Umoja na Ukarimu wa Kanisa la Mwanzo
30 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. 33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. 34 Wala hapakuwepo mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, 35 wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.
36 Yosefu, Mlawi kutoka Kipro, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake Mwana wa Faraja), 37 aliuza shamba alilokuwa nalo, akaleta hizo fedha alizopata na kuziweka miguuni pa mitume.
Kifo cha Anania na Safira
1 Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja. 2 Huku mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume.
3 Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? 4 Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.”
5 Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia. 6 Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakamchukua nje kumzika.
7 Saa tatu baadaye mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia. 8 Petro akamuuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.”
9 Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho wa Bwana? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakuchukua nje.”
10 Saa ile ile akaanguka chini miguuni mwake na kufa. Nao wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe.
Hali ya Kanisa Wakati Huu 31 BK
11 Hofu kuu ikalipata kanisa lote pamoja na watu wote waliosikia juu ya matukio haya.
13 Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu. 14 Hata hivyo, waliomwamini Bwana wakazidi kuongezeka, wanaume na wanawake.
12 Mitume wakafanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Walioamini wote walikuwa wakikusanyika katika ukumbi wa Solomoni.
15 Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao. 16 Pia watu wakakusanyika kutoka miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu. Hao wote wakaponywa.
Malaika Anawafungua Mitume Kutoka Gerezani 32 BK
17 Kisha kuhani mkuu na wenzake wote waliokuwa pamoja naye, waliokuwa wa kundi la Masadukayo, wakajawa na wivu. 18 Wakawakamata mitume na kuwatia gerezani. 19 Lakini wakati wa usiku, malaika wa Bwana akaja, akafungua milango ya gereza na akawatoa nje. Akawaambia, 20 “Nendeni, mkasimame Hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya uzima huu mpya.”
21 Waliposikia haya wakaenda Hekaluni alfajiri wakaendelea kufundisha watu.
Kuhani mkuu na wale waliokuwa pamoja nao walipowasili, alikusanya baraza na wazee wote wa Israeli wakatuma wale mitume waletwe kutoka gerezani.