukufu na anasa alizojipatia.
Kwa kuwa moyoni mwake hujivuna, akisema,
‘Mimi ninatawala kama malkia;
mimi si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.’
8 Kwa hiyo mapigo yatampata kwa siku moja:
mauti, maombolezo na njaa.
Naye atateketezwa kwa moto,
kwa maana Bwana Mungu amhukumuye ana nguvu.
9 “Wafalme wa dunia waliozini naye na kushiriki anasa zake watakapoona moshi wa kuungua kwake, watamlilia na kumwombolezea. 10 Kwa hofu kubwa ya mateso yake, watasimama mbali na kulia na wakisema:
“ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa,
ee Babeli mji wenye nguvu!
Hukumu yako imekuja katika saa moja!’
11 “Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumwomboleza kwa sababu hakuna anunuaye bidhaa zao tena: 12 Bidhaa za dhahabu, za fedha, za vito vya thamani na vya lulu, kitani safi, nguo za rangi ya zambarau, hariri, nguo nyekundu, aina zote za miti ya udi, na vifaa vyote vya pembe za ndovu, vifaa vyote vya miti yenye thamani kuliko yote, shaba, chuma na marmar, 13 bidhaa za mdalasini, vikolezi, za uvumba, manemane, na uvumba wenye harufu nzuri, za divai, na mafuta ya zeituni, za unga mzuri na ngano; ngʼombe na kondoo; farasi na magari; na miili na roho za wanadamu.
14 “Watasema, ‘Yale matunda ambayo roho yako iliyatamani yamekoma. Utajiri wako wote na fahari yako vimetoweka, wala haviwezi kupatikana tena kamwe!’ 15 Wale wafanyabiashara waliotajirika kwa bidhaa hizo kutoka kwake watasimama mbali naye kwa hofu kubwa ya mateso yanayompata. Watalia na kuomboleza wakipiga kelele wakisema:
16 “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa,
uliyekuwa umevikwa mavazi ya kitani safi,
ya rangi ya zambarau na nyekundu,
ukimetameta kwa dhahabu,
vito vya thamani na lulu!
17 Katika muda wa saa moja utajiri wote mkubwa
kama huu umeangamia!’
“Kila nahodha, na wote wasafirio kwa meli, na wote wapatao kipato chao kutokana na bahari, watasimama mbali. 18 Watakapouona moshi wa kuungua kwake watalia wakisema, ‘Je, kulipata kuwako mji mkubwa kama huu?’ 19 Nao watajirushia mavumbi vichwani mwao, huku wakilia na kuomboleza, wakisema:
“ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa,
mji ambao wote wenye meli baharini
walitajirika kupitia kwa mali zake!
Katika saa moja tu ameangamizwa!
20 Furahia kwa ajili yake, ee mbingu!
Furahini watakatifu, mitume na manabii!
Mungu amemhukumu
kwa vile alivyowatendea ninyi.’ ”
21 Kisha malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe kubwa kama la kusagia akalitupa baharini akisema:
“Hivyo ndivyo mji mkubwa Babeli
utakavyotupwa chini kwa nguvu
wala hautaonekana tena.
22 Nyimbo za wapiga vinubi na waimbaji,
wapiga filimbi na wapiga tarumbeta
kamwe hazitasikika tena ndani yako.
Ndani yako kamwe hataonekana tena fundi
mwenye ujuzi wa aina yoyote.
Wala sauti ya jiwe la kusagia
kamwe haitasikika tena.
23 Mwanga wa taa
hautaangaza ndani yako tena.
Sauti ya bwana arusi na bibi arusi
kamwe haitasikika ndani yako tena.
Wafanyabiashara wako walikuwa watu maarufu wa dunia.
Mataifa yote yalipotoshwa kwa uchawi wako.
24 Ndani yake ilionekana damu ya manabii na ya watakatifu
na wote waliouawa duniani.”