Sehemu ya 2: Mgawanyo wa Jumla wa Nchi

Muhtasari wa Ushindi

1444 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yoshua 12:1–13:14

1 Hawa ndio wafalme wa nchi ambao Waisraeli waliwashinda na kuitwaa nchi yao upande wa mashariki mwa Yordani, kuanzia Bonde la Arnoni mpaka Mlima Hermoni, pamoja na eneo lote la upande wa mashariki ya Araba:

2 Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala huko Heshboni.

Alitawala kuanzia Aroeri kwenye ukingo wa Bonde la Arnoni, kuanzia katikati ya bonde, hadi kwenye Mto Yaboki, ambao ni mpaka wa Waamoni. Hii ilijumlisha nusu ya Gileadi. 3 Pia alitawala Araba ya mashariki kuanzia Bahari ya Kinerethi hadi Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), hadi Beth-Yeshimothi, kisha kuelekea kusini chini ya materemko ya Pisga.

4 Nayo nchi ya Ogu mfalme wa Bashani, aliyekuwa mmoja wa mabaki ya Warefai, aliyetawala Ashtarothi na Edrei.

5 Naye alitawala katika Mlima Hermoni, Saleka, Bashani yote hadi mpaka wa watu wa Geshuri, na watu wa Maaka na nusu ya Gileadi, hadi kwenye mpaka wa Sihoni mfalme wa Heshboni.

6 Mose, mtumishi wa Bwana, na Waisraeli wakawashinda. Naye Mose mtumishi wa Bwana akawapa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase nchi ya hao wafalme ili iwe milki yao.

7 Hawa ndio wafalme wa nchi ambao Yoshua na Waisraeli waliwashinda upande wa magharibi mwa Yordani, kuanzia Baal-Gadi katika Bonde la Lebanoni hadi kufikia Mlima Halaki, unaoinuka ukielekea Seiri. (Yoshua alitoa nchi zao kwa makabila ya Israeli iwe urithi wao sawasawa na mgawanyiko wa makabila yao: 8 nchi ya vilima, shefela, upande wa magharibi, Araba, materemko ya milima, jangwa, na Negebu; nchi za Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi):

9 mfalme wa Yeriko mmoja

mfalme wa Ai (karibu na Betheli) mmoja

10 mfalme wa Yerusalemu mmoja

mfalme wa Hebroni mmoja

11 mfalme wa Yarmuthi mmoja

mfalme wa Lakishi mmoja

12 mfalme wa Egloni mmoja

mfalme wa Gezeri mmoja

13 mfalme wa Debiri mmoja

mfalme wa Gederi mmoja

14 mfalme wa Horma mmoja

mfalme wa Aradi mmoja

15 mfalme wa Libna mmoja

mfalme wa Adulamu mmoja

16 mfalme wa Makeda mmoja

mfalme wa Betheli mmoja

17 mfalme wa Tapua mmoja

mfalme wa Heferi mmoja

18 mfalme wa Afeki mmoja

mfalme wa Lasharoni mmoja

19 mfalme wa Madoni mmoja

mfalme wa Hazori mmoja

20 mfalme wa Shimron-Meroni mmoja

mfalme wa Akishafu mmoja

21 mfalme wa Taanaki mmoja

mfalme wa Megido mmoja

22 mfalme wa Kedeshi mmoja

mfalme wa Yokneamu katika Karmeli mmoja

23 mfalme wa Dori (katika Nafoth-Dori) mmoja

mfalme wa Goimu katika Gilgali mmoja

24 mfalme wa Tirsa mmoja

wafalme jumla yao ilikuwa thelathini na mmoja.

13:1 Yoshua alipokuwa mzee na umri wake ukiwa umesogea sana, Bwana akamwambia, “Wewe ni mzee sana, na bado kumesalia sehemu kubwa sana za nchi ambazo ni za kutwaliwa.

2 “Nchi iliyosalia ni hii: maeneo yote ya Wafilisti na Wageshuri: 3 kutoka Mto Shihori ulioko mashariki mwa Misri, kuelekea kaskazini kwenye eneo la Ekroni, ambayo yote ilihesabika kama ya Wakanaani (maeneo yale matano ya watawala wa Kifilisti, ambayo ni Gaza, Ashdodi, Ashkeloni, Gathi na Ekroni: ndiyo nchi ya Waavi); 4 kuanzia kusini, nchi yote ya Wakanaani, kuanzia Ara ambayo ni ya Wasidoni, ikienea hadi Afeki, na eneo la Waamori, 5 eneo la Wagebali; Lebanoni yote kuelekea mashariki, kuanzia Baal-Gadi chini ya Mlima Hermoni hadi Lebo-Hamathi.

6 “Na kuhusu wakaaji wote katika maeneo ya milima, kuanzia Lebanoni hadi Misrefoth-Maimu, pamoja na eneo lote la Wasidoni, mimi mwenyewe nitawafukuza watoke mbele ya Waisraeli. Hakikisha umegawa nchi hii kwa Israeli kuwa urithi, kama nilivyokuagiza, 7 sasa basi, ligawanye eneo hili kwa yale makabila tisa na ile nusu ya kabila la Manase kuwa urithi.”

8 Ile nusu nyingine ya Manase, Wareubeni na Wagadi, walishapokea urithi Mose aliokuwa amewapa mashariki mwa Yordani, sawasawa na mtumishi wa Bwana alivyowagawia.

9 Eneo lao lilienea toka Aroeri, iliyoko ukingoni mwa Bonde la Arnoni kuanzia mji ulio katikati ya bonde, likijumlisha nchi ya uwanda wa juu wote wa Medeba mpaka Diboni, 10 nayo miji yote ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala Heshboni, hadi mpakani mwa Waamoni. 11 Vilevile ilijumlisha Gileadi, eneo la Wageshuri na Wamaaka, mlima wote wa Hermoni na Bashani yote ikienea hadi Saleka: 12 yaani ufalme wote wa Ogu katika Bashani, aliyekuwa ametawala katika Ashtarothi na Edrei, na ndiye pekee alisalia kwa Warefai. Mose alikuwa amewashinda na kuteka nchi yao. 13 Lakini Waisraeli hawakuwafukuza watu wa Geshuri na wa Maaka, kwa hiyo wanaendelea kuishi miongoni mwa Waisraeli mpaka leo hii.

14 Lakini kwa kabila la Lawi, Mose hakupeana urithi, kwa kuwa sadaka za kuteketezwa kwa moto zilizotolewa kwa Bwana, Mungu wa Israeli, ndizo zilizokuwa urithi wao, kama alivyowaahidi.