Walawi Wanawekwa Wakfu

1490 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Hesabu 8

1 Bwana akamwambia Mose, 2 “Sema na Aroni umwambie, ‘Wakati utakapoziweka zile taa saba, zinatakiwa kuangaza eneo lililo mbele ya kinara cha taa.’ ”

3 Aroni akafanya hivyo; akaziweka zile taa ili zielekee mbele kwenye kinara cha taa, kama vile Bwana alivyomwamuru Mose. 4 Hivi ndivyo kinara cha taa kilivyotengenezwa: Kilitengenezwa kwa dhahabu iliyofuliwa, kuanzia kwenye kitako chake hadi kwenye maua yake. Kinara cha taa kilitengenezwa sawasawa kabisa na kielelezo ambacho Bwana alikuwa amemwonyesha Mose.

5 Bwana akamwambia Mose: 6 “Watwae Walawi kutoka miongoni mwa Waisraeli wengine na uwatakase kwa kawaida ya ibada. 7 Ili kuwatakasa fanya hivi: Nyunyizia maji ya utakaso juu yao; kisha uwaambie wanyoe nywele kwenye mwili mzima, wafue nguo zao na hivyo wajitakase wenyewe. 8 Waambie wamchukue fahali mchanga pamoja na sadaka yake ya nafaka ya unga laini uliochanganywa na mafuta; kisha utamchukua fahali mchanga wa pili kwa ajili ya sadaka ya dhambi. 9 Walete Walawi mbele ya Hema la Kukutania na ukusanye jumuiya yote ya Waisraeli. 10 Utawaleta Walawi mbele za Bwana, na Waisraeli wataweka mikono yao juu ya Walawi. 11 Aroni atawaweka Walawi mbele za Bwana kama sadaka ya kuinua kutoka kwa Waisraeli, ili kwamba wawe tayari kuifanya kazi ya Bwana.

12 “Baada ya Walawi kuweka mikono yao juu ya vichwa vya hao mafahali wawili, tumia mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi kwa Bwana, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Walawi. 13 Waambie hao Walawi wasimame mbele ya Aroni na wanawe, kisha wawatoe kama sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana. 14 Kwa njia hii utakuwa umewatenga Walawi kutoka kwa Waisraeli wengine, nao Walawi watakuwa wangu.

15 “Utakapokuwa umekwisha kuwatakasa Walawi na kuwatoa kama sadaka ya kuinuliwa, watakuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania. 16 Wao ndio Waisraeli ambao watatolewa kabisa kwangu. Nimewatwaa kama mali yangu mwenyewe badala ya mzaliwa wa kwanza, mzaliwa wa kwanza wa kiume kutoka kwa kila mwanamke wa Kiisraeli. 17 Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume katika Israeli, awe wa mwanadamu au mnyama, ni wangu. Wakati nilipowaua wazaliwa wote wa kwanza huko Misri, niliwatenga kwa ajili yangu mwenyewe. 18 Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wote wa kwanza wa kiume katika Israeli. 19 Kati ya Waisraeli wote, nimempa Aroni na wanawe Walawi kama zawadi ili wafanye kazi katika Hema la Kukutania kwa niaba ya Waisraeli, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili pasiwepo na pigo lolote litakalowapata Waisraeli wakati watakapokaribia mahali patakatifu.”

20 Mose, Aroni na jumuiya yote ya Waisraeli wakawafanyia Walawi kama Bwana alivyomwamuru Mose. 21 Walawi wakajitakasa wenyewe na wakafua nguo zao. Kisha Aroni akawasogeza mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili kuwatakasa. 22 Baada ya hayo, Walawi walikuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania chini ya usimamizi wa Aroni na wanawe. Waliwafanyia Walawi kama vile Bwana alivyomwamuru Mose.

23 Bwana akamwambia Mose, 24 “Hili linawahusu Walawi: Wanaume wenye umri wa miaka ishirini na mitano au zaidi watakuja kushiriki katika kazi kwenye Hema la Kukutania, 25 lakini watakapofika umri wa miaka hamsini, ni lazima waache kazi zao za kawaida wala wasiendelee. 26 Wanaweza kuwasaidia ndugu zao kufanya wajibu wao katika Hema la Kukutania, lakini wao wenyewe kamwe hawatafanya hiyo kazi. Basi, hivi ndivyo utakavyogawa wajibu kwa Walawi.”

Matumizi ya Tarumbeta za Fedha

Hesabu 10:1–10

1 Bwana akamwambia Mose: 2 “Tengeneza tarumbeta mbili za fedha ya kufua, uzitumie kwa kuita jumuiya pamoja na wakati wa kuvunja makambi ili kuondoka. 3 Tarumbeta zote mbili zikipigwa, jumuiya yote itakusanyika mbele yako katika ingilio la Hema la Kukutania. 4 Kama tarumbeta moja tu ikipigwa, viongozi, yaani wakuu wa koo za Israeli, ndio watakaokusanyika mbele yako. 5 Wakati mlio wa kujulisha hatari ukipigwa, makabila yaliyo na makambi upande wa mashariki yataondoka. 6 Ukisikika mlio wa pili wa jinsi hiyo, walioko kwenye makambi ya kusini wataondoka. Mlio huo wa kujulisha hatari utakuwa ishara ya kuondoka. 7 Ili kukusanya kusanyiko, piga tarumbeta zote, lakini siyo kwa mlio wa kujulisha hatari.

8 “Wana wa Aroni, makuhani, ndio watakaopiga hizo tarumbeta. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu na kwa vizazi vijavyo. 9 Wakati mtakapopigana vita katika nchi yenu wenyewe dhidi ya adui anayewaonea, piga tarumbeta kwa mlio wa kujulisha hatari. Ndipo utakumbukwa na Bwana Mungu wenu na kuokolewa kutoka kwa adui zenu. 10 Pia nyakati za furaha yenu, yaani sikukuu zenu zilizoamriwa na sikukuu za Mwezi Mwandamo, mtapiga tarumbeta juu ya sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za amani, nazo zitakuwa ukumbusho kwa ajili yenu mbele za Mungu wenu. Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”

Jinsi Wingu Lilivyowaongoza Watu

Hesabu 9:15–23

15 Katika siku hiyo ambayo Maskani, Hema la Ushuhuda, iliposimamishwa, wingu liliifunika. Kuanzia jioni mpaka asubuhi wingu lililokuwa juu ya Maskani lilionekana kama moto. 16 Hivyo ndivyo lilivyoendelea kuwa; wingu liliifunika wakati wa mchana, na usiku lilionekana kama moto. 17 Wakati wowote wingu lilipoinuka kutoka juu ya Hema, nao Waisraeli waliondoka; mahali popote wingu liliposimama, Waisraeli walipiga kambi. 18 Kwa amri ya Bwana Waisraeli waliondoka, na kwa amri yake walipiga kambi. Kwa muda wote wingu liliposimama juu ya Maskani, Waisraeli walibaki wamepiga kambi.

19 Wakati wingu lilipobaki juu ya Maskani kwa muda mrefu, Waisraeli walitii amri ya Bwana nao hawakuondoka. 20 Wakati mwingine wingu lilikuwa juu ya Maskani kwa siku chache tu; kwa amri ya Bwana wangelipiga kambi na kisha kwa amri yake wangeliondoka. 21 Wakati mwingine wingu lilikuwepo kuanzia jioni mpaka asubuhi tu, na lilipoinuka asubuhi, nao waliondoka. Ikiwa ni mchana au usiku, wakati wowote wingu lilipoinuka, waliondoka. 22 Ikiwa wingu lilikaa juu ya Maskani kwa siku mbili au mwezi au mwaka, Waisraeli wangebaki wamepiga kambi na hawakuondoka; lakini lilipoinuka, wangeondoka.

23 Kwa amri ya Bwana walipiga kambi, na kwa amri ya Bwana waliondoka. Walitii amri ya Bwana, kufuatana na agizo lake kupitia Mose.