Nchi Inagawanywa

1444 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yoshua 14:1–5

1 Basi haya ndiyo maeneo Waisraeli waliyopokea kama urithi katika nchi ya Kanaani, ambayo kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni na viongozi wa koo za kabila za Israeli waliwagawia. 2 Urithi wao uligawanywa kwa kura kwa yale makabila tisa na nusu, kama Bwana alivyoamuru Mose. 3 Mose alikuwa amewapa yale makabila mawili na nusu urithi wao upande wa mashariki mwa Yordani, lakini Walawi hawakupewa urithi miongoni mwa hao wengine, 4 kwa kuwa wana wa Yosefu walikuwa makabila mawili; Manase na Efraimu. Walawi hawakupata mgawo wa ardhi, bali walipewa miji tu kwa ajili ya kuishi, pamoja na maeneo ya malisho kwa ajili ya makundi yao ya kondoo, mbuzi na ngʼombe wao. 5 Kwa hiyo Waisraeli wakagawana ile nchi, kama vile Bwana alivyomwagiza Mose.

Urithi wa Makabila Mawili na Nusu

Yoshua 13:15–33

15 Haya ndiyo maeneo ambayo Mose alikuwa amewapa kabila la Reubeni ukoo kwa ukoo:

16 Eneo la Aroeri lililo ukingoni mwa Bonde la Arnoni, na kuanzia mji ulio katikati ya bonde, pia uwanda wote wa juu kupita Medeba 17 hadi Heshboni na miji yake yote kwenye uwanda wa juu, ikijumlishwa miji ya Diboni, Bamoth-Baali, Beth-Baal-Meoni, 18 Yahasa, Kedemothi, Mefaathi, 19 Kiriathaimu, Sibma, Sereth-Shahari juu ya kilima kilicho katika bonde, 20 Beth-Peori, materemko ya Pisga na Beth-Yeshimothi: 21 miji yote ya uwanda wa juu na eneo lote la utawala wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala katika Heshboni. Mose alikuwa amemshinda Sihoni, pia watawala wakuu wa Wamidiani, ambao ni Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba, waliokuwa wameungana na Sihoni, ambao waliishi katika nchi ile. 22 Pamoja na wale waliouawa katika vita, Waisraeli walikuwa wamemuua kwa upanga Balaamu mwana wa Beori aliyekuwa mchawi. 23 Mpaka wa Wareubeni ulikuwa ni ukingo wa Mto Yordani. Miji hii na vijiji vyake ndiyo iliyokuwa urithi wa Wareubeni ukoo kwa ukoo.

24 Haya ndiyo maeneo ambayo Mose alikuwa amewapa kabila la Gadi, ukoo kwa ukoo:

25 Nchi ya Yazeri, miji yote ya Gileadi na nusu ya nchi ya Amoni iliyoenea hadi Aroeri, karibu na Raba; 26 na kuanzia Heshboni mpaka Ramath-Mispa na Betonimu, na kutoka Mahanaimu hadi eneo la Debiri; 27 na katika bonde, Beth-Haramu, Beth-Nimra, Sukothi na Safoni na sehemu iliyobaki ya eneo la utawala wa Sihoni mfalme wa Heshboni (upande wa mashariki mwa Mto Yordani, eneo inayoishia kwenye Bahari ya Kinerethi). 28 Miji hii na vijiji vyake ilikuwa urithi wa kabila la Gadi ukoo kwa ukoo.

29 Haya ndiyo maeneo ambayo Mose alikuwa amewapa hiyo nusu ya kabila la Manase, yaani kwa nusu ya jamaa ya uzao wa Manase, ukoo kwa ukoo:

30 Eneo lililoenea kuanzia Mahanaimu, na kujumlisha Bashani yote, ufalme wote wa Ogu mfalme wa Bashani, makazi yote ya Yairi huko Bashani, miji sitini, 31 nusu ya Gileadi, na Ashtarothi na Edrei (miji ya kifalme ya Ogu katika Bashani). Hii ilikuwa kwa ajili ya wazao wa Makiri mwana wa Manase, kwa ajili ya nusu ya wana wa Makiri, ukoo kwa ukoo.

32 Huu ndio urithi alioupeana Mose wakati alipokuwa katika tambarare za Moabu, ngʼambo ya Yordani mashariki mwa Yeriko. 33 Lakini kwa kabila la Walawi, Mose hakuwapa urithi; Bwana Mungu, Mungu wa Israeli ndiye urithi wao, kama alivyowaahidi.

Urithi wa Kalebu

Yoshua 14:6–15

6 Kisha watu wa Yuda wakamwendea Yoshua huko Gilgali, naye Kalebu mwana wa Yefune yule Mkenizi, akamwambia, “Unajua jambo ambalo Bwana alimwambia Mose mtu wa Mungu huko Kadesh-Barnea kukuhusu wewe na mimi. 7 Nilikuwa na umri wa miaka arobaini, wakati Mose mtumishi wa Bwana, aliponituma kutoka Kadesh-Barnea kuipeleleza hiyo nchi. Nami nikamletea taarifa kama kulingana na nilivyosadiki moyoni. 8 Lakini ndugu zangu tuliopanda nao waliifanya mioyo ya watu iyeyuke kwa hofu. Bali mimi, nilimfuata Bwana Mungu wangu kwa moyo wote. 9 Hivyo katika siku ile, Mose akaniapia, ‘Nchi ambayo umeikanyaga kwa miguu yako itakuwa urithi wako na wa watoto wako milele, kwa sababu umemfuata Bwana Mungu wangu kwa moyo wote.’

10 “Sasa basi, kama vile Bwana alivyoahidi, ameniweka hai kwa miaka arobaini na mitano tangu wakati alipomwambia Mose jambo hili, wakati Waisraeli wakiwa wanazunguka jangwani. Hivyo mimi hapa leo, nina umri wa miaka themanini na mitano! 11 Bado ninazo nguvu kama siku ile Mose aliponituma. Bado ninazo nguvu za kwenda vitani sasa kama vile nilivyokuwa wakati ule. 12 Basi nipe nchi hii ya vilima, ambayo Bwana aliniahidi siku ile. Wewe mwenyewe ulisikia wakati ule kwamba Waanaki walikuwako huko na miji yao ilikuwa mikubwa na yenye maboma, lakini, kwa msaada wa Bwana, nitawafukuza watoke huko kama vile alivyonena.”

13 Ndipo Yoshua akambariki Kalebu mwana wa Yefune, na akampa Hebroni kama urithi wake. 14 Hivyo Hebroni imekuwa mali ya Kalebu mwana wa Yefune Mkenizi tangu wakati ule, kwa sababu alimwandama Bwana, Mungu wa Israeli, kwa moyo wote. 15 (Hebroni uliitwa Kiriath-Arba hapo mwanzo, kutokana na huyo Arba ambaye alikuwa mtu mkuu kupita wote miongoni mwa Waanaki.)

Kisha nchi ikawa na amani bila vita.

Yoshua 15:13–19

13 Kwa kufuata maagizo ya Bwana kwake, Yoshua alimpa Kalebu mwana wa Yefune sehemu katika Yuda: Kiriath-Arba, yaani Hebroni (Arba alikuwa baba wa zamani wa Anaki). 14 Kutoka Hebroni Kalebu alifukuza hao wana watatu wa Anaki, nao ni Sheshai, Ahimani na Talmai, wazao wa Anaki. 15 Kutoka hapo akaondoka kupigana dhidi ya watu walioishi Debiri (jina la Debiri hapo kwanza uliitwa Kiriath-Seferi). 16 Kalebu akasema, “Nitamwoza binti yangu Aksa kwa mtu atakayeweza kupigana na kuteka Kiriath-Seferi.” 17 Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu yake Kalebu, akauteka; hivyo Kalebu akamtoa Aksa binti yake aolewe naye.

18 Siku moja Aksa alipokuja kwa Othnieli, alimsihi Othnieli amwombe baba yake, Kalebu, shamba. Aksa aliposhuka kutoka juu ya punda wake, Kalebu akamuuliza, “Je, wataka nikufanyie nini?”

19 Akamjibu, “Naomba unifanyie jambo moja la hisani. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Basi Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.