Kusanyiko la Kwanza la Watu

1015 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Nyakati 23:1

1 Daudi alipokuwa mzee aliyeshiba siku, akamfanya Solomoni mwanawe kuwa mfalme juu ya Israeli.

1 Nyakati 28:1–10

1 Daudi akawaita maafisa wote wa Israeli wakusanyike huko Yerusalemu: yaani, maafisa walio juu ya makabila, majemadari wa vikosi katika utumishi wa mfalme, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, maafisa wanaosimamia mali zote na mifugo ya mfalme na wanawe, wakiwemo maafisa wa jumba la kifalme, mashujaa na askari wote walio hodari.

2 Mfalme Daudi akainuka na kusema: “Nisikilizeni ndugu zangu nanyi watu wangu. Nilikuwa na nia ya kujenga nyumba ili iwe mahali pa kukaa Sanduku la Agano la Bwana kwa ajili ya kuwa mahali pa kuwekea miguu ya Mungu wetu, nami nikafanya maandalizi ya kuijenga. 3 Lakini Mungu akaniambia, ‘Wewe hutajenga nyumba kwa Jina langu, kwa sababu wewe umepigana vita na umemwaga damu.’

4 “Hata hivyo, Bwana, Mungu wa Israeli, alinichagua mimi kutoka jamaa yangu yote niwe mfalme juu ya Israeli milele. Alimchagua Yuda kuwa kiongozi na kutoka nyumba ya Yuda akaichagua jamaa yangu na kutoka wana wa baba yangu ikampendeza kunifanya niwe mfalme juu ya Israeli yote. 5 Miongoni mwa wanangu wote, naye Bwana amenipa wengi, amemchagua Solomoni mwanangu ili kukikalia kiti cha enzi cha ufalme wa Bwana juu ya Israeli. 6 Aliniambia, ‘Solomoni mwanao ndiye atakayejenga nyumba yangu na nyua zangu, kwa maana nimemchagua yeye kuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake. 7 Nitaufanya imara ufalme wake milele kama akiendelea kuzishika amri zangu na sheria zangu, kama afanyavyo hivi leo.’

8 “Hivyo basi ninawaagiza mbele za Israeli yote na kusanyiko hili la Bwana naye Mungu wetu akiwa anasikia: Kuweni na bidii kuzifuata amri za Bwana Mungu wenu, ili mpate kumiliki nchi hii nzuri na kuwaachia wana wenu kuwa urithi milele.

9 “Nawe Solomoni mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa kujitoa kwa moyo wote na kwa nia ya kumkubali, kwa maana Bwana huuchunguza kila moyo na kujua kila kusudi la kila fikira. Ukimtafuta, ataonekana kwako; bali kama ukimwacha, yeye atakukataa milele. 10 Angalia basi, kwa maana Bwana amekuchagua wewe ili ujenge Hekalu kuwa mahali patakatifu. Uwe hodari ukafanye kazi hiyo.”

Zaburi 91

1 Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana,

atadumu katika uvuli wake Mwenyezi.

2 Nitasema kumhusu Bwana, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu,

Mungu wangu, ambaye ninamtumaini.”

3 Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji,

na maradhi ya kuambukiza ya kuua.

4 Atakufunika kwa manyoya yake,

chini ya mbawa zake utapata kimbilio,

uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako.

5 Hutaogopa vitisho vya usiku,

wala mshale urukao mchana,

6 wala maradhi ya kuambukiza

yanayonyemelea gizani,

wala tauni iharibuyo adhuhuri.

7 Ijapo watu elfu wataangukia kando yako,

kumi elfu mkono wako wa kuume,

lakini haitakukaribia wewe.

8 Utatazama tu kwa macho yako

na kuona adhabu ya waovu.

9 Kama ukimfanya Aliye Juu Sana kuwa makao yako:

naam, Bwana ambaye ni kimbilio langu,

10 basi hakuna madhara yatakayokupata wewe,

hakuna maafa yataikaribia hema yako.

11 Kwa kuwa atawaagiza malaika zake kwa ajili yako,

wakulinde katika njia zako zote.

12 Mikononi mwao watakuinua,

ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe.

13 Utawakanyaga simba na nyoka wakali,

simba mkubwa na nyoka utawaponda kwa miguu.

14 Bwana asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa;

nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu.

15 Ataniita, nami nitamjibu;

nitakuwa pamoja naye katika taabu,

nitamwokoa na kumheshimu.

16 Kwa siku nyingi nitamshibisha

na kumwonyesha wokovu wangu.”

Yaelekea ni Zaburi ya Miaka ya Mwisho ya Maisha ya Daudi

Zaburi 145

Wimbo wa Sifa. Wa Daudi.

1 Nitakutukuza wewe, Mungu wangu Mfalme,

nitalisifu jina lako milele na milele.

2 Kila siku nitakusifu

na kulitukuza jina lako milele na milele.

3 Bwana ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana,

ukuu wake haupimiki.

4 Kizazi kimoja kitasifia kazi zako kwa kizazi kingine,

watasimulia matendo yako makuu.

5 Watasema juu ya utukufu wa fahari ya ukuu wako,

nami nitatafakari juu ya kazi zako za ajabu.

6 Watasimulia uwezo wa kazi zako za kutisha,

nami nitatangaza matendo yako makuu.

7 Wataadhimisha wema wako mwingi,

na wataimba kwa shangwe juu ya haki yako.

8 Bwana ni mwenye neema na mwingi wa huruma,

si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo.

9 Bwana ni mwema kwa wote,

ana huruma kwa vyote alivyovifanya.

10 Ee Bwana, vyote ulivyovifanya vitakusifu,

watakatifu wako watakutukuza.

11 Watasimulia utukufu wa ufalme wako

na kusema juu ya ukuu wako,

12 ili watu wote wajue matendo yako makuu

na utukufu wa fahari ya ufalme wako.

13 Ufalme wako ni ufalme wa milele,

mamlaka yako hudumu vizazi vyote.

Bwana ni mwaminifu kwa ahadi zake zote

na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.

14 Bwana huwategemeza wote waangukao,

na huwainua wote waliolemewa na mizigo yao.

15 Macho yao wote yanakutazama wewe,

nawe huwapa chakula chao wakati wake.

16 Waufumbua mkono wako,

watosheleza haja ya kila kitu kilicho hai.

17 Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,

na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.

18 Bwana yu karibu na wote wamwitao,

karibu na wote wamwitao kwa uaminifu.

19 Huwatimizia wamchao matakwa yao,

husikia kilio chao na kuwaokoa.

20 Bwana huwalinda wote wampendao,

bali waovu wote atawaangamiza.

21 Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana.

Kila kiumbe na kilisifu jina lake takatifu

milele na milele.