Kuwasili kwa Yethro
1490 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Basi Yethro, kuhani wa Midiani, baba mkwe wa Mose, akawa amesikia kila kitu Mungu alichomfanyia Mose na watu wake wa Israeli, pia jinsi Bwana alivyowatoa Israeli Misri.
2 Baada ya Mose kumrudisha mkewe Sipora, Yethro baba mkwe wake alimpokea 3 pamoja na wanawe wawili. Jina la mmoja aliitwa Gershomu, kwa kuwa Mose alisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.” 4 Mwingine aliitwa Eliezeri, kwa kuwa alisema, “Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa kutoka upanga wa Farao.”
5 Yethro, baba mkwe wa Mose, pamoja na wana wawili wa Mose na mkewe, wakamjia Mose huko jangwani, mahali alipokuwa amepiga kambi karibu na mlima wa Mungu. 6 Yethro alikuwa ametuma ujumbe kwake Mose, kusema, “Mimi Yethro baba mkwe wako ninakuja kwako pamoja na mke wako na wanao wawili.”
7 Kwa hiyo Mose akatoka kumlaki baba mkwe wake, akainama na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia hemani. 8 Mose akamwambia baba mkwe wake kuhusu kila kitu Bwana alichomfanyia Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na pia kuhusu shida zote walizokutana nazo njiani na jinsi Bwana alivyowaokoa.
9 Yethro akafurahishwa sana kusikia juu ya mambo yote mazuri Bwana aliyowatendea Waisraeli kuwaokoa kutoka mkono wa Wamisri. 10 Yethro akasema, “Sifa na ziwe kwa Bwana, aliyekuokoa wewe kutoka mikononi mwa Wamisri na Farao, na aliyewaokoa watu kutoka mikononi mwa Wamisri. 11 Sasa najua ya kuwa Bwana ni mkuu kuliko miungu mingine yote, kwa kuwa amewatendea hivi wale waliowatenda Israeli kwa ujeuri.” 12 Kisha Yethro, baba mkwe wa Mose, akaleta sadaka ya kuteketezwa na dhabihu nyingine kwa Mungu, naye Aroni pamoja na wazee wote wa Israeli wakaja kula chakula pamoja na baba mkwe wa Mose mbele za Mungu.
13 Siku iliyofuata, Mose akachukua nafasi yake kama hakimu wa watu, nao wakasimama kumzunguka kuanzia asubuhi hadi jioni. 14 Baba mkwe wake alipoona yote Mose anayowafanyia watu, akasema, “Ni nini hiki unachowafanyia watu? Kwa nini wewe unakuwa mwamuzi wa watu hawa peke yako, wakati watu hawa wamesimama wakikuzunguka tangu asubuhi mpaka jioni?”
15 Mose akamjibu, “Kwa sababu watu wananijia kutaka mapenzi ya Mungu. 16 Kila wakiwa na shauri huletwa kwangu, nami huamua kati ya mtu na mwenzake na kuwajulisha juu ya amri na sheria za Mungu.”
17 Baba mkwe wa Mose akamjibu, “Unachofanya sio kizuri. 18 Wewe pamoja na watu hawa wanaokujia mtajichosha bure. Kazi ni nzito sana kwako, huwezi kuibeba mwenyewe. 19 Sasa nisikilize mimi, nitakupa shauri, naye Mungu na awe pamoja nawe. Yapasa wewe uwe mwakilishi wa watu mbele za Mungu na ulete mashauri yao kwake. 20 Uwafundishe amri na sheria, tena uwaonyeshe namna ya kuishi na kazi zinazowapasa wao kufanya. 21 Lakini uchague watu wenye uwezo miongoni mwa watu wote, watu wanaomwogopa Mungu, watu waaminifu wanaochukia mali ya dhuluma, uwateuwe wawe maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi. 22 Waweke wawe waamuzi wa watu kwa wakati wote, lakini waambie wakuletee kila shauri lililo gumu; yale yaliyo rahisi wayaamue wao wenyewe. Hii itafanya mzigo wako kuwa mwepesi, kwa sababu watashirikiana nawe. 23 Kama ukifanya hivi, na ikiwa Mungu ameagiza hivyo, utaweza kushinda uchovu, nao watu hawa wote watarudi nyumbani wameridhika.”
24 Mose akamsikiliza baba mkwe wake na kufanya kila kitu alichosema. 25 Mose akawachagua watu wenye uwezo kutoka Israeli yote, akawafanya kuwa viongozi wa watu, maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi. 26 Wakatumika kama waamuzi wa watu kwa wakati wote. Mashauri magumu wakayaleta kwa Mose, lakini yale yaliyo rahisi wakayaamua wenyewe.
Safari ya Kumi na Mbili: Kutoka Sinai hadi Kibroth-Hataava
16 Wakaondoka katika Jangwa la Sinai na kupiga kambi huko Kibroth-Hataava.
Mpangilio wa Msafara
11 Katika siku ya ishirini ya mwezi wa pili wa mwaka wa pili, wingu liliinuka kutoka juu ya maskani ya Ushuhuda. 12 Ndipo Waisraeli wakaondoka kutoka Jangwa la Sinai wakasafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine mpaka wingu lilipotua katika Jangwa la Parani. 13 Waliondoka kwa mara ya kwanza kwa agizo la Bwana kupitia kwa Mose.
14 Vikosi vya kambi ya Yuda vilitangulia kwanza chini ya alama yao. Nashoni mwana wa Aminadabu alikuwa kiongozi wao. 15 Nethaneli mwana wa Suari alikuwa kiongozi wa kabila la Isakari, 16 naye Eliabu mwana wa Heloni alikuwa kiongozi wa kabila la Zabuloni. 17 Ndipo Maskani iliposhushwa, nao wana wa Gershoni na wana wa Merari ambao waliibeba wakaondoka.
18 Vikosi vya kambi ya Reubeni vilifuata, chini ya alama yao. Elisuri mwana wa Shedeuri alikuwa kiongozi wao. 19 Shelumieli mwana wa Surishadai aliongoza kikosi cha kabila la Simeoni, 20 naye Eliasafu mwana wa Deueli aliongoza kikosi cha kabila la Gadi. 21 Kisha Wakohathi wakaondoka, wakichukua vitu vitakatifu. Maskani ilikuwa isimamishwe kabla wao hawajafika.
22 Vikosi vya kambi ya Efraimu vilifuata, chini ya alama yao. Elishama mwana wa Amihudi alikuwa kiongozi wao. 23 Gamalieli mwana wa Pedasuri aliongoza kikosi cha kabila la Manase, 24 naye Abidani mwana wa Gideoni alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Benyamini.
25 Mwishowe, kama kikosi cha nyuma cha ulinzi wa vikosi vyote, vikosi vya kambi ya Dani viliondoka chini ya alama yao. Ahiezeri mwana wa Amishadai alikuwa kiongozi wao. 26 Pagieli mwana wa Okrani aliongoza kikosi cha kabila la Asheri, 27 naye Ahira mwana wa Enani aliongoza kikosi cha kabila la Naftali. 28 Huu ndio ulikuwa utaratibu wa kuondoka wa vikosi vya Waisraeli walipokuwa wanaondoka.