Yerusalemu Mpya na paradiso Mpya
Furaha ya kiroho ya kanisa la mbinguni, lililokusanywa kutoka kwa wanadamu wote, inaonyeshwa zaidi kwa ishara za Yerusalemu Mpya na paradiso nyingine, mifano inayojulikana sana ya hali ya mbinguni katika vipindi viwili vya awali vya mpango wa Mungu.
96 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
9 Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba ya hayo mapigo saba ya mwisho akaja akaniambia, “Njoo, nami nitakuonyesha bibi arusi, yaani, mke wa Mwana-Kondoo.” 10 Naye akanichukua katika Roho hadi kwenye mlima mkubwa na mrefu, akanionyesha ule Mji Mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu. 11 Ulikuwa ukingʼaa kwa utukufu wa Mungu kama kito chenye thamani sana, kama yaspi, safi kama kioo. 12 Ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mawili, pakiwa na malaika kumi na wawili kwenye hayo malango. Kwenye malango hayo yaliandikwa majina ya yale makabila kumi na mawili ya Israeli. 13 Kulikuwa na malango matatu upande wa mashariki, matatu upande wa kaskazini, matatu upande wa kusini na matatu upande wa magharibi. 14 Ukuta wa huo mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na juu yake yaliandikwa majina ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.
15 Huyo malaika aliyesema nami alikuwa na ufito wa dhahabu wa kupimia huo mji, malango yake na kuta zake. 16 Mji huo ulikuwa mraba, urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Akaupima huo mji kwa huo ufito akakuta una kama kilomita 2,200; urefu wake na upana wake na kwenda juu kwake vilikuwa sawa. 17 Akaupima ukuta wake, ulikuwa na unene wa dhiraa 144 kwa kipimo cha kibinadamu ambacho huyo malaika alikuwa akikitumia. 18 Ukuta huo ulijengwa kwa yaspi hali mji wenyewe ulijengwa kwa dhahabu safi, ikingʼaa kama kioo. 19 Misingi ya kuta za mji huo zilipambwa kwa kila aina ya kito cha thamani. Msingi wa kwanza ulikuwa wa yaspi, wa pili yakuti samawi, wa tatu kalkedoni, wa nne zumaridi, 20 wa tano sardoniki, wa sita akiki, wa saba krisolitho, wa nane zabarajadi, wa tisa yakuti manjano, wa kumi krisopraso, wa kumi na moja hiakintho, wa kumi na mbili amethisto. 21 Yale malango kumi na mbili yalikuwa ni lulu kumi na mbili, kila lango lilikuwa limetengenezwa kwa lulu moja. Barabara kuu ya mji huo ilikuwa ya dhahabu safi ingʼaayo kama kioo.
22 Sikuona Hekalu ndani ya huo mji kwa sababu Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo ndio hekalu lake. 23 Ule mji hauhitaji jua wala mwezi kuuangazia, kwa sababu utukufu wa Mungu ndio nuru yake na Mwana-Kondoo ndiye taa yake. 24 Mataifa yatatembea yakiangaziwa na nuru yake na wafalme wa duniani wataleta fahari yao ndani yake. 25 Malango yake hayatafungwa kamwe, kwa maana hakutakuwa na usiku humo. 26 Utukufu na heshima za mataifa zitaletwa humo. 27 Lakini kitu kichafu hakitaingia humo kamwe, wala mtu yeyote atendaye mambo ya aibu au ya udanganyifu. Bali watakaoingia humo ni wale tu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.
22:1 Kisha yule malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, maangavu kama kioo yakitiririka kutoka kwenye kile kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo, 2 kupitia katikati ya barabara kuu ya huo mji. Kwenye kila upande wa huo mto kulikuwa na mti wa uzima utoao matunda ya aina kumi na mbili, ukizaa matunda yake kila mwezi. Nayo majani ya mti huo ni kwa ajili ya uponyaji wa mataifa. 3 Katika mji huo hakutakuwa tena na laana, bali kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo humo na watumishi wake watamtumikia, 4 nao watamwona uso wake na Jina lake litakuwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, kwa maana Bwana Mungu atakuwa nuru yao, nao watatawala milele na milele.
6 Kisha yule malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kuaminika na kweli. Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumishi wake yale ambayo hayana budi kutukia upesi.”
7 “Tazama, naja upesi! Amebarikiwa yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.”
8 Mimi, Yohana, ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Nami nilipokwisha kuyasikia na kuyaona, nilianguka chini nikasujudu miguuni pa yule malaika aliyekuwa akinionyesha mambo hayo. 9 Lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi ni mtumishi pamoja nawe na ndugu zako manabii na wote wanaoyashika maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu!”
Maneno ya Unabii Hayapaswi Kutiwa Muhuri
Kristo anatangaza kwamba maneno ya unabii wa Ufunuo hayapaswi kutiwa muhuri, kwa kuwa yamekusudiwa kuwapa wanadamu wote maarifa na kuwaboresha.
10 Kisha akaniambia, “Usiyafunge maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, kwa sababu wakati umekaribia. 11 Atendaye mabaya na aendelee kutenda mabaya, aliye mchafu na aendelee kuwa mchafu, yeye atendaye haki na aendelee kutenda haki, na yeye aliye mtakatifu na aendelee kuwa mtakatifu.”
12 “Tazama, naja upesi! Thawabu yangu i mkononi mwangu, nami nitampa kila mtu sawasawa na alivyotenda. 13 Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.
14 “Wamebarikiwa wale wafuao mavazi yao, ili wapate haki ya kuuendea huo mti wa uzima na kuuingia huo mji kupitia kwenye malango yake. 15 Huko nje wako mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu, na kila mtu apendaye udanganyifu na kuufanya.
Wito wa Mwisho wa Kristo kwa Ulimwengu
Kristo sasa anatoa wito wake wa mwisho kwa ulimwengu kupitia Roho wa unabii. Anatangaza tena uungu wake na ubinadamu wake, anawaalika wanadamu wote kuingia katika kanisa la Wakristo, anawaamuru wayafanye Maandiko kuwa mwongozo wao, na anatangaza kurudi kwake.
16 “Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kushuhudia mambo haya kwa ajili ya makanisa. Mimi ndimi Shina na Mzao wa Daudi, ile Nyota ya Asubuhi ingʼaayo.”
17 Roho na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Naye asikiaye na aseme, “Njoo!” Yeyote mwenye kiu na aje, na kila anayetaka na anywe maji ya uzima bure.
18 Namwonya kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki: Mtu yeyote akiongeza humo chochote, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. 19 Kama mtu yeyote akipunguza humo chochote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
20 Yeye anayeshuhudia mambo haya asema, “Hakika, naja upesi!”
Amen. Njoo, Bwana Yesu.
Yohana Anatamani Sana Kuja kwa Kristo
Yohana anamalizia Ufunuo kwa shauku kubwa ya kuja kwa Kristo na sala ya kuomba baraka kwa makanisa.
21 Neema ya Bwana Yesu iwe na watakatifu wote. Amen.